Hepatitisi B

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Hepatitisi B
Mwainisho na taarifa za nje
SpecialtyInfectious diseases Edit this on Wikidata
ICD-10B16.,
B18.0-B18.1
ICD-9070.2-070.3
OMIM610424
DiseasesDB5765
MedlinePlus000279
eMedicinemed/992 ped/978
MeSHD006509

Hepatitisi B (homa ya ini B) ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vya hepatitis B vinavyoathiri ini, hivyo ni aina ya homa ya ini. Ni kimojawapo kati ya virusi vitano vinavyojulikana vya homa hiyo: A, B, C, D, na E. Virusi hivyo vinaweza kusababisha maambukizi makali na ya muda mrefu.

Watu wengi hawana dalili mwanzoni mwa maambukizi. Wengine huanza kuugua haraka kwa kutapika, kupata ngozi ya manjano, kuhisi uchovu, kutoa mkojo mweusi na kupatwa na maumivu ya fumbatio.[1] Mara nyingi dalili hizi hudumu kwa majuma machache na ni nadra maambukizi ya kwanza yasababishe kifo.[1][2] Inaweza kuchukua siku 30 hadi 180 kabla ya dalili kutokea.[1]

Kwa wanaoambukizwa wakati wa kuzaliwa, asilimia 90 hupata ugonjwa wa muda mrefu hepatitis B ilhali chini ya asilimia 10 ya wanaoambukizwa baada ya umri wa miaka mitano hupona.[3]

Wengi wa walio na ugonjwa wa muda mrefu hawana dalili; hata hivyo, sirosisi na saratani ya ini vinaweza kutokea.[4] Matatizo hayo husababisha vifo vya asilimia 15 hadi 25 ya walio na ugonjwa wa muda mrefu.[1]

Visababishi na utambuzi[hariri | hariri chanzo]

Virusi hivyo huenezwa kwa kutangamana na damu au viowevu vya mwili vinavyoambukiza. Hivyo mwanzoni ulijulikana kama hepatitisi ya seramu.[5] Maambukizi ya wakati wa kuzaliwa au kutokana na kutangamana na watu wengine utotoni ndiyo njia kuu ya kuambukiza hepatitisi B katika maeneo ambapo ugonjwa huo hupatikana sana. Katika maeneo ambapo ugonjwa huu ni wa nadra utumiaji wa sindano za mishipa na ngono ndizo njia kuu za kuambukiza.[1]

Visababishi vingine vya hatari vinajumuisha: kufanya kazi katika kituo cha afya, ubadilishaji wa damu, dialisisi, kuishi na mtu aliyeambukizwa, kusafiri katika nchi ambapo maambukizi ni mengi, na kuishi katika taasisi.[1][3] Kupiga chale na tiba sindano vilisababisha visa vingi katika miaka ya 1980; hata hivyo, hii imepungua kwa kuongezeka kwa utasa.[6]

Virusi hepatitis B hivyo haviwezi kuenezwa kwa kushikana mikono, kutumia vyombo sawa vya kula, kubusu, kukumbatia, kukohoa, kupiga chafya, au kunyonyesha.[3] Maambukizi haya yanaweza kutambuliwa siku 30 hadi 60 baada ya mtangamano. Utambuzi hasa ni kwa kupima damu kwa sehemu za virusi na kwa antibodi dhidi ya virusi hivyo.[1]

Kinga na tiba[hariri | hariri chanzo]

Maambukizi hayo yameweza kuzuiwa kwa chanjo tangu mwaka 1982.[7][1] Uchanjaji umependekezwa na Shirika la Afya Duniani katika siku ya kwanza ya maisha ikiwezekana. Dozi mbili au tatu zaidi zinahitajika baadaye kwa matokeo bora. Chanjo hii hufaulu kwa hadi takribani asilimia 95.[1] Takribani nchi 180 zilitoa chanjo hiyo kama sehemu ya programu za kitaifa kufikia mwaka wa 2006.[8] Pia imependekezwa kuwa damu yote ichunguzwe hepatitisi B kabla ya kumwekea mtu na kuwa kondomu zitumiwe kupunguza maambukizi.

Utafiti unalenga sasa kutengeneza vyakula vilivyo na dawa ya chanjo ya hepatitisi B (HBV).[9] Ugonjwa huu unaweza kuathiri sokwe wakuu wengine pia.[10]

Katika maambukizi ya kwanza, utunzaji unalingana na dalili alizonazo mhusika. kwa wale wanaopata ugonjwa wa muda mrefu dawa zinazodhibiti virusi kama vile tenofovir au interferon zinaweza kusaidia, hata hivyo, dawa hizi ni ghali. Ubadilishaji wa ini hutumiwa wakati mwingine kwa sirosisi.[1]

Uenezi[hariri | hariri chanzo]

Takribani thuluthi moja ya watu duniani wameweza kuambukizwa wakati mmoja maishani mwao, wakiwemo milioni 240  hadi milioni 350  walio na maambukizi ya muda mrefu.[11][1] Zaidi ya watu 750,000 hufariki kila mwaka kutokana na hepatitisi B.[1]

Ugonjwa huu sasa hupatikana sana katika Mashariki mwa Asia na Afrika Kusini kwa Sahara ambapo kati ya asilimia 5 na 10 ya watu wazima wana ugonjwa wa muda mrefu. Viwango kule Uropa na Amerika Kaskazini ni chini ya asilimia 1.[1]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. 1.00 1.01 1.02 1.03 1.04 1.05 1.06 1.07 1.08 1.09 1.10 1.11 1.12 "Hepatitis B Fact sheet N°204". who.int. July 2014. Iliwekwa mnamo 4 November 2014.  Check date values in: |date=, |accessdate= (help)
  2. Raphael Rubin; David S. Strayer (2008). Rubin's Pathology : clinicopathologic foundations of medicine ; [includes access to online text, cases, images, and audio review questions!] (toleo la 5. ed.). Philadelphia [u.a.]: Wolters Kluwer/Lippincott Williams &Wilkins. uk. 638. ISBN 9780781795166. 
  3. 3.0 3.1 3.2 "Hepatitis B FAQs for the Public — Transmission". U.S. Centers for Disease Control and Prevention (CDC). Iliwekwa mnamo 2011-11-29. 
  4. Chang MH (June 2007). "Hepatitis B virus infection". Semin Fetal Neonatal Med 12 (3): 160–167. PMID 17336170. doi:10.1016/j.siny.2007.01.013.  Check date values in: |date= (help)
  5. Barker LF, Shulman NR, Murray R, Hirschman RJ, Ratner F, Diefenbach WC, Geller HM (1996). "Transmission of serum hepatitis. 1970". Journal of the American Medical Association 276 (10): 841–844. PMID 8769597. doi:10.1001/jama.276.10.841. 
  6. Thomas HC (2013). Viral Hepatitis (toleo la 4th ed.). Hoboken: Wiley. uk. 83. ISBN 9781118637302. 
  7. Pungpapong S, Kim WR, Poterucha JJ (2007). "Natural History of Hepatitis B Virus Infection: an Update for Clinicians". Mayo Clinic Proceedings 82 (8): 967–975. PMID 17673066. doi:10.4065/82.8.967. 
  8. Williams R (2006). "Global challenges in liver disease". Hepatology (Baltimore, Md.) 44 (3): 521–526. PMID 16941687. doi:10.1002/hep.21347. 
  9. Thomas, Bruce (2002). Production of Therapeutic Proteins in Plants. uk. 4. ISBN 9781601072542. Iliwekwa mnamo 25 November 2014.  Check date values in: |accessdate= (help)
  10. Plotkin, [edited by] Stanley A.; Orenstein,, Walter A.; Offit, Paul A. (2013). Vaccines (toleo la 6th ed.). [Edinburgh]: Elsevier/Saunders. uk. 208. ISBN 9781455700905. 
  11. Schilsky ML (2013). "Hepatitis B "360"". Transplantation Proceedings 45 (3): 982–985. PMID 23622604. doi:10.1016/j.transproceed.2013.02.099. 
Makala hii kuhusu mambo ya tiba bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hepatitisi B kama sababu yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.