Elijah Masinde
Elijah Masinde (au Elija Masinde) alianzisha jumuiya ya Dini ya Musambwa kati ya Wabukusu huko magharibi mwa Kenya na kuiongoza tangu mwaka 1943 hadi mauti yake mwaka 1987.
Utoto na Ujana
[hariri | hariri chanzo]Masinde alizaliwa kati ya mwaka 1910-1912 katika eneo la Kimilili (leo: wilaya ya Bungoma) karibu na mlima Elgon. Ukoo wake ni Wabukusu ambao ni kati ya koo 18 za Waluhya.
Alipokuwa kijana alikuwa mchezaji wa mpira wa miguu. Aliwahi kuchezea timu za Kimilili Location Football team na Bukusu Union team.
Mnamo mwaka 1940 alipokuwa na umri wa miaka 30 hivi alianza kuonekana jinsi alivyochukizwa na utawala wa kikoloni.
Wito wa Musambwa
[hariri | hariri chanzo]Mwanzo wa 1943 aliota ndoto aliyosikia sauti ya Mungu. Kitabu cha James Bandi Shimanyula “Elijah Masinde and the Dini ya Musambwa” ( kufuatana na [1] Ilihifadhiwa 9 Septemba 2006 kwenye Wayback Machine.) kina taarifa ifuatayo:
“Usiku mmoja Aprili 1943 Mungu alimjia Masinde alipolala usingizi akamwambia:
"Mimi ni Wele wa Musambwa. Ninasema kutoka Sayoni kwenye mlima mtakatifu wa Elgon. Nimekuita wewe Masinde uwe kiongozi wa Dini ya Musambwa. Uwaambie Wabukusu wote kumwamini roho wa Musambwa. Watakuwa na chakula tele. Wafuasi wa Musambwa wasivae nguo za Mzungu. ... Nitawaponya walio bubu, vipofu na walemavu. Mnapaswa kuchukia Wazungu. Utakapofika mwisho wa dunia nitafungua mlango na wewe Masinde pamoja na wafuasi wa dini ya Musambwa mtaingia mbinguni."
Kitabu kinataja maneno ya Masinde mwenyewe: “Mungu ameniteua kuwa msemaji wake. Ameniambia kuwaunganisha Waafrika na kuwafudisha neno lake. Nimeongea na Mungu mara nyingi. Ananiahidi ya kwamba mimi nitakuwa mtu wa pekee atakayebaki wakati dunia hii itakapokwisha."
Nabii na Kiongozi wa Dini ya Musambwa
[hariri | hariri chanzo]Masinde alianza kuhubiri mbele ya Wabukusu wenzake juu ya wito wake. Alipowaambia wasilipe kodi na kuchoma vipande vyao vya kitambulisho alitupwa jela na Waingereza. Baada ya kutoka alijenga jumuiya ya "Dini ya Musambwa" na kuwa na wafuasi wengi kati ya Waluhya.
Masinde alikuwa na uwezo na kipaji kikubwa cha kuhubiri. Alihubiri bila woga akiwataka wakoloni kuondoka Afrika na kuacha kila walichokikuta. Aliwataka pia kuwaacha Waafrika kuabudu kufuatana na mila zao. Mara ya kwanza kwa Masinde kuonyesha chuki yake kwa utawala wa kikoloni ni pale alipoamua kuacha kazi aliyokuwa akifanya chini ya utawala huo kwa kutotaka kutumikia wakoloni. Cheo chake kilikuwa ni "Native Tribunal Process Server."
Mara ya kwanza kabisa kufungwa ilikuwa ni mwaka 1945. Serikali ya kikoloni ilishindwa kumwelewa Masinde na kuamua kumchukilia kama mwendawazimu na hivyo kumweka katika hospitali ya vichaa ya Mathare kwa maiaka miwili. Mwaka 1948 Masinde alishtakiwa kwa kosa la uhaini na kupelekwa uhamishoni huko Lamu ambako alikaa hadi mwaka 1961. Baada ya kuachiliwa huru, Masinde aliendelea na shughuli za kidini na kisiasa. Alikuwa akiunga mkono chama cha Kenya African National Union (KANU) jambo ambalo lilimpunguzia umaarufu wake kwakuwa watu wengi wa eneo analotoka walikuwa wakiunga mkono chama cha Kenya African Democratic Union (KANU).
Hata hivyo Rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta alisajili jumuiya yake ya Dini ya Musambwa na hivyo kutambulika rasmi kwa mara ya kwanza hapo mwaka 1964.
katika uhai wake Masinde alifikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi mbalimbali. Baada ya uhuru wa Kenya alifungwa jela tena na serikali ya Jomo Kenyatta kwa miaka 15. Serikali mpya ya Rais Daniel Arap Moi ilimrudishia uhuru wake akaishi maisha ya utulivu huko Kimilili hadi kifo chake tarehe 9 Juni 1987.
Wafuasi wa Dini ya Musambwa wamepungua lakini bado wako. Mara mbili kwa mwaka hupanda mlima Elgon na kufanya ibada ya sadaka wakichinja mwanakondoo, hua au dume wa ng'ombe.
Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- Makala juu ya uinjilisti wa kikristo inayotaja kitabu cha Shimanyula Ilihifadhiwa 9 Septemba 2006 kwenye Wayback Machine.
- Makala fupi ya New York Times wakati wa kifo cha Masinde
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Elijah Masinde kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |