Yo Rap Bonanza

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Yo Rap Bonanza ni tamasha la kila mwaka lililoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 nchini Tanzania, kuonyesha vipaji vya kurap. Liliandaliwa na Dj Kim na The Boys Promotion.[1]

Onyesho la kwanza lilifanyika mwaka wa 1993 na la pili na la mwisho lilikuwa mwaka wa 1995. Yo Rap Bonanza linatambulika kama shindano la kwanza la hip hop nchini Tanzania. Mamia ya wasanii, hasa kutoka jijini Dar es Salaam walichuana vikali kwa muda wa siku mbili katika ghorofa ya saba ya hoteli ya New Africa.[2]

Shindano la Yo Rap Bonanza linatajwa kwamba liliweka misingi mipya ya muziki wa Hip Hop nchini Tanzania japokuwa nyimbo za wasanii wengi walizokuwa wakiimba zilikuwa ni katika lugha ya Kiingereza, wengi wakikopi staili za makundi ya Marekani, mashairi ya Kiswahili yalionesha kuwavutia watu wengi sana waliofurika kwenye tamasha hilo.[3][4]

Wasanii wengi walipata umaarufu baada ya kushiriki Yo Rap Bonanza. Saleh J, alikua mmoja wa wasanii wa muziki wa hip-hop wanaotambulika na kuheshimika mara baada ya kushinda shindano hilo.[5][6] Ni katika tamasha hilo ndipo vipaji vingine vilipoibuka, wakiwemo wasanii kama Nigga One, Eazy B, D Rob, KBC, Y Thang, Killa B na wengine wengi.[7]

Baada ya Yo! Rap Bonanza kumalizika, wasanii waliofanya vyema kwenye mashindano hayo, waliungana na kuunda makundi mbalimbali, likiwemo Kwanza Unit, chini yake Ramadhan Mponjika ‘Chief Rhymson’ akiwa na Kibacha (KBC), D-Rob na Eazy B, baadaye wakaongezeka wanachama wengine kama Bugzy Malone, Papa Sav, Abbas Maunda, Baraka, Ndoti, Fresh-G, Y-Thang na Adili. Pia lilizaliwa kundi lingine, Deplomatz lililokuwa likiundwa na Saigon na Dola Soul (Balozi). Mbali na makundi, pia wasanii wengine walianza kufanya kazi kama wasanii binafsi, wakiwemo Joseph Mbilinyi kipindi hicho akiitwa II Proud kabla ya baadaye kuja kubadili jina na kuitwa Mr II (Sugu).

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Dar Es Salaam: Histories from an Emerging African Metropolis edited by James R. Brennan, Andrew Burton, Yusufu Qwaray Lawi, British Institute in Eastern Africa page 257 and page 261
  2. "Yo Rap Bonanza". www.liquisearch.com. Iliwekwa mnamo 2022-07-31. 
  3. Lemelle, Sidney J. "Ni wapi Tunakwenda: Hip Hop Culture and the Children of Arusha". In The Vinyl Ain’t Final: Hip Hop and the Globalization of Black Popular Culture, ed. by Dipannita Basu and Sidney J. Lemelle, 230-54. London; Ann Arbor, MI: Pluto Press
  4. Clark, Msia Kibona. (2013). The struggle for hip hop authenticity and against commercialization in Tanzania. Journal of Pan African Studies, 6 (3), 5-21.
  5. Cabidon (2020-08-28). "The Origin Of Bongo Flava". Gilox (kwa en-US). Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-03-26. Iliwekwa mnamo 2022-07-31. 
  6. "Afropop Worldwide | Tanzanian Hip-Hop: A Primer". Afropop Worldwide (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2022-07-31. 
  7. "Hip-hop in Tanzania". Music In Africa (kwa Kiingereza). 2015-03-03. Iliwekwa mnamo 2022-07-31.