Benki ya Dunia
Benki ya Dunia ni taasisi ya kimataifa yenye shabaha ya kusaidia maendeleo ya nchi za dunia. Si benki ya kawaida. Inashirikiana na Umoja wa Mataifa na hasa Shirika la Fedha la Kimataifa lakini si chini ya UM moja kwa moja. Ni mali ya nchi wanachama 185 zinazopigia kura katika mikutano yake kulingana na thamani ya hisa zao katika rasilmali ya benki.
Muundo wa Benki ya Dunia
Benki ya Dunia ina matawi mawili ambayo ni
- Benki ya Kimataifa ya Marekebisho na Maendeleo (International Bank for Reconstruction and Development - IBRD) iliyoanzishwa mwaka 1945 inayojulikana kama "Benki ya Dunia" hasa.
- Shirikisho la Kimataifa la Maendeleo (International Development Association - IDA) iliyoanzishwa mwaka 1960.
Taasisi za ziada ambamo kila nchi mwanachama inapaswa kuingia pia ni
- Muungano wa Kimataifa wa Fedha (International Finance Corporation IFC),
- Shirika la Uthibiti wa Uwekezaji (Multilateral Investment Guarantee Agency MIGA) na
- Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Mizozo ya Uwekezaji (International Centre for Settlement of Investment Disputes ICSID).
Makao makuu yapo Washington DC nchini Marekani. Kikatiba mwenyekiti wa benki ni mtu wa Marekani.
Hisa na kura
Maazimio hufuata kura za wanachama zinazolingana na idadi ya hisa za nchi hizo katika rasilmali ya benki (kwa mabano: IFC). Nchi zenye kura nyingi ni:
- Marekani 16,39% (23,68%)
- Japani 7,87% (5,88%)
- Ujerumani 4,49% (5,37%)
- Ufaransa 4,3% (5,04%)
- Uingereza 4,3% (5,04%)
(Hali ya mwaka 2004)
Shabaha ya kazi
Benki (IBRD) inalenga kutoa mikopo kwa nchi zilizoendelea kiasi na pia nchi maskini zenye uwezo wa kulipia mikopo. Shirikisho la Maendeleo (IDA) inaangalia mahitaji ya nchi maskini kabisa.
Kwa jumla taasisi za Benki ya Dunia hutoa mikopo kwa riba ndogo au hata zisizo na riba halafu pia misaada zisizorudishwa kwa nchi maskini kwa kusudi la kujenga elimu, afya, barabara na mawasiliano.
Historia
Benki ilianzishwa mwaka 1945 baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Shabaha ilikuwa kusaidia nchi za Ulaya zilizoharibiwa katika vita. Mkopo wa kwanza wa milioni USD 250 ulitolewa kwa Ufaransa.