Wikipedia:Vita ya uhariri

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Fitina hutokea!
Njia hii afadhali!

Vita ya uhariri inatokea kama wanawikipedia hawawezi kuelewana juu ya makala fulani.

Kutokea kwa vita ya uhariri[hariri chanzo]

Mara nyingi vita ya uhariri inaanza kama mtumiaji A anaona kile anachosoma kama makosa katika makala fulani. Anaamua kusahihisha kosa lile au kuandika makala yote upya. Hatua hii inaweza kumkasirisha mtumiaji B aliyeanzisha makala na haoni kosa lolote ndani yake.

Kama mtumiaji B anaamua kurejesha makala jinsi ilivyokuwa mwenzake A ataibadilisha tena na kadhalika. Vita imeshaanza. Kuna wanawikipedia wanaotumia siku mfululizo kwa njia hii.

Kuepukana na vita ya uhariri: Kujadiliana kwanza[hariri chanzo]

Katika wikipedia kubwa michezo ya aina hii hutokea mara nyingi. Kwa bahati nzuri wikipedia ya Kiswahili imeweza kuepukana na balaa ile hadi sasa (kufikia makala 15,000).

Shauri bora ni kujadiliana kwanza. Ukiona makala yenye makosa fuata hatua hizi:

  • kama ni jambo dogo sahihisha tu; kama mhariri aliyetangulia ana neno ndiye anaweza kuingia katika majadiliano. Labda atakueleza kumbe haikuwa kosa ili mpate kuelewana.
  • kama ni makala iliyowekewa kazi nyingi tayari angalia kwenye "historia" ni nani aliyehariri ukurasa hadi sasa.
  • kama ni mtumiaji aliyejiandikisha umwandikie kwenye ukurasa wake wa majadiliano, pia andika hoja kwenye ukurasa wa majadiliano wa makala yenyewe ("Naona habari ya ABC si sawa naona iwe hivyo DEF kwa sababu hizo za XYZ").
  • subiri angalau siku 1 heri 2 kama unapata jibu
  • halafu badilisha jinsi unavyoona kama huna majibu

Kumaliza vita kama inatokea: Wakabidhi[hariri chanzo]

Hata ukifuata hatua hizi vita bado inaweza kutokea. Ukishindwa kuelewana na wahariri wenzako lete tatizo kwenye ukurasa wa jumuiya. Hapa anzisha kichwa kipya na eleza kwa kifupi tatizo.

Wakabidhi wataangalia tatizo hili na kushauri. Unaweza pia kumwandikia mkabidhi fulani moja kwa moja kwenye ukurasa wake wa majadiliano.

Labda mkabidhi atalinda ukurasa kwa siku kadhaa na kuzuia mabadiliko hadi wapinzani wako tayari kuelewana.