Wikipedia:Makala ya wiki/Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

(maelezo ya picha)

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) (ing. Tanzania People's Defense Force TPDF) ni jeshi lililoanzishwa mnamo mwezi wa Septemba katika mwaka wa 1964. Ilichukua nafasi ya jeshi la Tanganyika Rifles lililorithiwa na ukoloni wa Kiingereza. Chanzo cha jeshi nchini Tanzania kilikuwa jeshi la kikoloni la Uingereza katika Afrika ya Mashariki. Mwaka 1919 Uingereza ilikabidhiwa utawala juu ya Tanganyika na Shirikisho la Mataifa. Baada ya uhuru mwaka 1961 vikosi vya King's African Rifles katika Tanganyika vilibadilishwa jina na kuwa Tangayika Rifles (TR). Pamoja na kubadilika jina Tanganyika Rifles ilikuwa na muundo sawa na Kings African Rifles (KAR). Maafisa wenye mamlaka bado walikuwa Waingereza, pamoja na Waafrika watano waliopandishwa cheo wakati wa uhuru na kupokea mafunzo katika vyuo vya kijeshi vya Kiingereza. Jeshi jipya lilipangwa katika vikosi viwili vyenye makao makuu huko Dar es Salaam na Tabora. Afisa mkuu alikuwa Brigedia Jenerali Patrick Sholto Douglas. Kwa jumla kulikuwa na hali ya kutoridhika kati ya askari wa TR. Sababu yake ilikuwa matumaini ya kwamba uhuru ungeleta mabadiliko makubwa zaidi na nafasi za kupanda cheo baada ya kuondoka kwa maafisa wazungu. Lakini maafisa Waingereza waliendelea kuajiriwa na serikali ya Nyerere na tofauti kubwa katika mapato na hali ya makazi ya Wazungu na Waafrika ziliendelea. ►Soma zaidi