Nenda kwa yaliyomo

Utawala huria

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Bendera ya waanakisti katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Hispania mnamo 1937
Mikhail Bakunin alikuwa mfuasi mashuhuri wa utawala huria wakati wa karne ya 19

Utawala huria (pia: uanakisti kutoka Kigir. ἀναρχία anarkhia "bila utawala") ni itikadi ya kisiasa inayokataza kila aina ya utawala wa wanadamu juu ya wanadamu wengine. Haikuibali kipaumbele kwa "wakubwa" wa kila aina juu ya watu wengine.

Wafuasi wa utawala huria hutaka kujenga jamii kama ushirikiano wa hiari kati ya watu huru ama watu mmoja-mmoja walio huru au vikundi vya watu vinavyoshirikiana kwa hiari. Wafuasi wa utawala huria wanataka kuondoa mfumo wa ngazi ya madaraka unaowapa maafisa wa juu uwezo na hali ya kuwamulia wengine wa ngazi za chini. Kutokana na msingi huu wanakataa dola na vyombo vyake kama serikali hasa kama ni serikali ya kidikteta au ya kifalme.

Menginevyo kuna mikondo mingi kati ya vikundi mbalimbali wa wafuasi wa utawala huria. Wengine wanakazia zaidi nafasi ya mtu binafsi wakitazama jamii kama jumla ya watu binafsi; wengine huona umuhimu wa kugawa jamii katika vikundi vingi ambako kila mtu anajiunga na kundi na vikundi vinashirikiana kwa pamoja kwa hiari na kwa kupatana.

Kwa jumla uanakisti au utawala huria ni mwendo ulioanza katika Ulaya wakati wa karne ya 19 katika mazingira ya utawala mkali wa wafalme na makabaila. Hapo waanakisti wa kwanza walijiuliza eti ni msingi gani ambako mfalme au mkabaila anadai utii wakajibu hakuna kwa sababu kila mtu ni sawa na huru si halali kumlazimisha.

Waanakisti Warusi hasa walijaribu kumpindua tsar kwa njia za kigaidi kwa kumtupia mabomu au kwa bunduki.

Uanakisti uliendelea katika nchi penye udikteta; katika Hispania wafuasi wa utawala huria walikuwa harakati kubwa sana kati ya wafanyakazi wa viwandani katika nusu ya kwanza ya karne ya 20.

Lakini katika nchi penye demokrasia palikuwa na wafuasi wachache tu wa itikadi hiyo. Hadi leo waanakisti huwa na vikundi vidogo kati ya wanafunzi na wasoma lakini bila athira kubwa ya kisiasa.