Usiku wa Yalda

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Faili:PICHA YA USIKU WA YALDA.jpg
Vyakula vya Yalda.

Usiku wa Yalda au Usiku wa Chelleh ni moja kati ya sherehe kongwe zaidi za Kiirani. Sherehe hiyo hufanyika ikiwa ni kusherehekea usiku mrefu zaidi wa mwaka, kisha hufuata kipindi cha mchana kuwa mrefu zaidi katika nusu ya kaskazini mwa dunia. Usiku huo huwa baina ya kipindi cha kuzama jua tarehe 30 mwezi wa Aazar ambayo ni siku ya mwisho ya kipindi cha msimu wa mapukutiko (Fall) hadi kuchomoza jua katika siku ya kwanza ya mwezi Disemba, ambayo huwa siku ya kwanza ya kuanza kipindi cha msimu wa baridi kali (Winter).

Kwa kawaida katika usiku huo, familia za Kiirani huandaa na kula chakula kizuri cha usiku pamoja na matunda na hasa tikiti maji na komamanga. Baada ya hapo, wanafamilia hula vitafunwa tofauti, hutoa visa mbalimbali na kisha wakubwa wa familia huwasomea wanafamilia baadhi ya beti za mashairi za malenga Hafez. Kwa maelfu ya miaka sasa, Wairani wamekuwa wakisherehekea usiku huo wa mwisho wa msimu wa mapukutiko kwa kutekeleza mila na desturi katika miji mbalimbali nchini Iran, usiku unaotajwa kuwa ni mrefu zaidi wa mwaka na wenye giza nene mno.

Historia inaeleza kuwa, sherehe ya usiku wa Yalda ilianza zama za kale mno, na wala haifahamiki ni muda gani hasa ilipoanza, lakini wanaakiolojia walio wengi wanaeleza kuwa, usiku huo ulianza yapata miaka elfu saba iliyopita. Imetajwa kuwa, vyombo vilivyotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi kabla ya kipindi cha historia, imeonyesha kuwepo michoro ya wanyama inayonasibishwa na miezi ya Kiirani kama vile nge na kondoo dume ndani ya vyombo hivyo. Pamoja na maelezo hayo yote, jambo lililokuwa wazi ni hili kuwa, usiku wa Yalda ulitambuliwa rasmi yapata miaka 500 kabla ya kuzaliwa Kristo, na historia yake kuingizwa kwenye kalenda rasmi ya Wairani wa kale katika zama za Daryush wa Kwanza, kalenda ambayo inajumuisha kalenda za Wamisri na Wababeli.

Kwa muda mrefu, nambari 40 imekuwa na nafasi maalum katika utamaduni wa Kiirani. Wairani wa zamani waliugawanya msimu wa baridi kuwa "Chelleh Kubwa" na "Chelleh Ndogo", ambao ulikuwa na sehemu mbili za siku arobaini. Usiku wa mwisho wa mwezi wa Aazar huitwa chelleh: kwa sababu ni mwanzo wa chelleh kubwa inayoambatana na msimu wa baridi kali. Baada ya siku arobaini hufanyika sherehe ya kumalizika chelleh kubwa na kuanza chelleh ndogo. Kwa mujibu wa mila na desturi za kale za usiku wa Yalda, iingiapo tarehe Mosi Disemba, wafalme wa Kiirani  waliweka chini mataji yao ya kifalme, huelekea jangwani wakiwa wamevalia nguo nyeupe na kukaa juu ya mazulia meupe. Walinzi, mabawabu wote kwenye kasri ya mfalme, wahudumu na watumwa hupewa uhuru wa  kwenda mjini na kuishi kama watu wengine; na watu wote iwe  mfalme, waziri au watu wa kawaida huwa sawa na wenye kulingana.

Leo hii sherehe ya usiku wa Yalda huadhimishwa na Wairani kwa kukaa pamoja katika usiku huo, na baada ya wanafamilia kukusanyika wakuu wa familia huanza kueleza visa na hekaya za zamani sanjari na kula matikiti maji, komamanga, jamii ya karanga, vitafunwa na anuwai nyingine za matunda, aghalabu matunda yanayotumika ni yale yenye mbegu nyingi. Kwa vile tikiti maji na komamanga ambayo yana rangi nyekundu, huchukuliwa kama viwakilishi wa jua wakati wa usiku.

Wakati unaopendwa na wengi katika usiku huo, unapowadia ni wakati wa kutafuna jamii ya karanga, ambayo ni  mchanganyiko kama vile korosho, karanga, pistachio, lozi na matunda yaliyokaushwa.

Kitanga cha usiku wa Yalda kinaongeza uzuri wa usiku huu mara dufu. Kitanga hicho hutandikwa na kuwekwa matunda ya aina mbalimbali, jambo linalothibitisha uwepo wa usiku huo. Kitanga cha usiku wa Yalda pia hupambwa na ishara nyingi, mfano komamanga linaashiria baraka na furaha, tikiti maji nalo linaashiria jua, joto la majira ya joto na baraka na jamii ya karanga na vitafuno kama vile, pistachio, lozi, korosho, matunda yaliyokaushwa na kadhalika, vyote hivyo huandaliwa kwenye usiku huo. Kwa kawaida, matunda ya  msimu wa mapukutiko na vitafunwa  vitamu   huwekwa pambizoni mwa kitanga cha usiku wa chelleh.

Kwa vile watu wa kale walikuwa wakiwasha moto kama ishara ya kupata joto na mwangaza, vilevile baadhi yao walikuwa wakitumia njia hiyo ili kuepukana na giza; kwa minajili hiyo husherehekea usiku huo kwa kuwasha moto ili sherehe yao ifane zaidi sanjari na kupata mwangaza wa moto huo.