Nenda kwa yaliyomo

Sadd

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Eneo la Saaa katika Sudani Kusini (picha ya satelaiti wakati wa ukame 1993)

Sadd (pia: "Sudd" katika tahajia ya Kiingereza, kutoka Kar. سد sadd = kizuizi) ni eneo kubwa la mabwawa matope katika Sudan Kusini linalopitiwa na mto Nile.

Ukubwa na Sadd unabadilika na kiwango cha maji yanayotoka Ziwa Viktoria. Kwa wastani urefu wake ni 320 km kutoka kaskazini hadi kusini na upana waka kati ya upande wa mashariki hadi magharibi ni 240 km; eneo lake linalofunikwa kwa maji huwa kati ya 20,00 na 130,000 km², kwa wastani juu ya 30,000 km². Miji inayopakana eneo lake ni Bor upande wa kusini, Wau na Bentiu upande wa magharibi na Malakal upande wa kaskazini.

Ekolojia

[hariri | hariri chanzo]

Sadd kwa jumla ni eneo lenye rutba kubwa. Mimea asilia ni pamoja na mafunjo, tete, na mimea mengi mengine. Kuna pia mabaki ya misitu ya mvua penye miti ya mbambakofi kando yake. Penye maji mengi na ya kudumu kuna mimea inayoelea juu ya maji ikishikwa na mizizi mirefu hadi tako la bwawa; kama maji yanapanda juu vipande vikubwa vya mimea hii vinasukumwa na kukata mizizi yao vikifuata mwendo wa maji kama visiwa vya kuelea vyenye urefu hadi 30 km. Visiwa hivi vya kuelea kwa karne nyingi vilikuwa kizuizi kikali cha usafiri kwa mashua na maboti kwenye Nile vikaipa eneo hili jina la "sadd" yaani kizuizi vikizuia usafiri mtoni.

Maeneo makubwa yanafunikwa kwa manyasi ya aina nyingi yanayokuwa marefu wakati wa mvua na mafupi wakati wa ukame. Sehemu za sadd zimelimwa kwa mashamba na wakazi wa eneo.

Sehemu za kando za Sadd ni muhimu kwa wafugaji wa Sudan Kusini wanaopeleka wanayama hapa wakati wa ukame.

Hidrolojia

[hariri | hariri chanzo]

Eneo la Sadd halina mtelemko mkubwa kwa hiyo maji ya Nile hutembea polepole sana. Mkasi mdogo husasabisha maji kukaa kwa wiki nyingi kwenye eneo kubwa. Eeno kubwa la uso wa maji katika mazingira yenye joto kali husababisha maji mengi kuvukiza na uvukizaji ni mkubwa kiasi cha nusu ya maji yote yanayofika Sadd kupotea.

Tangi mwanzo wa karne ya 20 serikali iliona hii ni tatizo kwa sababu uvukizaji mkubwa ktika Sadd unapunguza kiwango cha maji yanayofikia kaskazini hasa Misri penye watu wengi.

Wakoloni Waingereza walianza kuchimba lalio la Nile kupitia eneo la Sadd mnamo mwaka 1900 wakilenga kuunda njia kwa meli za mtoni kupita hapa lakini mfereji huu haukusaidia kupita kwa maji haraka zaidi.

Kwa hiyo kumekuwa na mipango tangu miaka ya 1930 kuchimba mfereji mkubwa kando la Sadd kwa nia ya kuharakisha mwendo wa maji na kupunguza upotevu wa uvukizaji. Mfereji wa Jonglei yenye urefu wa 360 km ungeunganisha miji ya Bor na Malakal na kubeba takriban 20% ya maji yanayoingia katika Sadd kutoka kusini. Kazi zilianzishwa mwaka 1974 lakini zilikwama 1984 kutokana na hali ya vita katika Sudan Kusini. Takriban 240 km zimeshachimbwa.

Kuna mashaka kuhusu matokeo kwa Sudan Kusini kama mfereji unakamilishwa. Serikali ya Sudan Kusini inasubiri utafiti wa kisayansi kabla ya kuendelea na shughuli. Kuna hofu ya kwamba hasara ya kiekolojia katika mazingira ya Sadd ya sasa inaweza kuwba kuliko faida. Misri na Sudan Kaskazini zinalenga kukamilisha mradi kwa sababu wanaona faida ya kuongezeka kwa maji huko kwao.

Tazaa pia

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu: