Dogodogo Center

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Dogodogo Center ni shirika lisilo la kiserikali linashughulika na watoto walio katika mazingira magumu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania. Inasimamiwa na shirika la masista wa Maryknoll.

Mwanzilishi wa Dogodogo Center ni Sista Jean Pruitt. Sista Jean Pruitt alianzisha Dogodogo Center mwaka 1993 baada ya kuona watoto wakirandaranda mitaa ya Posta na kulala kando ya barabara bila ya msaada wowote. Sista Jean aliamua kuanza namna ya kuwasaidia watoto hawa na ndipo alipopata wazo la kuwasaidia kwa kuwapatia mahitaji muhimu ya matibabu na chakula.

Miaka ya 1993 tatizo la watoto wa mitaani halikuwa kubwa nchini Tanzania hivyo haikuwa rahisi kwa watu wengine kuona shida hii ambayo Sista Jean Pruitt aliweza kuiona. Sr. Jean Pruitt alitafuta misaada mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kuwaandikia wafadhili mbalimbali juu ya shida ya watoto wa mitaani na wengi walielewa na kufadhili.

Dogodogo Center ina vituo vifuatavyo

  • kituo cha kukutana na watoto wanaoishi barabarani kilichopo kwenye kitovu cha Dar es Salaam. Inaweza kupokea hadi watoto 100 kila siku wanaofika kutoka barabarani. Hapa wanaweza kuoga, kuosha nguo na kujipikia chakula. Wafanyakazi wa kituo wanafahamiana na watoto wakiandaa kuchagua watoto 50 kila mwaka wanaoondolewa barabarani na kupelekwa mahali wanapoendelea na masomo ya shule au mafunzo ya kazi za kujitegemea.
  • kituo cha Kigogo ambako wanatunzwa watoto 30 wanaosoma kwenye shule za msingi. Wanaofaulu vizuri wanapewa msaada kusoma sekondari.
  • kituo cha mafunzo cha Bunju Multipurpose Training Centre (MTC). Hapo wanaishi vijana 100 wanaofuata kozi ya miaka 2 katika fani kama useremala, ushonaji au sanaa za muziki na maigizo.


Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]