Cuban Marimba Band
Cuban Marimba Band | |
---|---|
Juma Kilaza na Cuban Marimba.
| |
Maelezo ya awali | |
Asili yake | Morogoro, Tanzania |
Aina ya muziki | Muziki wa dansi |
Cuban Marimba Band ilikuwa bendi ya muziki wa dansi kutoka Morogoro, Tanzania. Bendi ilianzishwa na Salum Abdallah Yazidu (SAY) mnamo 1948 ikiwa na jina la Kihispania maarufu kama La Paloma.
Historia yake
[hariri | hariri chanzo]Kuanzia miaka ya 1920 mpaka 1940, wanamuziki na wapenzi wa muziki walifuatilia sana muziki kutoka Cuba kupitia sahani za santuri za wakati huo. Kulikuwa na vikundi kama Trio Matamoros na Sexteto Habanero, ambao walitoa santuri zikiwa na namba zinazoanzia GV1, GV2 na kuendelea na kupata upenzi mkubwa katika sehemu kubwa ya Afrika. Ni vikundi hivi ambavyo viliingiza mitindo kama rhumba, Bolelo, Chacha na kadhalika, na muziki huu kuwa ndio mbegu ya muziki wa dansi wa Afrika mpaka leo. Hali halisi bendi za muziki wa dansi zingepata mengi ya kimapinduzi kama zingeweza kusikiliza na kuelewa muziki wanaoupiga kiini chake ni nini.
Nia ya kutaka kujua muziki wa Cuba na kuanzishwa kwa Cuban Marimba
[hariri | hariri chanzo]Kutokana na hamu hiyo ya kuujua na kuupiga muziki wa kiCuba kisawasawa, Salum Abdallah aliwahi kutoroka kwao Morogoro akakimbilia Mombasa ili apande meli aende Cuba, bahati mbaya safari yake iliishia Mombasa, baada ya kuibiwa fedha zake na kulazimika kuanza kazi ya kuchoma mishkaki katika jiji hilo, ambako alianza kupata shida lakini kwa kuwa baba yake alikuwa mwarabu, Ushirika wa waarabu wa Mombasa walimtaarifu mzee huyo kuhusu alipo mwanae na alimfuata na kumrudisha Morogoro.
Salum Abdallah Yazidu aliyefahamika sana kama SAY, mwaka 1948 alianzisha bendi yake akaiita La Paloma, ambalo ni jina la wimbo maarufu ambao uliotoka Cuba ukiwa na jina hilo lenye maana Njiwa, wimbo huu unaendelea kupigwa hadi leo ukiimbwa na kurekodiwa kwa lugha mbalimbali duniani, marehemu Elvis Presley akiwa moja wapo aliyewahi kurekodi wimbo uliotokana na huo wa La Paloma, hata hapa Tanzania bendi nyingi huzisikia zikipiga wimbo huu na kuweka maneno yake ya papo kwa papo hasa kabla dansi rasmi halijaanza. Bendi ya La Paloma ndio ilikuja kuwa Cuban Marimba Band, Salum Abdallah aliiongoza bendi hiyo mpaka kifo chake 1965.
Kifo cha Salum Abdallah na mikoba kuendelezwa na Juma Kilaza
[hariri | hariri chanzo]Alhamisi tarehe 18 Novemba, 1965 ilikuwa siku yenye hekaheka kubwa mjini Morogoro, ugeni mkubwa ulikuwa unasubiriwa katika mji huo. Mheshimiwa Julius Kambarage Nyerere na Mheshimiwa Rashid Mfaume Kawawa, viongozi wakuu wa nchi wakati huo, walikuwa wakisubiriwa na wananchi wa hapa katika sherehe ya kufungua Chuo cha Kilimo ambacho kwa sasa kinajulikana kama SUA (Sokoine University of Agriculture). Pamoja na wageni hao pia alitegemewakuweko aliyekuwa Mbunge wa Morogoro mjini wakati huo Mheshimiwa Oscar Kambona.
Bendi mbili kubwa maarufu za pale Morogoro mjini zote zilitegemea kupiga siku hiyo, na pia zilipangiwa kutembelewa na viongozi hao. Kutokana na ushindani mkubwa wa bendi hizo wanamuziki na washabiki wa bendi hizo walikuwa roho juu kusubiri mpambano wa usiku huo. Kwenye muda wa saa kumi na mbili jioni baada ya shamrashamra za kupokea viongozi kwisha bwana Ramadhan Mdidi aliyekuwa msaidizi wa mmoja wa madreva wa Salum Abdallah alikuja kumueleza mkuu wao huyo kuwa moja ya gari lake limenasa kwenye mchanga katikamkondo wa mto walikokuwa wakichimba mchanga, kwa hiyo ilikuwa busara kuliondoa gari usiku uleule au la mvua ingenyesha gari lingeweza kuchukuliwa na maji. Salum Abdallah akaagiza gari likavutwe. Salum Yazidu Abdallah ndiye aliyekuwa kiongozi muimbaji wa bendi ya Cuban Marimba, pia alikuwa ana malori kadhaa aliyokuwa akiyatumia pia katika mradi wa kujenga nyumba za National Housing pale Morogoro.
Salum akamtuma mwanamuziki wake Waziri Nyange atangulie kwenye ukumbi ambako wangepiga muziki ili kutyuni vyombo tayari kwa onyesho la usiku ili yeye aende na lori jingine kwenda kuvuta gari lililonasa kwenye mchanga. Siku hiyo Cuban Marimba walikuwa wapige muziki Community Center wakati wenzao Morogoro Jazz Band walikuwa wapige Kichangani. Kiasi cha saa moja hivi mmoja wa waliokuwemo kwenye lori lililoondoka na Salum Abdallah alirudi mbio nyumbani na kuwataarifu kuwa kumetokea ajali na Salum ameumia. Ajali hii ilikuwa ya ajabu na imekuwa daima ikileta maneno kwa walioikumbuka. Kwa maelezo ya waliokuwepo, giza lilikuwa limekwisha ingia na wakati lori likikariba Msamvu taa zilizimika ghafla na gari ikayumba lakini taa zikawaka tena, kiasi cha waliokuwemo kuanza kucheka, lakini kicheko chao kilikatika ghafla baada ya kugundua kuwa mlango wa upande aliokuwa amekaa Salum ulikuwa wazi naye amedondoka. Walirudi nyuma na kumkuta akiwa kalala barabarani akiugulia kwa maumivu.
Mzungu mmoja alipita wakati uleule na gari dogo akawapa lifti watu wawili toka kwenye lile lori, mmoja akaenda nyumbani kwa Salum kutoa habari na mwingine akaenda kuchukua taxi iliyomchukua majeruhi mpaka hospitali. Hivyo wote waliopata habari wakakimbilia hospitali wakamkuta mwenzao anaugulia maumivu, madaktari walimuomba anyooshe mikono na kisha miguu alipoweza, wakaamini hajavunjika bali ni maumivu ya juu juu ambayo yangeisha, kiasi cha kumruhusu arudi kwake na awahi matibabu kesho yake asubuhi. Salum mwenyewe akawaambia wenzie wafungue vyombo wasipige dansi siku ile, wengi wakakesha nae. Usiku kucha ulikuwa wa maumivu makubwa, asubuhi mgonjwa alipelekwa hospitali akafanyiwa upasuaji ikagundulika alivunjika kiuno na mifupa kupasua kibofu cha mkojo, jambo ambalo kutokana na kuchelewa kugundulika lilikuwa ni baya sana. Kama saa 7 mchana alitolewa chumba cha upasuaji na wenzie waliokuwa wakisubiri wakaambiwa waende makwao wakale vizuri ili waje baadaye kutoa damu kwa ajili ya mgonjwa.
Wakatoka kwa furaha wakijua mambo yatakuwa mazuri. Walielekea kwenye klabu yao wakatengeneza chakula na kula kwa furaha. Kulianza hata kuwa na utani kuwa ,’Mwarabu akipona atatoa kibao cha kikali cha tukio hilo’ Ikumbukwe kuwa baba yake Salum alikuwa Mwarabu halisi. Lakini ilipotimu saa kumi jioni taarifa ikaja kuwa Salum amefariki. Watu wakaanza kumiminika nyumbani kwake, wakakuta hata maiti imeshafikishwa kwake na imewekwa katika chumba kimoja ambacho kilikuwa kimetayarishwa kwa ajili ya fremu ya duka. Inasemekana baada ya Salum kufariki Daktari Mkuu wa Mkoa aliendesha gari lake hadi nyumbani kwa Salum na kupaki gari lake nje na kuanza kulia jambo ambalo mara moja ndugu walielewa kuwa mambo yameharibika, hivyo waliweza kutayarisha sehemu hiyo ambayo iliwezesha watu kuja kuweza kuona mwili wa Salum kwa mara ya mwisho. Haikuchukua muda habari zilisambaa na ulinzi ukalazimika ukimarisha kwa kusaidiwa na polisi.
Watu wakakesha na marehemu. Kesho yake hali ilizidi kuwa ngumu wakati wa kusindikiza maiti kwenda makaburini ilikuwa kama kila mtu alikuwa akitaka japo abebe kidogo jeneza, hadi ikalazimu FFU wawepo kuleta amani. Jeneza la Salum liliweza kubebwa kutoka Nunge nyumbani kwa mama yake hadi Msamvu kwenye eneo alipozikwa, watu wakiwa wamejipanga mstari mrefu, hakukutumiwa gari.[1]
Baada ya kifo chake, Juma Kilaza na Cuban Marimba
[hariri | hariri chanzo]Aliyeichukua bendi na kuiendeleza alikuwa Juma Kilaza. Kilaza aliiendeleza vizuri kwa kutunga mamia ya nyimbo yaliyofurahisha sana watu miaka ya 60 na 70. Morogoro ulikuwa mji uliosifika kwa muziki, huku kukiwa na Mbaraka Mwinshehe na Morogoro Jazz Band, na huku Juma Kilaza na Cuban Marimba. Kuna watu walikuwa wakihamia Morogoro wikiendi na kurudi Dar siku ya Jumatatu asubuhi.
Kati ya nyimbo maarufu za Cuban Marimba zinazodumu kwenye kumbukumbu ni Shemeji Shemeji Wazima Taa, Wangu Ngaiye na wimbo Ee Mola Wangu, ambao Salum Abdallah awali aliutunga kwa mashairi marefu lakini akachukua beti chache kutengenezea muziki akilalamika kuwa kuna walimwengu wanamtakia mabaya, lakini siku ya kufa atawashitakia maiti wenzake kuhusu ubaya huo, wimbo huu ulikuja onekana baadaye kama ulikuwa ukitabiri aina ya kifo chake.
Kutabiri kifo chake kupitia wimbo
[hariri | hariri chanzo]Wimbo wake huu alioutunga kabla ya kifo chake pia ulileta tafsiri nyingi hasa kutokana na kifo chake cha ajabu. kwa maumivu.
E Mola wangu E Mola wangu, Nivue na ya dunia, Hao walimwengu , hao walimwengu , Wanitafuta kwa madawa, Wataka wadhulumu roho yangu, Wapate furahiwa, Natoa salamu zangu, Ningalimo mu dunia, Kwa ndugu na jamaa zangu Za mapenzi na furaha Za kuwatoa uchungu Ajali itakaponifikia Nahadithi ndugu zangu, Nyuma waliobakia, Kibeba maiti yangu Huku wakinililia Ninashtakia Mungu Nilotendwa mu dunia
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ "Kifo cha Salum Abdallah katika blogu ya Anko John Kitime". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-04-25. Iliwekwa mnamo 2016-11-21.