Nenda kwa yaliyomo

Calestous Juma

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Calestous Juma (Juni 9, 1953 – Desemba 15, 2017) alikuwa mvumbuzi na mtafiti wa sayansi kutoka nchini Kenya aliyefundisha kwenye Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani.

Katika maisha yake kama mtafiti na mwalimu wa chuo alishughulika maswali ya sayansi, teknolojia na maendeleo endelevu na hasa maswali ya biotekinolojia na bioanwai. Alikazia njia za kuleta uvumbuzi kwa kilimo barani Afrika.[1]

Maisha yake[2]

[hariri | hariri chanzo]

Calestous Juma alikulia katika fukwe za Ziwa Viktoria ambako alipata elimu ya msingi akasoma shule ya sekondari ya Port Victoria (Bunyala - Busia). Aliendelea kusoma ualimu kwenye Chuo cha Ualimu Egoji, Meru. 1974 hadi 1978 alikuwa mwalimu wa shule huko Mombasa kabla ya kujiunga na gazeti la Daily Nation, Nairobi alipoandika kuhusu mambo ya Sayansi na Mazingira.

Baadaye Juma alijiunga na taasisi ya Environment Liaison Centre International inayojihusisha na mambo ya mazingira. Hapa alikuwa mhariri wa jarida la Ecoforum[3]. 1982-1987 aliendela na masomo kwenye Chuo Kikuu cha Sussex, Uingereza alipopata shahada ya uzamili katika fani ya Sayansi, Teknolojia na Viwanda halafu ya uzamivu wa sayansi kutoka idara ya utafiti ya sayansi za siasa. Aliendelea kuandika juu ya maeneo mbalimbali kwenye masuala ya sayansi, teknolojia na maendeleo endelevu.

Tangu 1984 alichukua nafasi kama mtafiti katika taasisi na miradi mbalimbali aliposhughulika hasa maswali ya biotekinolojia.

Mnamo mwaka 1988, Calestous Juma alianzisha Taasisi ya Mafunzo ya Teknolojia (en:African Centre for Technology Studies) mjini Nairobi, taasisi ya kwanza ya kiutafiti ya kujitegema katika Afrika.[4]: 6 .

1995 - 1998 aliteuliwa kuwa katibu mtendaji wa ofisi kuu ya Mapatano ya Kimataifa kuhusu Bioanuwai (Secretariat of the Convention on Biological Diversity)[5] iliyoanzishwa kwa kufuatilia maazimio ya Kongamano ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira na Maendeleo mjini Rio de Janeiro mwaka 1992 (United Nations Conference on Environment and Development, Rio de Janeiro Earth Summit).

Mwaka 1998 alihamia Chuo Kikuu cha Harvard alipoitwa kuwa mshauri wa Harvard Center for International Development, tangu 1999 kuongoza Mradi wa Sayansi, Tekinolojia na Uvumbuzi. Tangu 2002 alikuwa profesa wa Maendeleo ya Kimataifa kwenye Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma (Harvard Kennedy School). Hapo aliongoza pia miradi ya Uvumbuzi wa Kilimo katika Afrika na Sayansi, Tekinolojia na Utandawazi.

Heshima na tuzo

[hariri | hariri chanzo]

Calestous Juma alikuwa mtu aliyetambuliwa na mamlaka zinazotambulika kimataifa katika masuala ya matumizi ya sayansi na teknolojia ili kuleta maendeleo endelevu duniani kote.[6] Aliwahi kutambuliwa na jarida la kiafrika liitwalo (the New African magazine) kuwa mmoja kati ya watu 100 wenye ushawishi mkubwa barani Africa mnamo mwaka 2012, 2013 na 2014. Alikuwa profesa wa utekelezaji wa maendeleo kimataifa na alikuwa mkuu wa kitengo cha Ubunifu kwaajili ya mpango mkakati wa maendeleo ya kiuchumi huko Chuo Kikuu cha Harvard.

Kitabu chake cha hivi karibuni kiitwacho The New Harvest: Agricultural Innovation in Africa kilichapishwa na Oxford University Press mnamo mwaka 2011.[7][8]

Kwa kutambua wasifu wake huo, Juma aliweza kuchaguliwa na vitivo mbalimbali vikiwemo Royal Society of London, National Academy of Sciences, The World Academy of Sciences (TWAS), uingereza Royal Academy of Engineering, the African Academy of Sciences na the New York Academy of Sciences. Nchini Kenya alipokea tuzo la Mkuki wa Moto.

Mwaka 2015 Juma alikoselewa baada ya kuonekana alishirikiana na kampuni ya Monsanto kutetea mazao yaliyobadilishwa kinasaba (genetically modified crops) katika makala mbalimbali bila kuonyesha[9] mawasiliano yake na Monsanto. Alijitetea kuwa hakupokea malipo kwa makala husika[10].

Calestous Juma alikuwa na matatizo ya kiafya tangu mnamo 2015. Tarehe 15 Desemba 2017 aliaga dunia mjini Boston.[11]

  1. Biography of C Juma Ilihifadhiwa 4 Oktoba 2017 kwenye Wayback Machine., tovuti ya African Success, iliangaliwa Desemba 2017
  2. CV Calestous Juma, tovuti ya Chuo cha Harvard, iliangaliwa Desemba 2017
  3. "Tovuti ya Ecoforum". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-12-26. Iliwekwa mnamo 2017-12-16.
  4. Calestous Juma (PDF), Novemba 2012, uk. 27, iliwekwa mnamo Januari 22, 2017{{citation}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  5. Former executive secretaries, tovuti ya Mapatano kuhusu Bioanwai CBD, iliangaliwa Desemba 2017
  6. name="List of Fellows">"List of Fellows". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2016-06-08. Iliwekwa mnamo 2017-12-16.
  7. Juma, Calestous (Januari 2011). The New Harvest: Agricultural Innovation in Africa. New York: Oxford University Press. ISBN 978-0199783199.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  8. "The New Harvest: Agricultural Innovation in Africa". Belfer Center for Science and International Affairs. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-01-12. Iliwekwa mnamo 27 Aprili 2014.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  9. Global Risks of Rejecting Agricultural Biotechnology , tovuti ya geneticliteracyproject.org, iliangaliwa Desemba 2017
  10. Harvard professor failed to disclose connection, tovuti ya Boston Globe, toleo la 1 Oktoba 2015, iliangaliwa Desemba 2017
  11. Harvard Professor Calestous Juma, Born in Kenya, Dies in U.S., tovuti ya allafrica.com, ya tar. 16 December 2017