Western

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Filamu za western)

Western (kutoka kiing. "West" - magharibi) ni aina ya fasihi, hadithi na filamu yenye asili katika Marekani. Western husimulia hadithi za watu walioishi wakati wa karne ya 19 hadi mwanzo wa karne ya 20 Marekani ilipoenea katika sehemu za magharibi ya Amerika ya Kaskazini. Filamu kuhusu kipindi hiki zilianza kupatikana tangu mwanzo wa karne ya 20.

Kazi muhimu ya hadithi hizo ilikuwa kuwapa watu wa Marekani picha kuhusu historia yao na kuhusu tabia nzuri ya mababu walioanzisha na kueneza taifa lao. Ukweli wa kihistoria jinsi ilivyo katika hadithi za kitaifa haukuzingatiwa mara nyingi.

Filamu za Western zilitengenezwa baadaye pia huko Ulaya hasa Spaghetti Western na mara nyingi zilicheza na aina za wahusika jinsi zilivyokuwa kawaida katika filamu za Marekani.

Mazingira ya kihistoria ya filamu hizi[hariri | hariri chanzo]

Katika nyakati zile Marekani ilitawala sehemu za mashariki za Amerika ya Kaskazini tu na kupanua polepole kuelekea magharibi hadi kufikia Pasifiki na baadaye pia kutawala maeneo ya katikati. Palikuwa na eneo la "mpakani" (frontier) ambako wakulima walowezi na wafugaji kutoka Marekani waliingia katika nchi ya wakazi asilia au Maindio na kuanzisha makazi yao huko. Mashamba na miji yale yalikuwa nje ya eneo la Marekani yenyewe. Kwa hiyo maisha yalikuwa kwa muda bila sheria wala serikali. Hata kama maeneo mapya yaliingizwa katika Maungano ya Madola ya Amerika taasisi za serikali zilikuwa mbali kwa muda na kazi ya kuratibu maisha ilibaki mkononi wa watu wenyewe katika eneo fulani.

Macowboy kazini

Wahusika katika hadithi za Western[hariri | hariri chanzo]

Hadithi zinazosimuliwa katika filamu za western mara nyingi huwa na watu wafuatao:

  • Cowboy au mchunga ng'ombe - anayeonyeshwa mara nyingi kama mtu mwenye kazi ngumu asiye na elimu lakini ni hodari. Kwa kawaida ni mtu mwema.
  • Sheriff au mpolisi - anayepigana na waovu; huishi na kulala ofisini mwake anapoangalia pia wafungwa. Kazi yake ni pamoja na kutetea wafungwa wale kama watu wa mji wanataka kuwanyonga mara moja. Kwa kawaida ana uwezo wa kutumia bunduki yake haraka sana. Huwa ni mtu mwema.
  • Rancher au mwenye shamba la mifugo - yeye ni mwajiri wa macowboy. Ama ni mtajiri sana au yeye ni maskini anayeanza kujenga maisha yake na kupambana na matatizo ya kila aina. Mara nyingi ni mtu mwema lakini hutokea pia kama mbaya anayetaka kujitajirisha hata akimwua jirani
  • Watu wa mjini - ama mwenye duka au mwenye kilabu. Anahofia waovu wanaopita mjini na kupora pesa zake. Kwa kawaida huwa mwoga asiye tayari kumsaidia sheriff.
    • Undertaker au mzishi ni mtu wa mjini wa pekee anayefurahia kila maiti inayoongeza mapato yake. Kwa hiyo hana neno na waovu na kwa kawaidi hawana neno naye. Asipokuwa na nafasi ya pembeni kabisa katika hadithi yeye huwa ni mwanafalsafa wa filamu mwenye hekima nyingi kuhusu maisha na mauti.
  • Mwanamke - aina yake ilikuwa haba huko magahribi ya kale kwa hiyo hakuna nafasi nyingi kwa waigizaji wa kike katika filamu za Western. Mwanamke hupatikana kwa namna mbili.
    • Ama yeye ni mke wa rancher au wa mtu wa mjini. Huonyeshwa kama mcha Mungu na hodari akishika bunduki.
    • Au yeye ni mwimbaji katiba kilabu anayedharauliwa na watu wa kawaida lakini macowboy humpenda; mara nyingi ni rafiki wa siri wa sheriff au mwovu mkuu anayeweza kumsaidia; hali halisi yeye ni mkahaba lakini filamu za Western za kawaida hawaonyeshi upande huu wa kazi yake waziwazi isipokuwa tangu kupatikana kwa Spaghetti Western upande huu wa maisha umeonyeshwa pia kiasi.
    • Mwanamke wa pekee ni binti wa rancher anayerudi kutoka masomoni. Alipoondoka alikuwa msichana mdogo lakini akirudi ni mrembo anayesababisha mvurugo kati ya wanaume wa eneo mara moja. Huingzwa hasa katika filamu pasipo na haja ya damu nyingi.
    • Kazi muhimu ya mwanamke katika filamu hizi ni kuwapa wanaume sababu ya kupigana juu yao ama kwa mikono -hasa kilabuni wanapovunja viti vingi pamoja na kioo kikubwa kilichopo katikati ya rafu ya vyupa- au kwa bunduki. Hii ni sababu ya kwamba undertaker huwaheshimu wakinamama hata asipopata nafasi nyingi ya kuwazika.
  • Mwovu mkuu na wenzake ni pilipili na sukari ya filamu za Western. Wanafika kutoka nje na kuleta kifo mpaka wameuawa wenyewe.
    • Mara wanashambulia benki mara wanafuata mipango ya kulipiza kisasi kwa sababu sheriff wa mji aliwahi kumwua kaka wa mwovu mkuu miaka 23 iliyopita. Wengine wameajiriwa na rancher mbaya kumfukuza jirani wake mwema kwa sababu chemchemi ya pekee iko ndani ya eneo lake.
    • Wakati mwingine mwovu huonyeshwa kuwa na tabia nzuri kwa sababu ameshakata shauri kuacha maovu lakini kwa bahati mbaya tangazo lenye picha yake linaloahidi kiasi cha pesa kwa yeyote anayemkamata au kumwua liko katika ofisi ya sheriff. Kwa hiyo sheriff anapaswa kumwinda. Kama sheriff angependelea kutomwona au kumsahau kuna mwovu wa aina nyingine ni headhunter au mwindaji wa waovu wanotafutwa anayetaka kichwa chake kwa sababu ya pesa.
Macowboy na Maindio (bado hai)
  • Mmeksiko ni mtu mdogo asiyeongea Kiingereza sanifu ni mtu anayestahili kupigwa na kudharauliwa na macowboy. Kosa lake ni ya kwamba miaka kadhaa iliyopita alishindwa na Waamerika na kubaki kwenye nchi iliyovamiwa na Marekani. Katika mawestern za baadaye mara chache anapata nafasi ya kumwua mwovu pia.
  • Indio au mwenyeji asilia wa Amerika ni hatari. Anaiba mifugo na kushambulia ovyo wazungu wazuri Wamarekani. Kama mkurugenzi wa filamu ana pesa ya kuajiri waigizaji wa kutosha maindio wengi sana hushambulia nyumba ya rancher au hata mji wote wakikaribia kushinda lakini kwa bahati nzuri cavallery (jeshi la farasi) hufika na kuwafukuza. Katika Western za baadaye inaweza kutokea ya kwamba sababu za Waindio zaelezwa kwa nini wanashambulia kwa mfano kwa sababu Wamarekani walitwaa ardhi yao au kuua watoto wao. Lakini hii si lazima kwa sababu marafiki wa filamu za Western hupenda kuona maajabu ya Western hawapendi kutafakari mno.

Maajabu ya Western[hariri | hariri chanzo]

Tabia ya ajabu ya watu katika filamu hizi ni wakifika mjini baada ya kusafiri njia ndefu kwa farasi kwenye jua kali huingia mara moja kilabuni. Hapa hawanywi maji au angalau bia lakini mara moja pombe kali ya whiskey wakiagiza chupa kimoja (lita 0.7).

Tabia nyingine ya ajabu ni ya kwamba wakipigwa risasi hufa mara moja bila kulia. Huanguka tu na kuwa kimya. Hakuna wajeruhiwa wanaoendelea kulia kwa masaa mengi usiku wote. Wengine hawaagi dunia mara moja lakini huwa na hotuba kabla ya kufa. Kuna pia aina nyingine wakipigwa risasi wanakata tu kipande cha shati na kufunika jeraha na kuendelea na mapigano bila matatizo.