Kalamashaka
Kalamashaka (kwa jina lingine K-Shaka) ni kundi la hip hop lenye makao yake katika mtaa wa Dandora, kitongoji katika mji wa Nairobi, Kenya. Kinajumuisha wasanii watatu: Oteraw, Kama na Johny. Kikundi hiki kiliundwa katika miaka ya katikati ya 1990. Walikuwa maarufu kwa wimbo wao Tafsiri Hii uliovuma sana mwaka wa 1997. Kundi hili lilifungua pazia kwa wasanii nyota kadhaa wa kimataifa kati yao Coolio na Lost Boyz na wameimba pamoja na Dead Prez na wasanii wengine wa kimataifa. Wametumbuiza katika nchi kadhaa kama vile Nigeria, Uswidi, Uholanzi, Afrika Kusini, Norway miongoni mwa nyingine. Kalamashaka walifungua njia kwa hip hop katika lugha ya Kiswahili na ikawa inatawala nchini Kenya. Kikundi hiki ni maarufu na mashabiki wake kwa muziki wake wa hardcore rap na wenye ujumbe wa kijamii na kisiasa. Albamu yao ya kwanza Ni Wakati iliyotolewa mwaka wa 2001 ilivuma sana na Channel O ya Afrika Kusini ilicheza mmoja ya video "Fanya Mambo" kutoka katika albamu hii. Albamu hii iliangazia uhalifu mitaani, ukabila, siasa na migogoro ya Afrika. Umaarufu wao ulianza kupungua wakati mitindo ya Genge na Kapuka ilipoibuka ambayo ilikuwa inaweza kuchezeka kwa urahisi na yenye tasfoa ambayo asilimia kubwa ya vijana wanapendelea kusikiliza kuliko muziki wa kifalsafa. Stesheni za redio za FM husita kucheza miziki yenye mpigo wa kijamii kama unaochezwa na Kalamashaka na kupelekea kupungua kwa umaarufu wao. Hata hivyo, kikundi hiki kimeendelea kufanya kazi na kukataa kubadili mtindo kulingana na nyakati na kufanya biashara ya muzik. Kundi hili lilisukuma makundi mengine kama Mashifta, Gidi Gidi Maji Maji, K-South, Necessary Noize na wasanii wengine wengi.
Kikundi hiki kimesaidia vijana wengine wa Dandora kuanza kuimba muziki wa rap. Wanajulikana pia kwa kuanzisha kikundi cha Ukoo Flani Mau Mau ambacho ni mkusanyiko wa takribani wanamuziki wa rap 24 kutoka Nairobi na Mombasa pamoja na Watanzania wachache. Ukoo Flani Mau Mau ilitoa albamu ya Kilio Cha Haki mwaka wa 2004 na kufiuatia na Dandora Burning iliyotolewa mwaka wa 2006. Hawapati kupewa usikizaji mkubwa katika redio au muziki wao kuchezwa kama wanamuziki wa genge na kapuka lakini bado wana mashabiki wengi.
Kama (jina halisi Kamau Ngigi) alitoa albamu yake ya kwanza peke yake, Kamaa mwaka wa 2009. Albamu ilitayarishwa na Ambrose Akwabi wa Mandugu Digital. Wakati huo huo, Kalamashaka wanaifanyia kazi albamu ya Hakuna Case. Albamu hii itatayarishwa na mwanamuziki mkenya mkaazi wa Uswidi Ken Gonga, ambaye alikuwa katika wimbo wa Kalamashaka "Fanya Mambo" [0]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- KalamashakaTovuti ya awali yenye picha kadhaa
- Kilio Cha Haki (through archive.org)
- Ukoo Flani Mau Mau (through archive.org)
- Ukurasa wa Myspace wa Ukoo Flani