Mambou Aimée Gnali

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mambou Aimée Gnali (amezaliwa 18 Oktoba 1935) ni mwanasiasa wa zamani wa Jamhuri ya Kongo. Mwaka 1963 alikuwa wa kwanza kuchaguliwa katika kikundi cha kwanza cha wanawake katika Bunge la Taifa (Jamhuri ya Kongo). Baadaye aliwahi kuwa Waziri wa Utamaduni na Sanaa kuanzia Januari 1999 hadi Agosti 2002.

Maisha binafsi[hariri | hariri chanzo]

Mambou Aimée Gnali, ambaye ni wa kabila la Wavili, alizaliwa Brazzaville mwezi Oktoba mwaka 1935.[1] Familia yake ilihamia Nkayi wakati baba yake alipohamishiwa katika mji huo. Baada ya miaka miwili ya masomo huko Pointe-Noire, alianza kuhudhuria shule ya bweni ya Masista wa Mtakatifu-Joseph de Cluny huko Brazzaville. Mwaka 1947, alihamishiwa shule ya upili ya Jeanne d'Arc huko Orléans nchini Ufaransa. Hata hivyo, alifukuzwa na kurudi Kongo mwaka 1952, akamaliza elimu yake katika shule ya Savorgnan de Brazza na kuwa msichana wa kwanza katika Afrika ya Kati ya Kifaransa kupata cheti cha kumaliza masomo ya sekondari.[1] Alirejea Ufaransa na kusomea fasihi ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Paris, ambapo alijiunga na Shirikisho la Wanafunzi Weusi wa Kiafrika nchini Ufaransa, akawa mwanachama wa kamati yake ya utendaji.[1]

Baada ya kupata diploma yake, ambayo ilimfanya kuwa mmoja wa wanawake wa kwanza wa Kongo kupata shahada ya chuo kikuu,[2] aliarejea Congo mwezi wa Septemba 1963 na akaanza kufundisha katika shule ya upili huko Pointe-Noire. Hata hivyo, baada ya kuwa mwanachama wa Harakati ya Taifa ya Mapinduzi (MNR), alikuwa mgombea wa chama hicho katika Uchaguzi wa Bunge la Jamhuri ya Kongo wa mwaka 1963. Bila upinzani wowote katika uchaguzi huo, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Taifa kutoka jimbo la Pointe-Noire, akawa mmoja wa kundi la kwanza la wanawake watatu kuingia bungeni.


Baada ya kukataliwa kwa nafasi ya kufundisha katika shule huko Brazzaville mwaka 1965, alihamia Marekani kuendelea na elimu yake, akimaliza kozi katika Chuo Kikuu cha Lawrence, Chuo Kikuu cha Saint Louis, na Chuo Kikuu cha Columbia. Baada ya kurudi Kongo mwaka 1967, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Elimu mwaka 1968, akishikilia wadhifa huo hadi mwaka uliofuata. Pia alifundisha katika École normale supérieure huko Brazzaville mpaka alipojiunga na UNESCO mwaka 1971. Alihusika katika miradi ya elimu katika nchi kadhaa za Afrika, akiishi Paris hadi mwaka 1978 na baadaye Dakar hadi mwaka 1991.[1]

Baada ya kurudi Kongo, alichaguliwa kuwa mjumbe wa baraza la mji wa Pointe-Noire mwaka 1992, na akawa naibu meya mwaka 1995.[1] Mwezi Januari 1999 aliteuliwa kuwa Waziri wa Utamaduni na Sanaa, akiwa na jukumu la Utalii. Jean-Claude Gakosso aliteuliwa kumrithi tarehe 18 Agosti 2002.[3] Baadaye alijiunga na Chama cha pour l'Alternance Democratique, akawa katibu wake mkuu.[2]


Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. 1.0 1.1 1.2 1.3 1.4 GNALI Aimée Mambou Le Maitron
  2. 2.0 2.1 John Frank Clark & Samuel Decalo (2012) Historical Dictionary of Republic of the Congo p198
  3. List of governments of Congo since 1999 Archived 2008-11-22 at the Wayback Machine, izf.net Kigezo:In lang.
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mambou Aimée Gnali kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.