Zoroasta
Zoroasta, pia Zarathustra alikuwa mwanzilishaji wa dini ya Uzoroasta na nabii ya kwanza wa imani hii.
Hakuna uhakika wala juu ya mahali wala wakati alipoishi. Leo hii wataalamu wengi wanaamini aliishi katika mashariki ya Uajemi ya Kale.
Habari zilihifadhiwa kimdomo kwa muda mrefu na kuandikwa karne baada yake kwa hiyo ni vigumu kujua umri wa habari zake. Wataalamu wamekadiria wakati wa maisha yake kati ya miaka 1800 KK na 600 KK ilhali hakuna uhakika.
Jina lake liliandikwa katika maandiko ya kale zaidi kwa umbo la Zarathustra. Kimatifa amejulikana zaidi kwa umbo la Kigiriki yaani Zoroasta (Ζωροάστηρ zoroaster). Waajemi wa leo pamoja na waumini wake wanamwita ama "Zartosht" au "Zardosht".
Kile kinachojulikana juu yake ni hasa kutokana na mashairi ya "Gatha" ambayo ni msingi wa kitabu kitakatifu cha imani yake kinachoitwa Avesta. Hapo anaonekana alikuwa kasisi katika dini ya Kiajemi ya kale alipopata ufunuo kuwa miungu mingi si kwlei badala yake kuna Mungu mmoja tu. Huyu Mungu alijulikana kwake kwa jina Ahura Mazda ni muumba wa kila kita anayetafuta mema kwa wote. Ahura Mazda ana mpinzani wa kiroho mwenye jina la Ahriman anayetafuta mabaya. Kila mtu ana wajibu kuamua kati ya mema na mabaya na akiamua mema anatakiwa kushirikiana na Ahura Mazda katika uumbaji wake.