Njia Nyeupe

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Njia nyeupe)
Njia nyeupe jinsi inavyoonekana usiku (picha ilipigwa jangwani pasipo na machafuko wa nuru)
Galaksi yetu jinsi inaaminiwa kuonekana vile kama tunaiangalia kutoka juu; picha ya galaksi ya mbali yenye mikono miwili ya parafujo
Galaksi yetu inafanana na hii NGC 4565 tunayoona kutoka pembeni kabisa. Tunatambua vizuri jinsi gani mlia wa nyota zake unanenepa kidogo kwenye kitovu penye nyota nyingi.

Njia Nyeupe (kwa Kiingereza Milky Way), pia "mkokoto wa kondoo za Sumaili" [1] ni jina la mlia mpana wa nyota nyingi unaoonekana angani wakati wa usiku kama wingu jeupe linalong`aa.

Hali halisi hii ni jinsi tunavyoona galaksi yetu ambamo mfumo wa Jua letu pamoja na Dunia ni sehemu zake.

Umbo na umbali

Galaksi yetu imekadiriwa kuwa na nyota zaidi ya bilioni 100 hadi bilioni 400[2]. Inafanana na kisahani chenye umbo la parafujo. Kipenyo cha kisahani hicho ni miakanuru 100,000 ikiwa na unene wa miakanuru 3,000.

Galaksi iliyo karibu zaidi angani inaitwa Andromeda ikiwa na umbali wa miakanuru milioni 2.5.

Isipokuwa sayari za Jua letu na galaksi ya Andromeda (inayoonekana kama nyota moja), nyota zote ni kama Jua letu yaani tufe kubwa sana la gesi joto.

Kuonekana kwa Njia Nyeupe kutoka duniani

Nyota karibu zote tunazoziona kwa macho yetu ni sehemu za Njia Nyeupe. Kutegemeana na kiwango cha giza tunaweza kuona kati ya nyota 3,000 hadi 6,000 bila msaada wa darubini.

Si rahisi kuona nyota nyingi tukiwa mjini kwa sababu mwanga wa taa za mjini unaakisiwa katika angahewa na kuzuia kuona mianga hafifu nje ya angahewa.

Idadi kubwa zaidi ya nyota za Njia Nyeupe hatuwezi kuona wala kubainisha, kwa hiyo zinatokea machoni kama ukungu mweupe tu.

Uwezo wetu wa kuona nyota nyingi zaidi umepunguzwa na kuwepo kwa mavumbi ya kinyota kati ya mahali petu na kitovu cha galaksi.

Muundo

Galaksi yetu ina umbo la parafujo (spirali) ya kisahani. Mahali petu pamoja na Jua pako kando kiasi ndani ya uwiano wa kisahani hiki. Tuko takriban 2/3 ya umbali wa kipenyo kutoka kitovu cha kisahani.

Ikitazamwa kutoka juu galaksi yetu ina umbo la parafujo yenye mikono mbalimbali. Picha hii tumeipata kutokana na kuangalia galaksi za mbali angani zinazoonekana kutoka juu ilhali parafujo inaonekana.

Soma pia

Viungo vya nje

Wikimedia Commons ina media kuhusu:

Marejeo

  1. Yaani njia ya kondoo wa Ismaili; kuhusu majina ya nyota na sayari zilizojulikana kwa Waswahili na hivyo kuwa na majina asilia linganisha Jan Knappert, The Cosmology of Swahili Islamic Literature, in: Swahili Islamic poetry, Brill 1971, Vol 1 uk 96-97 - taz google booksearch [1]
  2. https://asd.gsfc.nasa.gov/blueshift/index.php/2015/07/22/how-many-stars-in-the-milky-way/ Maggy Massetti: How Many Stars in the Milky Way?, tovuti ya NASA July 22, 2015, iliangaliwa Mei 2022
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Njia Nyeupe kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.