Malala Yousafzai
'
Malala Yousafzai | |
---|---|
Amezaliwa | 12 Julai 1997 Mingora, Pakistan |
Nchi | Pakistan |
Kazi yake | Mwanaharakati |
Malala Yousafzai (kwa Kipashtuni: ملاله یوسفزۍ, kwa Kiurdu: ملالہ یوسف زئی; amezaliwa 12 Julai 1997) ni mwanaharakati wa kupigania haki ya elimu kwa watoto na usawa wa kijinsia kwa wanawake kutoka nchini Pakistan. Malala ni mtoto wa kwanza katika familia yao ya watoto watatu. Ana wadogo zake wawili wa kiume, Khushal na Atal Yousafzai. Baba yake jina lake ni Ziauddin Yousafzai na mamake ni "Toor Pekai Yousafzai" ambaye alikuja kufunzwa kusoma na kuandika ukubwani baada ya harakati za binti yake kupamba moto. Mama huyu aliyeacha shule akiwa na umri wa miaka sita baada ya kuacha kutokana kuwa mwanamke pekee katika shule hiyo.[1]
Mwaka wa 2014, alitunukiwa tuzo ya Nobel ya Amani 2014 pamoja na Kailash Satyarthi. Ni kijana kuliko yeyote yule aliyewahi kupewa tuzo ya Nobel.[2]
Maelezo kutoka katika kitabu cha Malalala
[hariri | hariri chanzo]Kitabu cha Malala Yousafzai kinaitwa "I Am Malala: The Story of the Girl Who Stood Up for Education and Was Shot by the Taliban". Ndani yake kuna habari za maisha yao ya hekaheka huko nchini Pakistani na harakati za Taliban katika kufisha elimu kwa mtoto wa kike.[3] Malala alisimama kidete kuhakikisha usawa kielimu unapatikana katika mji wao wa "Swat Valley". Jambo ambalo lilipelekea shida nyingi kutokea, kupingwa na sehemu kubwa ya jamii waliolewa na dini. Huku wakijisikia vibaya kwa uwezo wa Malala katika kuhoji ni sehemu gani katika dini imeeleza ya kwamba mtoto wa kike au mwanamke asipate elimu isipokuwa wanaume pekee.[4] Huku mzee wake, mzee "Ziauddin Yousafzai", akipata kashfa na maneno kejeli mengi ya kwamba anajifanya anaishi Kizungu. Ajabu iliyopo, baba na mwana wanafanana mawazo. Inaanza na "Ziauddin Yousafzai" ambaye alitaka mtoto wake aishi kipekee, namna ambavyo yeye anaona inafaa, ilimradi tu asivuke maandiko ya dini yanavyotaka, alimtaka aachane na hizi mbwembwe za walimwengu wa leo kuongeza chumvi ya dini ilimradi tu mambo fulani yasifanyike. Kwa utamaduni wa Wapashtuni, mtoto wa kiume ana thamani kubwa sana kuliko wa kike. Wanapendelea zaidi kupata mtoto wa kwanza wa kiume kuliko wa kike. Kwa familia hii ilikuwa tofauti kidogo, mtoto aliyezaliwa wa kwanza ni wa kike, na baba alimpenda kupita kiasi. Alimtia hamasa ya kujiamini hadi raha. Alimwondolea stereotypes zote za katika jamii yao na kumtaka aishi kama yeye anavyoona inafaa.[5]
Jina pekee alilopewa lina-maanisha "ondoa huzuni", asihuzunike kwa kuzaliwa mwanamke. Hali hii ilimfanya Malala akue katika misingi ya kujiamini na kujitambua kupita maelezo. Baba alimtaka mwanae asome na apate elimu ili ajue ulimwengu upo vipi. Katika safari hii ya elimu, iliambatana na uanaharakati wa kupigania haki za watoto na wamama katika elimu. Siku zilienda, maisha ya baadaye akapata kujulikana na karibia taifa zima katika harakati yake ya kupigania haki ya mtoto wa kike katika elimu. Mwaka wa 2011 anapata tuzo ya Amani ya Taifa kwa Vijana kwa nchi ya Pakistani. Hasa katika kutetea haki ya usawa wa elimu.[6] Hii ilileta shida kwake, kwani balaa lilianza hapa na vitisho mbalimbali. Pamoja na yote haya, huko Pakistani hali si shwari kutokana na eneo lao kuvamiwa na Taliban. Siku moja ya tarehe 9 Oktoba 2012 ilikuwa siku ya majonzi kwa mji wa Swat Valley na ulimwengu baada ya Mtalibani mmoja kusimamisha gari la shule ambalo Malala alikuwa amepanda na kuuliza "Nani Malala"? Baada ya kupata jibu, alifyatua risasi tatu mfululizo na kumpiga mbili Malala, moja sikioni, nyengine kwenye KOMWE na kuzama hadi eneo la bega.[7]
Kwa uwezo wa Mungu, bi mdogo alipelekwa hospitali ya karibu, lakini baadaye kusafirishwa mjini kwa ajili ya matibabu zaidi katika hospitali ya jeshi, huko alifanyiwa upasuaji wa awali wa kutoa risasi na mabaki yake, lakini bado huduma za afya zilikuwa hafifu, mama mmoja aliyejulikana kwa jina la Fiona, Daktari Mwingereza, katika hospitali ya Queen Elizabeth huko mjini Birmingham, alitaka mtoto apelekewe nchi za nje kwa matibabu zaidi. Awali mzee wake hakuweza kwenda kutokana na kukosa vibali, lakini polepole ilifanikiwa. Lakini safari ya kwenda ilianza na Fiona aliyekabidhiwa mtoto na baba yake Malala.[8] Walifika Uingereza na kuanza matibabu kama ilivyohitajika. Mungu mkubwa walifanikiwa kumtibu kwa kiasi kikubwa na baadaye kupata salamu tele kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Akiwa huko Uingereza, 2014, alipata tuzo ya Nobel ya Amani kwa kazi ya kusimamia amani na usawa kijinsia huko Pakistani. Ikiwa ni ya kwanza kutolewa kwa raia wa Pakistani, na ya kwanza kutwaliwa na mpokeaji mwenye umri mdogo kuliko wote.[9]
Malala anaamini kupigwa kwake bunduki kumemfanya azidi kupata hamasa ya kuendelea na harakati na si woga tena kama walivyodhani watu wa Taliban. Amehidi kujitolea kwa hali na mali nguvu zake kuhakikisha usawa wa elimu unapatikana ulimwenguni kote na si Pakistani pekee. Kitabu kinaeleza pia jinsi nchi ya Pakistani ilivyokuwa na mizengwe katika suala zima la utawala na namna ambavyo hawajali wananchi wake licha ya matatizo yanayowatokea. Bado suala la viongozi kuawa kila kukicha. Maisha ya mtu hayana thamani nchini humo. Taliban walitamba hakuna mfano. Vilevile ujasili wa baba yake katika kaunzisha shule kwa tabu, hadi kufanikiwa karibia miaka 20 baadaye na kabla ya matunda, yanazuka mengine. Tangu aingie Uingereza, Malala kaanzisha asasi ya kusaidia watoto inayoitwa "Malala Fund" inayokusidia kusaidia elimu kwa watoto na kina mama kwa ujumla.[10]
Kwa ujumla, kitabu kimeandikwa na Malala mwenyewe kwa msaada wa Mwanahabari na mwandishi mzuri Bi. Christina Lamb ambaye alikaa nae bega kwa bega katika kuhakikisha kitabu kina kamilika.[11][12]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Malala Yousafzai's mother, Toor Pekai, reveals she’s at school, learning to read and write Independent UK, Friday 16 October 2015.
- ↑ Malala Yousafzai - Fact Nobel Prize, wavuti rasmi, 2014
- ↑ The Taliban’s ‘alarmingly efficient’ war on education Gazeti la the Guardian.
- ↑ Malala Yousafzai: Why I Fight for Education wavuti ya National Geographic
- ↑ Malala: like father, like daughter wavuti ya Telegraph
- ↑ The Girl Who Wanted to Go to School gazeti la New-Yorker.
- ↑ Malala Yousafzai: Pakistan activist, 14, shot in Swat wavuti ya BBC, 2012.
- ↑ Birmingham doctor who treated Malala in Pakistan just hours after she was shot in the head, to star in new documentary Birminghammail.
- ↑ Malala becomes youngest person ever to win Nobel Prize wavuti ya BBC.
- ↑ What We Do Malala Fund wavuti.
- ↑ I Am Malala Ilihifadhiwa 8 Juni 2018 kwenye Wayback Machine. Christina Lamb.net
- ↑ My year with Malala Ilihifadhiwa 5 Juni 2018 kwenye Wayback Machine. Christina Lamb.net
Makala hii kuhusu mshindi wa Tuzo ya Nobel bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Malala Yousafzai kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |