Lango:Ujenzi/Makala iliyochaguliwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Koloseo mwaka 2007 wakati wa usiku
Koloseo mwaka 2007 wakati wa usiku

Koloseo (Kiitalia: Colosseo) ni kiwanja cha michezo cha kale mjini Roma kilichopo katika hali ya maghofu kutokana na umri wake wa miaka 2000. Ni kati ya majengo mashuhuri mjini Roma na duniani kwa ujumla. Wakati wa Dola la Roma ilikuwa jengo kubwa kabisa liliilojengwa na Waroma wa Kale.

Koloseo ilijengwa kuanzia mwaka 70 hadi 80 BK. Kaisari Vespasiano alianzisha ujenzi kwa kutumia mapato ya uwindo wa vita ya Waroma dhidi ya Uyahudi na hasa hazina ya hekalu ya Yerusalemu. Ilikamilishwa na Kaisari Titus.

Kiwanja kilikuwa na nafasi kwa watu 45,000 hadi 50,000. Watazamaji waliangalia maonyesho ambako watu au wanyama waliuawa. Michezo hii iligharamiwa na serikali kwa ajili ya wakazi wa mji kama burudani. Falsafa ya kisiasa ya Roma ilisema ya kwamba watu watulia wakipewa "panem et circenses" yaani "chakula na michezo".

Baada ya ushindi wa Ukristo mashindano ya kuua watu yalipingwa na kanisa. Shindano la mwisho lilitokea mwaka 434/435. Mapigano dhidi ya wanyama yaliendelea hadi mwaka 523. Lakini baada ya mwisho wa Dola la Roma idadi ya wakazi wa Roma ilipungua na Koloseo haikutumiwa tena kwa michezo.