Lango:Lugha/Intro

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Lugha (Kar: لغة) ni utaratibu kwa ajili ya kuwasiliana kati ya binadamu au kati ya viumbe vyovyote venye akili.

Mwaka wa 2008 umetangazwa kuwa Mwaka wa Lugha wa Kimataifa. Somo la lugha linaitwa maarifa ya lugha au isimu. Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zilizokua katika mpango maalum na zilizokubaliwa na jamii ya watu fulani ili zitumike katika mawasiliano.

Mara chache neno lugha linatumika kwa taratibu za kuwasiliana za wanyama. Lakini taratibu hizo ni tofauti sana: Katika lugha za wanyama, sauti moja ina maana moja tu. Lakini katika lugha za binadamu, sauti nyingi zinaunganishwa kutengeneza maneno, na maneno mengi yanaunganishwa kutengeneza sentensi.

Hivyo mnyama ambaye anaweza kutengeneza sauti ishirini tofauti anaweza "kusema" mambo ishirini tu. Kwa upande mwingine mtu ambaye anaweza kutengeneza sauti ishirini, anaweza kusema mambo zaidi ya millioni.