Bongo na Flava

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Bongo na Flava

Posta ya "Bongo na Flava"
Imeongozwa na Novatus Mugurusi (Rrah C)
Imetayarishwa na Staford Kihore
Mary MugurusiMtayarishaji Mtendaji
Suzan Mugurusi
John MahundiMtayarishaji Mtendaji
Imetungwa na Novatus Mugurusi
Nyota One Incredible
Makamua
Godliver Gordian
Fid Q
Wakazi
Saigon
Silipa Swai
Karabani
Muziki na Tamaduni Muzik
Lamar
Sinematografi Myovela Mfuaisi
Imehaririwa na Hurbert Lawrence
Imesambazwa na Proins Promotion LTD
Imetolewa tar. 2016
Ina muda wa dk. 135
Nchi Tanzania
Lugha Kiswahili

Bongo na Flava ni filamu ya muziki na maisha iliyotoka rasmi 2016 na kuja kuamshwa tena 2018 Aprili chini ya mwamvuli wa BongohoodZ kutoka nchini Tanzania.[1] Filamu imeongozwa na Novatus Mugurusi na kutayarishwa na Staford Kihore, Mary Mugurusi, John Mahundi, Suzan Mugurusi, Francis Makwaia na Karabani kwa ushirikiano na Dream High Pictures, Next Level, Makini Ent., Cheusi Dawa TV, Fischcrab Music na Atok. Ndani yake anakuja One the Incredible, Makamua, Fid Q, Godliver Gordian, Wakazi, Silipa Swai, Songa, Lamar, Salu Tee, Karabani na Saigon.[2][3]

Filamu inahusu harakati za kupigania kuwa mwanamuziki mkubwa katika Tanzania. Kufanikisha zoezi hilo, Zopa (One Incredible) anaamua kwenda Dar es Salaam kutimiza ndoto yake ya kuwa mchanaji mkubwa. Anakutana na Joe aliyemsitiri hadi hapo alipokuja kupata mafanikio yake.[4][5]

Filamu ilisifiwa na wengi, hasa kwa utumbuizaji mkubwa aliyoufanya One the Incredible. Miongoni mwa waliosifia ni pamoja na msanii wa muziki wa hip hop nchini Tanzania A.Y.[6]

Hii ndio filamu ya kwanza Tanzania kuleta mapinduzi halisi ya uigizaji wa maisha halisi kabisa ya mtaani. Awali ilikuwa watu wanaigiza tu hata kama sehemu ya matusi, ambayo huko mtaani ni jambo la kawaida kutukana ilikuwa hakuna. Lakini katika filamu hii imeigizwa katika maisha yaleyale ya mtaani kama jinsi nchi za nje wanavyoigiza maisha halisi ya wahuni.

Hadithi[hariri | hariri chanzo]

Hadithi inamwelezea Zopa (One the Incredible) aliyekuja mjini kwa rafiki yake wakuitwa Chidy aliyemuahidi ana kazi ya kumpa kumbe hakuwa na lolote bali utapeli tu. Mbaya zaidi anafika kwa kina Chidy anaambiwa Chidy kafungwa jela kwa kesi ya uuzaji wa bangi. Zopa anaomba hifadhi ya muda, bila mafanikio anaondoka mpweke mitaani huenda akafadhilika. Katika zurura yake katokea Coco Beach kakutana vijana wanaimba nyimbo kibao kwa kupiga akapela zenye mvuto. Anaunga nao, kwa pembeni kulikuwa na mtu anamuangalia kwa ustadi mkubwa jinsi Zopa anavyoghani. Kila jioni inapofika, mtihani wa kulala unaanza, sehemu anayolala kila siku katimuliwa na mwenye duka kwa matusi mazito. Siku aliyohama eneo tu, usiku wake kuna wahuni walimkuta wakampa kichapo cha nguvu. Wakamwacha akiwa hoi, kajisogeza hadi nyumba za jirani, kakuta maji barazani kafungua kaanza kunawa. Kidogo mwenye chumba anatokea (Makamua) anamkoromea, polepole wanafahamiana kama alimuona Coco Beach. Wanaongea mwishowe Joe anamkaribisha Zopa ndani.

Anaelezea kisa cha maisha yake hadi kufika DAR, jamaa anamwambia yaliyotokea yashatokea, muhimu tuhangaike tupate kipato cha kuchangia kulipa chumba. Joseph ni mishentauni, kazi za kunjunga karibia kila siku. Siku, wiki, mwezi mara mwaka, mafanikio bilabila. Zopa anaamua kujiongeza baada ya kumuona Runda (Salu Tee) anaingiza kiasi kikubwa akiwa kakaa tu kijiweni. Jose anamwambia mwamba ni pusha yule, sidhani kama kazi hiyo utaiweza. Isitoshe, huu ukanda wake, kamwe huwezi kuuzia hapa. Kwa kutumia fomula ya shida mgunduzi, Zopa anamchangulia mpango mzima Joseph namna ya kutoka kwa haraka au kujipatia vijisenti ambavyo vitamwezesha kujikimu na mambo ya msingi. Wanasogea kwa Runda, kwa masharti magumu, Runda anawapa njia. Wanamuona muhusika, wanafanikisha zoezi la kwanza. Ukawa utaratibu na mambo yakawa safi ndani ya muda mfupi, wakapanga nyumba nzuri zaidi. Zopa anapata mkwanja hadi wa kuingia studio na kutengeneza demo ya kanda mseto ya kwanza. Siku moja Zopa akiwa na Joseph Baa moja hivi, kwa mbali anamuona mtoto mzuri anaamua kumsogelea, kumkaribia kumbe Anita (Godliver Gordian) ambaye walisoma ote sekondari Kigoma. Anita anafikicha akili zake na kumkumbuka Zopa kama alisoma nae.

Wanafahamiana na kupeana muhtasari wa maisha wa kila mmoja kaja kufanya nini mjini hapa. Zopa alijinadi kama mwanamuziki, wakati Anita alisema yeye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha usimamizi wa fedha (IFM). Punde anatokea bwanake na kila mtu anabaki na hamsini zake. Baadaye wanakutana tena na Anita, safari hii mchana kweupe. Zopa anaamua kuacha uzoba na kuomba namba ya Anita zoezi ambalo halikufanikiwa. Lakini kwa msaada zaidi, Anita anamtajia klabu ya usiku ambayo anapenda kwenda sana inaitwa Club X. Zopa mfukoni majalala, anamsogelea Joseph amlipe pesa zake alizomkopesha. Joseph hana kitu, anamwambia kama vipi chukua puri moja kule home. Zopa anabeba tayari kwa kufanya usambazaji kule disko. Anita anatokea kaunta, anakutana na Zopa, wanaongea, kabla maongezi kunoga, anatokea mshefa wake, vurumai, kumbe bwana jamaa kaja na pira, wanamsachi wanamkuta na puri jamaa anaingia ndani kwa mara ya kwanza maishani mwake. Ili kutoka, anatakiwa awauze wanawe wanaomletea mzigo ndio kwake inakuwa salama. Kwa kuonesha ujanadume, Zopa anagoma. Heri abaki ndani kuliko kuwa snitch. Anita anakata tamaa, lakini anafanya alilofanya ndani ya miezi sita, mchizi anaachiwa.

Wanachukuzana hadi nyumba aliyopanga Zopa, ambapo alimuacha Joseph kabaki pale. Pale msala Joe kauza kila kitu kasepa zake. Zopa asiye na la kufanya, anasitiriwa kwa mara nyengine tena na Anita. Wanaishi pamoja kama mpenzi naogopa kusema nakupenda. Anita anamtafutia kazi ya baa Zopa, anaanza, anajikusanya tena, safari hii anataka kwenda kwa mtayarishaji mkubwa zaidi ili kupata kazi yenye ubora. Anamsogelea mwamba mmoja anaitwa Young Tozi (Karabani). Mwamba anamzingua sana, almanusura aingie kwenye dimbwi la walevi ili kukata mawazo. Kwa nasaha za Anita, anarudi kwenye mstari. Siku moja akiwa kazini kwake, anakuja msanii anayependa sana maishani mwake, Fingaprinti (Fid Q). Punde, Finga anaelekea maliwatoni, Zopa anamsalandia, anamchania madini, Finga anaingia mazima. Wanapeana demo ya kandamseto, lakini mabrazameni wake wanaicha pale. Mbaya zaidi ikiwa imelowa na mapombe. Linamgadhibisha Zopa, anaona dharau hii sasa. Anaacha kazi, anamtokea mchizi wake mmoja wa Diko (Wakazi) ambaye wanajuana kitambo. Kuna siku alikutana nae mchizi akiwa njema kinyama. Anampa mchongo wa kwamba yeye ana dili na sembe.

Akiwa sawa na yeye anaweza kumuunganishia. Zopa aliona huu ndio muda mwafaka wa kumtafuta mchizi huyo ili atoke kimaisha, maana muziki hauwezi tena kumtoa kimaisha. Mwamba anatokea, wanachukuzana hadi kwa taita, wanaseti mipango, tayari kwa gemu, Zopa ananyeta mbele ya wana wengine, anaomba mzigo asepe nao magetoni ili aweze kuumeza akiwa meni-am. Huko studio Fingaprinti anaona ngoma yake ubeti wa pili haifai yeye kuchana, anamkumbuka Zopa aliyemchania miraba ya kufa mtu kule maliwatoni, anawauliza wana kuna CD muliichukua pale, wanajifanya hawajui. Finga anaona sio kesi, anajisogeza eneo la baa, anamuulizia mchizi, anaambiwa kaacha kazi kwa hiari, anaomba namba ya simu, anamwendea hewani, lakini muda si rafiki kwa kupokea simu kwa sababu alikuwa anajitahidi kumeza kete ili aanze safari siku inayofuata. Finga king'ang'anizi, anaenda hewani tena na tena hatimaye Zopa anaacha kufanya anachofanya, na kupokea simu, anasikia sauti ya msanii ambaye ndiye mfano wake wa kuigwa anamtaka aje studio wafanye ote ngoma.

Taarifa hii inamrudisha Zopa mwenye fokasi ya mziki na kurudi ukumbini alipoketi Anita aliyekuwa anabubujikwa na machozi kwa kufanywa vibaya na Zopa. Zopa ana asili ya uungwana, anajishusha na kumpa mkasa mzima Anita. Azimio baada ya mashauriano ni kurudisha mzigo alipoutoa na hakuna safari. Licha ya onyo alizopewa aliona hakuna jinsi bora kufa kuliko kujiingiza kwenye mkasa huo. Anafanikiwa kuchomoka kwenye tundu hilo kimazabe, kisha huyo hadi studio na kufanya maajabu makubwa kwenye ngoma.

Siku zinaenda, goma linapigwa redioni analisikia, Finga anaingia nae mkataba wa kumsimamia na maisha aliyokuwa akiyataka ya kuwa msanii mkubwa yanatimia licha ya magumu aliyopitia. Filamu inaishia Zopa akiwa klabu na mnadio wa nguvu kutoka kwa Finga akiwa na washikaji zake.

Wahusika[hariri | hariri chanzo]


Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. "Bongo na flava ni bonge la movie na pia ni funzo kwa bongo movies - JamiiForums". JamiiForums (kwa en-US). Iliwekwa mnamo 2018-08-12. 
  2. D.-top Tz. "MOVIE l Bongo na Flava l Official bongo movie watch/download mp4". welcome to d-top tz. Iliwekwa mnamo 2018-08-12. 
  3. "New MOVIE: Bongo Na Flava | Watch - Bekaboy", Bekaboy (kwa en-US), 2018-04-07, ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-06-14, iliwekwa mnamo 2018-08-12 
  4. "Bongo na Flava - Thurday Movie Night @ Goethe Institut - Events in Tanzania, | Bongo!". www.bongo.co.tz. Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2018-08-09. Iliwekwa mnamo 2018-08-12. 
  5. Dizzim Online (2018-05-28), One The Incredible azungumzia filamu ya Bongo na Flava, single mpya na kazi na Adam Juma, iliwekwa mnamo 2018-08-12 
  6. "AY akubali walichofanya Fid Q, One, Wakazi, Songa na wengineo katika Bongo na Flava Film - Bongo5.com", Bongo5.com (kwa en-US), 2018-04-10, iliwekwa mnamo 2018-08-12