Nenda kwa yaliyomo

Simba (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Asadi (kundinyota))
Nyota za kundinyota Simba (pia Asadi, Leo) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Simba (pia Asadi, Leo) jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini
Picha ya Simba-Asadi pamoja na Asadi Mdogo jinsi ilivyowazwa na msanii Hall

Simba ni kundinyota la zodiaki linalojulikana pia kama Asadi au kwa jina la kimagharibi Leo[1]. Ni moja ya makundinyota yanayotatambuliwa na Umoja wa kimataifa wa astronomia [2]

Kiuhalisia nyota za Simba huwa haziko pamoja kama zionekanavyo kutokea duniani. Kuna umbali mkubwa kati ya nyota na nyota, pia kuna umbali mkubwa kati ya mahali zilipo nyota hizo na duniani bila kujali iwapo kwa mtazamo wetu zaonekana kuwa karibu au mbali. Kwahiyo kundinyota "Simba" linaonyesha eneo la angani jinsi lionekanavyo likiangaliwa kutokea duniani.

Jina

Mabaharia Waswahili waliita nyota hizi Asadi kutokana na Kiarabu أسد ʾasad ambalo linamaanisha "simba". Jina hili lilipokelewa na Waarabu kutoka kwa Wagiriki wa Kale waliosema Λέων leon "simba" na hao walipokea kundinyota hii tayari kutoka Babeli na Misri ya Kale. [3] [4]

Katika unajimu wa kisasa katika Afrika ya Mashariki jina "Asadi" limesahauliwa ikiwa kundinyota linaitwa "Simba" kwa tafsiri tu.

Mahali pake

Simba liko angani kwenye mstari wa Zodiaki kati ya Saratani (Cancer) upande wa magharibi na Nadhifa (Virgo) upande wa mashariki.

Magimba ya angani

Simba huwa na nyota nyingi zinazoonekana kwa macho ya kawaida. Nyota nne angavu zaidi zina magnitudi ya kwanza au pili ambazo ni

  • Maliki Junubi[5] (en:Regulus), pia Alfa Leonis ambayo ni nyota nyeupe-bluu yenye uangavu unaonekana wa 1.34, ikiwa na umbali wa miakanuru 77.5 kutoka duniani. Ni nyotamaradufu linayoweza kuonekana kwakutumia darubini ndogo ya mkononi kuwa ni kundinyota lenye nyota mbili zilizokaribiana. Jina lake latokana na Kiarabu ملكى malikiy "kifalme" [6] na جنوبى janubi "kusini"; jina la Kilatini "Regulus" linamaanisha "mfalme mdogo".
  • Beta Leonis (en:Denebola) iko upande wa kinyume wa kundinyota na jina la Kimagharibi ni mafupisho ya Kiarabu ذنب‌الاسد dhanab al asad "Mkia wa Simba". Ina uangavu unaoonekana wa 2.23 ikiwa na umbali wa miakanuru 36 kutoka kwa Dunia.[7]
  • Jabuha Asadi[8] (en:Algieba) au Gamma Leonis ni nyota maradufu yenye uangavu unaoonekana wa 2.08 ikiwa na umbali wa miakanuru 126 kutoka dunia. Jina lamaanisha ""paji la uso wa simba".
Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Aina ya spektra
α 32 Maliki Junubi (Regulus) 1,36m 78 B7 V
γ 41 Algieba 2,01m 126 K1 III + G7 III
β 94 Jabuha Asadi (en:Denebola) 2,14m 36 A3 V
δ 68 Zosma 2,56m 58 A4 V
ε 17 2,97m 251 G1 II
θ 70 Chertan 3,33m 170 A2 V
ζ 36 Adhafera 3,43m 260 F0 III
η 30 3,48m 2000 A0 Ib
ο 14 Subra 3,52m 116 A5 V
ρ 47 3,84m 2500 B1 Ib
μ Rasalas 3,88m 133 K2 III
ι 78 3,9m 70 F2 + G3

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Leo" katika lugha ya Kilatini ni "Leonis" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Leonis, nk.
  2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  3. Hinkley, Star-names and their meanings 252f
  4. Rogers, John H. 1998. "Origins of the Ancient Constellations: I. The Mesopotamian Traditions". Journal of the British Astronomical Association. 108 1: 9–28. Bibcode:1998JBAA..108....9R.
  5. ling. Knappert
  6. ling. Richard Hinckley Allen 1899, Star-Names and their Meanings uk. 256; ingawa Waarabu walitumia zaidi jina la qalb-al-asad" yaani moyo wa simba"
  7. Knappert hana jina la Kiswahili kwa nyota hii ingawa "Dhanabu ya Asadi" inawezekana kwa kulingana na "Dhanabu ya Ukabu"
  8. ling. Knappert

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 252 (online kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
Makundinyota ya Zodiaki
Majina ya kisasa yanafuatwa kwa mabano na jina la mabaharia na jina la Kilatini (la kimataifa)

Kaa (Saratani – Cancer )Kondoo (Hamali – Aries )Mapacha (Jauza – Gemini )Mashuke (Nadhifa – Virgo )Mbuzi (Jadi – Capricornus )MizaniLibra )Mshale (Kausi – Sagittarius )Ndoo (Dalu – Aquarius )Nge (Akarabu – Scorpius )Ng'ombe (Tauri – Taurus )Samaki (Hutu – Pisces )Simba (Asadi – Leo )