Sr. Jean Pruitt
Jean Pruitt amezaliwa tar 17 Oktoba 1939 katika jimbo la Kalifornia huko nchini Marekani. Ni mtoto wa pili katika familia ya watoto saba. Sr. Jean Pruitt ni sista wa jumuiya ya masista Wakatoliki wa Maryknoll huko Los Angeles. Ni raia wa Marekani anayefanya kazi na shirika la Maryknoll sisters chini ya Kanisa Katoliki Tanzania. Sr. Jean Pruitt ni mwanaharakati na mpiganiaji wa haki za watoto, Mwandishi wa vitabu na promota wa kazi za sanaa hasa kwa upande wa vijana nchini Tanzania. Sr. Jean alifika nchini Tanzania mwaka 1969. ni muasisi na mwanzilishi wa taasisi mbalimbali za kijamii ndani ya Tanzania.
Maisha ya awali
[hariri | hariri chanzo]Jean Pruitt amezaliwa tar 17, oktoba, 1939 nchini Marekani. Mwaka 1953 alihitimu katika shule ya Nativiti huko Los Angeles nchini Marekani, mwaka 1957 alihitimu kidato cha sita katika shule ya Bishop Conaty High School. Jean Pruitt alijiunga na shirika la Maryknoll sisters huko Los Angeles 1958 na baadaye mwaka 1967 alihitimu shahada ya Bachela ya elimu kwenye chuo cha Mary Rogers cha Maryknoll huko New York na Mwaka 1968 alihitimu na kupata shahada ya Ustawi wa jamii katika chuo kikuu cha Buffalo mjini New York nchini Marekani.
Taasisi alizoanzisha
[hariri | hariri chanzo]Sr. Jean Pruitt alitumwa Tanzania mwaka 1969 na jumuiya ya masista wa Maryknoll chini ya Kanisa Katoliki Tanzania, alianza kusaidia shughuli za Catholic Relief Services. Pamoja na kazi zake za kikanisa Sr. Jean Pruitt tangu awasili Tanzania, amekuwa chachu ya maendeleo ya vijana na watoto kwani ameanzisha taasisi nyingi sana ambazo zimeendeleza vijana wengi wasanii na zimeleta heshima kubwa ndani na nje ya Tanzania. 1971 Sr. Jean Pruitt alianzisha Nyumba ya Sanaa kama sehemu ya vijana kuonyesha kazi zao za kisanii na kuziuza. Nyumba ya sanaa lilikuwa duka la kwanza maalumu la ubunifu kwa vijana wa kitanzania kwa ajili ya kuonyesha na kuuza kazi zao za kisanii, huku wakipata ushauri na mwongozo kutoka kwa Sr. Jean Pruitt, Nyumba ya Sanaa ilianzia pale mtaa wa Mansfield. Sr. Jean Pruitt ni mmojawapo wa watu waliounda shirika la Caritas Tanzania 1972. Mwaka 1988 Sr. Jean Pruitt ni mmoja wa watu walioanzisha shirika lililojulikana kama Tanzania Mozambique Friendship Association (TAMOFA). Mwaka 1992 alianzisha Kituo cha kulelea watoto walio kwenye mazingira magumu cha Dogodogo Center, Mwaka 2000 Sr. Jean alianzisha shirika la Mtandao wa dini kwa watoto duniani kanda ya Afrika yaani GNRC - Africa. Sr Jean Pruitt alianzisha shirika hili baada ya kuhudhuria kwenye midahalo ya amani nchini Japan. Shirika hili lilianzia huko Japan kwa upande wa Africa Sr. Jean Pruitt ndiye muasisi wa kulitambulisha shirika hili nchini Tanzania. Shirika lingine aliloanzisha ni Stepping Stones Trust Fund Tanzania kwa ajili ya kusaidia jamii za wafugaji nchini Tanzania chini ya taasisi iitwayo EMUSOI.
Wasanii Maarufu aliowagundua
[hariri | hariri chanzo]Sr. Jean Pruitt aligundua vipaji vya wasaniii wengi sana hasa alipoanzisha Nyumba ya Sanaa. Wasanii aliyowagundua wanaojulikana na kitaifa na kimataifa ni George Lilanga. Huyu ni msanii aliyegunduliwa na Sr. Jean Pruitt pale nyumba ya Sanaa mwaka 1971. Ni msanii maarufu sana anayejulika nje na ndani ya nchi kwa kazi zake nzuri za sanaa ya uchoraji. Msanii mwingine aliyegunduliwa na Sr. Jean Pruitt ni Patrick Francis Imanjama ambaye anajulikana kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kazi zake nzuri za uchoraji wa picha za Etching, picha za rangi za maji na michoro ya kwenye vitabu. Patric amefanya maonyesho mbalimbali katika nchi za Ujerumani, Austria na New York chini ya Promota Sr. Jean Pruitt. Wasanii wengine ni Augustion Malaba, Henry Likonde na Edward Kiiza. Faili:Jean Pruitt .jpg
Tuzo alizopata
[hariri | hariri chanzo]Sr. Jean Pruitt amepata tuzo mbalimbali kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya jamii ya Tanzania. Mwaka 1983 alipata tuzo ya Taifa iliyojulikana kama National Award bestowed iliyotolewa na Mwalimu J.K.Nyerere kwa mchango wake wa kuendeleza viwanda vidogo vigodo SIDO. Tar 17 Desemba 2005, Sr. Jean Pruitt alipata tuzo ya Taifa ya ZEZE kwa kuendeleza wasanii na utamaduni wa Tanzania.
Marejeo ya Nje
[hariri | hariri chanzo]- Sister Jean Pruitt kwenye tovuti ya masista ya Maryknoll Ilihifadhiwa 25 Juni 2010 kwenye Wayback Machine.
- Muhtasari ya maisha na kazi ya Jean Pruitt Ilihifadhiwa 7 Februari 2011 kwenye Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Sr. Jean Pruitt kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |