Bi. Shakila

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Bi. Shakila
Taarifa za awali
Jina la kuzaliwaShakila Tatu Said Msengi
Pia anajulikana kamaShakila Tatu Said Msengi
Amezaliwa(1947-06-14)Juni 14, 1947
Tanga,Tanzania
Amekufa19 Agosti 2016 (umri 69)
Mbagala, Dar es Salaam, Tanzania
Kazi yakeMwimbaji, mtunzi
Miaka ya kazi1953–2016

Shakila Tatu Said Msengi (14 Juni 1947 - 19 Agosti 2016) alikuwa mwimbaji maarufu wa muziki wa Taarabu kutoka nchini Tanzania.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Bi Shakila alikuwa mzaliwa wa peke yake kwa baba na mama yake, alizaliwa tarehe 14 Juni 1947, tarehe moja na mwanamuziki mwingine mkongwe Mabruk Khamis wa Kilimanjaro Band anayejulikana kwa jina la Babu Njenje. Mama yake Babu Njenje alikuwa na tatizo la kutoa maziwa hivyo Babu Njenje alianza kwa kunyonyeshwa na mama yake wa Bi Shakila.

Kwa kadri ya maelezo yake mwenyewe Bi Shakila alianza muziki akiwa na miaka 6, alipokuwa na umri wa miaka 12, aliteuliwa kumuimbia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipotembelea Pangani, wakati wa kutafuta Uhuru. Na ni baada ya hapa ambapo aliweza kusikika na Bwana Khatibu ambaye aliweza kumshawishi kujiunga na kundi la Taarab lililokuwa pale Pangani lililoitwa Taarab Kijamvi, hakukaa sana katika kundi hilo akalazimika kuhamia Tanga kumfuata Bwana Khatib ambaye walibahatika kuzaa watoto watano.

Huko Tanga alijiunga na kundi la Shaabab Al Watan. Katika kundi hili hakupata nafasi ya kuimba katika kadamnasi, hivyo baada ya muda si mrefu Bi Shakila akiambatana ma mumewe walihamia kundi lililokuwa likimilikiwa na Mzee Kiroboto lililoitwa Young Noverty. Pamoja na Bi Shakila kupata uzoefu mkubwa wa kuimba mbele za watu kundi hili lilikuwa ni kutumbuiza bure katika vikao vya kahawa.

Hatimaye kundi hili lilikufa na zaidi ya nusu ya wasanii kujiunga na kundi la Black Star lililokuwa la mwarabu mmoja aliyekuwa anafanya kazi bandarini aliyeitwa Hassan Awadh na hapo ndipo Bi Shakila alipoanza kufahamika, na akapewa nyimbo kama Jongoo Acha Makuu, Mpenzi Amini, Majuto Yamenipata. Sifa zake zikaanza kuenea Afrika Mashariki. Mwaka 1972 tajiri mwingine Mwarabu aliyeitwa Sudi Said akanunua vyombo vipya vizuri na kuanzisha kundi la Lucky Star Musical Club, hapo Bi Shakila na wenzie tisa walihama Black Star na kuhamia Lucky Star.

Kwa kuwa kundi lilianzishwa wakati Bi Shakila alikuwa mja mzito, mtoto aliyezaliwa alimuita Lucky kwa ajili ya tukio hilo. Nyimbo nyingi zinazofahamika hadi leo za Bi Shakila zilirekodiwa wakati yuko kundi hili. Mapenzi Yamepungua, Kifo cha Mahaba, Macho Yanacheka. Bi Shakila aliendelea na kundi hili hadi mwaka 1984, Baada ya kifo cha mumewe alipumzika kwa muda kasha akahamia Dar es Salaam ambapo alijiunga na kundi la JKT alilodumu nalo mpaka alipostaafu.

Jioni ya tarehe 19 Agosti, 2016, Bi. Shakila alianguka ghafla na alipokimbizwa hospitali moja jirani na kwake Mbagala Charambe alipofika huko Bi Shakila alikata roho.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Bi. Shakila kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.