Soko la Kariakoo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Soko la Kariakoo jinsi linavyoonekana kwa mbali juu ya ghorofa
Kariakoo, Dar es Salaam katika miaka ya 1980/1970
Ndani ya soko la Kariakoo
Soko dogo (kulia) na Soko Kubwa katika miaka ya hivi karibuni, yaani, 2010 na kuendelea

Soko la Kariakoo ni soko kuu jijini Dar es Salaam na Tanzania ambapo kunafanyika biashara za aina zote za mahitaji muhimu ya kila siku ya binadamu. Biashara zinafanyika kwa jumla na rejareja. Soko hili linajumuisha majengo mawili makuu (soko kubwa na soko dogo) pamoja na maeneo yanazunguka majengo hayo. Soko la Kariakoo lipo katikati ya jiji la Dar es Salaam na ndiyo chanzo cha eneo zima la Kariakoo kujulikana kwa jina hilo. Jengo la Soko Kuu la Kariakoo lipo katika kiwanja namba 32 mtaani Kariakoo, katikati ya makutano ya mtaa wa Mkunguni na mtaa wa Nyamwezi na limezungukwa na mitaa ya Nyamwezi, Mkunguni, Sikukuu na Tandamti.

Historia ya soko[hariri | hariri chanzo]

Historia ya jina la Kariakoo na soko la Kariakoo inaanzia tangu enzi za ukoloni wa Mjerumani wakati Tanzania Bara ikiitwa Tanganyika.

Mahala lilipo soko hilo palijengwa jengo la utawala wa Wajerumani ambalo lilikusudiwa litumike kama ukumbi wa kuadhimisha sherehe za kutawazwa kwa Mfalme Kaiser Wilheim wa Ujerumani kwa wakati huo.

Hata hivyo baada ya jengo kukamilika halikutumika kama ilivyokusudiwa kuwa na badala yake lilitumika kama kambi ya kikosi cha wapagazi waliobeba mizigo ya vita kuu ya kwanza ya dunia waliojulikana kama Carrier Corps.

Jina hilo la maaskari wabeba mizigo katika Kiswahili lilitamkwa karia- koo na liliendelea kutumika kama jina la eneo lote linalozunguka jengo hili la Soko la Kariakoo.

Baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia kuisha rasmi mwaka 1919 na nchi Tanganyika kuanza kutawaliwa na Uingereza, jengo hilo lilianza kutumika kama soko na kuhudumia wakazi wa Dar es Salaam. Wakati huo wafanyabiashara walikuwa wakiuza bidhaa zao sakafuni kwa sababu hapakuwa na meza. Wafanyabiashara hao waliendelea kufanya biashara zao sakafuni hadi miaka ya 1960, meza za saruji zilipojengwa. Kwa kadiri jiji la Dar es Salaam lilivyokua na wakazi wake kuongezeka, ndivyo soko hilo lilielemewa kuhudumia wananchi.

Hali hiyo iliwafanya viongozi wa halmashauri ya jiji kuona haja ya kuwa na soko kubwa na la kisasa kulingana na maendeleo ya jiji, na hivyo wakaanza kujadili uwezekano wa kujenga soko jipya kubwa na la kisasa.

Ujenzi wa soko[hariri | hariri chanzo]

Uamuzi wa kujenga Soko Kuu la Kariakoo ulifanywa na serikali mwaka 1970 ambapo Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam iliagizwa kujenga soko jipya la kisasa ambalo lingechukua nafasi ya soko la zamani.

Matarajio ya serikali ya kujenga soko hilo yalikuwa ni kuwapatia wakazi wa jiji soko kubwa la chakula ambalo lingetosheleza mahitaji yao kwa muda wa miaka 50 hadi 70 Mipango ilikamilika na ujenzi ulianza rasmi Machi 1971.

Ramani ya jengo la soko ilitayarishwa na mchoraji wa ramani za majengo Mtanzania Beda Amuli. Kwa mujibu ya machapisho yanayoelezea historia ya soko hilo, mkandarasi huyo alitakiwa kwenda kujifunza katika nchi za Accra – Ghana na Lusaka-Zambia, kuangalia masoko yaliyojengwa katika miji hiyo miwili, ndipo atengeneze ramani yake, ambalo ndiyo soko linaloonekana hivi sasa. Mkandarasi aliyechora jengo hili ameweka baadhi ya maumbo yanayofanana na majengo hayo aliyokwenda kuyatazama. Hii ndiyo sifa pekee inalolifanya soko hili la Kariakoo kuwa la tofauti na masoko mengine katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Ujenzi wa soko ulikamilika Novemba 1975 kwa gharama ya shilingi milioni 22 na kufunguliwa rasmi Desemba mwaka huo huo ambapo Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mgeni rasmi.

Jengo la soko[hariri | hariri chanzo]

Soko hilo lina majengo mawili ambayo yameunganishwa katika Ghorofa ya chini ya ardhi. Jengo la kwanza linaweza kuitwa soko kubwa na jengo la pili soko dogo. Soko kubwa limegawanyika katika sehemu tatu ambayo ni ghorofa ya kwanza, sehemu ya katikati na ya chini maarufu kama shimoni. Eneo la Shimoni kuna mabucha 16 yanayouza nyama iliyokaguliwa kiafya toka mikoa ya Dodoma, Mwanza na Shinyanga, na samaki wabichi toka maziwa na mito ya Tanzania.

Soko dogo ni la rejareja ambalo si tofauti na masoko mengine katika Jiji la Dar es Salaam.

Ingawa eneo la Kariakoo limezungukwa na maduka yanayouza bidhaa mbalimbali, bado Soko la Kariakoo ndio soko kuu la mazao na bidhaa za kilimo nchini. Linauza mazao kwa bei ya jumla ya rejareja pamoja na vifaa vya kilimo.

Usimamizi wa soko[hariri | hariri chanzo]

Shirika la Masoko ya Kariakoo (SMK) linasimamia uendeshaji wa biashara za Soko la Kariakoo, kuweka kipaumbele katika shughuli za biashara mbili: Shirika linakodisha ardhi ya biashara kwa wauzaji wa Rejareja. Pia eneo la soko hilo lina maduka 82 katika soko kuu, yanayokodishwa kwa SMK kwa wauzaji wa rejareja. Mbali na mazao ya kilimo, maduka mengi yanauza vifaa vya kilimo na elektroniki. Pia, soko linatoa baadhi ya maduka nje yanayouza mboga za majani za rejareja katika soko dogo la nje. Kuhusu uendeshaji wake shirika hilo linasimamia soko la jumla kwa mazao ya kilimo na jamii ya samaki wakavu linalofanyika eneo la soko. SMK inatoza asilimia ya faida ambayo si zaidi ya asilimia nane tu ya bei ya mauzo kwa biashara ya jumla. Vile vile shirika linawatoza wafanyabiashara wa jumla ada ya usajili. Kwa masoko ya jumla na rejareja, Shirika linaweka daraja kati ya wakulima na wateja, ili wateja waweze kupata mahitaji yao yote ya nyumbani katika sehemu moja kwa bei nafuu na kuleta uthabiti kwa sekta ya kilimo ya nchi.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]