Takadini

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Takadini ni kitabu kilichoandikwa na Ben J. Hanson, mmojawapo miongoni mwa waandishi mashuhuri katika nchi za Afrika. Kilitolewa mara ya kwanza huko Harare (Zimbabwe) mwaka 1997.

Hii ni kazi ya riwaya ambayo huzungumzia matukio yanayotokea katika nchi za Afrika, hasa katika nchi ya Zimbabwe, ambapo watu wenye ulemavu wa ngozi, yaani zeruzeru, walikuwa wakiuawa kwa sababu ya kuamini mila na tamaduni zilizopitwa na wakati.

Kwa sasa tafsiri yake ya Kiswahili ni miongoni mwa vitabu teule katika shule za sekondari kidato cha tatu na cha nne nchini Tanzania.

Muhtasari wa kitabu cha Takadini[hariri | hariri chanzo]

Katika riwaya hii mwandishi ameweza kumzungumzia mzee Makwati, ambaye alikuwa na wake wanne. Wanawake hao ni Sekai (mke wa kwanza), Pindai (mke wa pili), Dadirai (mke wa tatu) pamoja na Rumbidzai (mke wa nne).

Kati ya wanawake hao wanne, watatu ambao ni Pindai, Dadirai, na Rumbidzai walibahatika kupata watoto, isipokuwa Sekai hakuweza kupata hata mtoto katika kipindi cha miaka tisa tangu kuolewa kwake.

Hali hiyo iilikuwa ikimnyima raha mzee Makwati kwani yeye alipenda sana kupata mtoto kutoka kwa Sekai, tena mtoto aliyekuwa akimtaka ni mtoto wa kiume, kwani wake zake wengine walibahatika kupata watoto wa kike.

Kitendo cha Sekai kukosa mtoto na kuendelea kupendwa na mumewe kilichukiwa na wake wenza ambao ni Dadirai na Rumbidzai: hao walimchukia sana Sekai kwa kuamini kuwa huenda alimpa dawa mume wao ili ampende zaidi mwanamke ambaye ni tasa. Kati ya wake wenza hao ni Pindai tu aliyekuwa anampenda Sekai.

Baada ya miaka tisa Sekai alipata ujauzito, kitendo hicho kilizidi kuwakasirisha Dadirai na Rumbidzai. Siku moja wakati Sekai akiwa anatapika nyuma ya kibanda, Dadirai na Rumbidzai walimwona Sekai akiwa anatapika. Dadirai na Rumbidzai wakaanza kutoa maneno ya kejeli. "Amai Chipo", Rumbidzai aliuliza ili kumuumiza roho Sekai, "ni ndama wangapi ambao ng'ombe wako mzee amepata kwa miaka minne iliyopita?" "Oh, amezaa watatu kwa miaka minne, Amai Tukai", Dadirai alijibu kwa sauti ya juu hata Sekai akasikia.

Mara zote Pindai, ndiye aliyekuwa anamfariji Sekai; wakati fulani alikuwa akimwelekeza Sekai asiwajibu kwani kinachowasumbua ni wivu. "Si ajabu: wale wawili wanahofia utapata mtoto wa kiume," Pindai alisema.

Wakati wa ujauzito wa Sekai, Makwati alikuwa na furaha zaidi kwani aliamini kuwa mke wake atamzalia mtoto wa kiume. Siku moja Makwati aliamua kumtembelea Sekai. Naye alijisikia vizuri na kutosheka ambapo Makwati alilala kando yake wakizungumza.

Ghafla kitoto kilicheza katika mfuko wa uzazi. Kwa msisimko mkubwa, Sekai aliutwaa mkono wa mumewe na kuutua juu ya tumbo lake. "Ha, mtoto ana nguvu huyu", Makwati alisema kwa mshangao. "Huenda atakuwa wa kike", Sekai alisema bila dhamira kubwa. Kauli ile ya Sekai ilimkasirisha sana mumewe. Makwati aliuliza kwa hamaki, "Unasemaje wewe mwanamke? Hapa tayari tuna idadi kubwa ya wanawake, mimi ninanyong'onyea kwa kuomba mtoto wa kiume". Hiyo ni dalili tosha iliyokuwa inaonesha kuwa mzee Makwati alikuwa anapenda mtoto wa kiume kuliko mtoto wa kike.

Hata wakati wa kujifungua kwa Sekai ulipofika walikuja wakunga wawili kwa ajili ya kumsaidia aweze kujifungua. Wakunga hao walikuwa Ambuya Tukai (Mkunga mkuu) na Ambuya Shungu (Mkunga msaidizi); aliyekwenda kuwaita wakunga hao ni Pedzisai. Wakunga hao walifika na kusubiri tukio la kujifungua kwa Sekai. Kadiri muda ulivyoongezeka lakini mtoto hakuwasili. Baada ya kusubiri, mtoto aliwasili: Ambuya Tukai alimwinua mtoto na kutangaza, "Ni mtoto wa kiume". Kitendo hicho kilimfurahisha sana Makwati baada ya kusikia kuwa mtoto wake aliyezaliwa ni wa kiume.

Kitu kikubwa tu ambacho wakunga wale walishangaa ni rangi ya mtoto. Kwa kawaida watoto wanapozaliwa huwa na ngozi nyepesi zaidi kuliko wazazi wao. Hata katika mwanga hafifu mtoto aliyewasili alikuwa na ngozi nyepesi zaidi, Ambuya Tukai alimtazama mtoto kwa makini akiwa mikononi mwa mama yake, alimsogelea Ambuya Shungu kisha akaonesha ishara kuwa "Mtoto ni musope. Ni wajibu wetu kumharibu!" Ambuya Shungu alistushwa na kauli hiyo, akamwambia Ambuya Tukai, "Kama ni hivyo tusifanye sasa, tumwache Sekai ahisi furaha mpya ya uzazi hadi kesho usiku; ni bora afurahie, japo kwa saa chache".

Pengine kauli ya Ambuya Shungu ndiyo iliyoleta uhai wa Takadini, kwani baada ya Sekai kupata nafuu kutokana na tukio lile la uzazi, Sekai alionekana ni mwenye furaha zaidi, kwani mtoto yule anaweza kumuondolea aibu ya kuonekana ni tasa katika jamii ile. Sekai alipopata nafuu, hakuamini kile alichokiona: alimtazama mtoto, aliona ngozi ni tofauti na kawaida. Alijionea kiumbe kama kilichopakwa mafuta, sawa na hatua ya kwanza ya mdudu atokapo katika yai. Tangu azaliwe Sekai hakuwahi kuona binadamu mwenye rangi nyepesi kama ile. Sekai alijiuliza, "Je, huyu ni mwanangu?"

Baada ya kutafakari kwa kitambo kuhusu asili ya mtoto wake, ghafla Ambuya Tukai aliingia ndani kwa Sekai na kugundua mashaka aliyonayo Sekai kwa mtoto wake. Ambuya Tukai alimsalimu Sekai, kisha Sekai alijibu salamu ya Ambuya Tukai. Sekai alimuuliza Ambuya Tukai, "Ambuya, nieleze ukweli, mtoto huyu ni wangu?" Ambuya alijibu,"Ndiyo,tumemtoa mtoto huyu mwilini mwako jana usiku." Macho ya Sekai yalibubujika machozi: "Lakini Ambuya, sijawahi kuona binadamu anayefanana na kiumbe huyu." Ambuya alimweleza Sekai kuwa hata yeye ameishi miaka mingi lakini hakuwahi kuona mtoto kama yule. Ambuya aliendelea kumweleza Sekai kuwa, "Ninachokumbuka, mwalimu wetu kiongozi aliwahi kutufundisha wakati nikichezwa unyago kuwa, mtoto kama huyu anazaliwa bila ngozi, mtoto yule aliondolewa na kutengwa mbali na mama yake." Kauli ile ilimshtua sana Sekai kwani alijua lazima mwanawe auwawe. "Hapana, Ambuya, lazima mtoto aishi: nimesubiri kwa muda mrefu na nimeshateseka sana juu yake, sitamwachia yeyote mwanangu."

Sekai alimuuliza Ambuya kama mumewe ameelezwa kuwa amejifungua mtoto wa kiume. Ambuya alimjibu Sekai kuwa mumewe ni mtu mwenye furaha kuu, bali hawafahamu atakachokifanya pale watakapomwambia kuwa mtoto wao ni musope! Hapo Sekai aliamua aende kwa mumewe kibandani mwake ili amueleze juu ya tukio lililotokea. Ambuya alijaribu kumzuia Sekai asiende kwa kuwa muda wa kuonana na mumewe ulikuwa bado. Sekai alitambua mila zao, lakini alitaka kuwahi kwa mumewe ili amueleze hali hiyo mapema zaidi. Sekai alimwachia mtoto Ambuya, moja kwa moja akaenda mpaka kibandani mwa Makwati akitaraji kumkuta. Wake wenza wote, pamoja na watoto wao hawakuwepo katika makazi hayo.

Sekai kibandani mwa Makwati[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kuoga na kujipaka mafuta, Sekai alikwenda mpaka kibandani kwa mumewe. Makwati alitabasamu baada ya kumuona Sekai akiwa pale. Sekai alimsogelea karibu mumewe, akapiga magoti na akapiga makofi pale viganja vya mikono yake vilipofunguka. Makwati alisema kwa furaha, "Mama wa mtoto wetu, umekijaza kibuyu changu furaha tele. Umeniweka juu kati ya watu wakati sikutarajia. Lakini mbona umekuja kuniona mapema hivi? Au mtoto wetu anaumwa?" Sekai huku akitazama ardhini alijibu, "Hajambo, mume wangu, isipokuwa tu..." alisita. Sekai baada ya kuona wasiwasi aliokuwa nao mume wake, ilibidi aeleze ukweli, akamueleza mume wake kuwa mtoto wao ni musope. Hapo Makwati, alimtazama mkewe kwa kutoamini kulikotisha sana. Hapo Makwati akahamaki, "Bila ngozi, Sope? Hilo sitalielewa. Inawezekanaje? Sema, we mwanamke! Ni kipi ulichokileta hapa kwetu? Kama unasema kweli, yupo wapi mtoto huyo? Ama ni uchawi au ni laana ya mizimu? Kwa nini huyo Sope yungali nasi?" Mfululizo wa maswali ulimfanya Sekai ashindwe kujibu! Lakini baadaye Sekai, huku akitokwa na machozi alinong'oneza, "Mume wangu, huyu ni mtoto wangu wa kwanza niliyemsubiri kwa miaka mingi, siwezi kukubali kumpoteza. La, humtaki, nirejeshe kwetu au hata msituni. Lakini usije kunilazimisha nitengane naye. Nitajitolea mhanga kwa ajili yake."

Sekai baada ya kusema hayo alijiinua kiasi hadi magotini kwa mumewe, lakini Makwati alijizuia kumsogelea na kumgusa mwanamke aliyempenda. Badala yake, Makwati alisema, "Tuliache suala hili hadi hapo tutakapomuona mtoto. Tutawauliza wazee jinsi ya kufanya baadaye." Baada ya maelezo hayo Sekai alirudi kibandani mwake, wakati huohuo Makwati aliamua kwenda nyumbani kwa Ambuya Tukai, ili kujua kuhusu mtoto yule.

Makwati nyumbani kwa Ambuya Tukai[hariri | hariri chanzo]

Baada ya mkewe kuondoka, na Makwati kupokea taarifa ambazo zilimchanganya kichwa kwa namna moja au nyingine, Makwati aliamua aende kwa Ambuya Tukai, ili aelezwe kuhusu taarifa za mtoto wake. Alipofika nyumbani kwa Ambuya, Makwati alitaka kujua kuhusu mwanawe mchanga. Ambuya alimweleza Makwati kuwa haamini kama mtoto hana ngozi, ngozi yake ni kama mche mchanga wa maharage uliochipua mizizi ghalani, au chungwa lililoanza kuiva, nywele zake ni sawa na asali iliyofifia. Ni kweli: ni wa ajabu, lakini anafanana na wewe kuliko ilivyo tofauti kati yetu."

Maelezo hayo, yalimchanganya sana Makwati. Makwati akawa anaamini, labda mke wake amelogwa au ni laana ya mizimu kwa kuwa ameishi na mwanamke tasa. Mwisho ilimbidi Ambuya Tukai amweleze Makwati kuwa, yeye kwa upande wake hilo halijui, labda aende kwa baba Zviyedzo (Nanga maarufu katika eneo la vijiji saba) Baada ya maelezo hayo, Makwati alijiandaa kuondoka na kumshukuru Ambuya kwa maelezo yake. Ambuya alimsisitiza Makwati kuwa asisahau kwenda kwa wazee ili waweze kuamua kitu cha kufanya kwanza.

Makwati nyumbani kwa Sekai[hariri | hariri chanzo]

Taarifa za kuzaliwa mtoto Sope ziliinea sana pale kijijini. Waswahili wanasema,"Habari njema huchechemea kwa mguu mmoja, lakini mbaya hukimbia kama sungura." Taarifa za kuzaliwa mtoto Sope, ziliwafurahisha sana Dadirai na Rumbidzai, kwani wao walikuwa na chuki zaidi dhidi ya Sekai. Jioni hiyo Makwati hakwenda kupiga gumzo na wazee wenzie katika dare. Giza lilipoenea na kijiji kilipokuwa kimya, Makwati aliamua kuvunja ukimya na kwenda kibandani kwa Sekai. Akamkuta ameketi mkekani, akimnyonyesha mtoto. Baada ya kufika Makwati, Sekai alimwinua mtoto ili baba yake amuone. Makwati alimwangalia yule mtoto, punde aliinua mikono na kuufunika uso wake kama anafukuza pepo. Makwati, baada ya kumuona mtoto, hatimaye alimudu kusema: "Sekai, umemfanya nini mwanangu? Umekuwa ukifanya jambo gani? Tafadhali nijibu." Jibu pekee la Sekai lilikuwa ni kilio, mpaka machozi yakawa yanamtiririka kidevuni na kumlowesha mtoto. Tuhuma hizo zilimfanya Sekai ajibu uchungu wake, "Maneno yako yanauma sana, yananila mifupa yangu. Unafahamu mapenzi yako yana maana gani kwangu. Unajua siku zote nilivyotaka kuwa wa kwanza kukupa mtoto wa kiume. La, kama ningekuwa na uhusiano wa mwanamume mwingine, lazima ungetambua."

Makwati alihuzunika sana juu ya hilo, kwani kitu alichokuwa akikitaka ni mtoto wa kiume; ni kweli, Makwati alishampata mtoto wa kiume, lakini tatizo, mtoto alikuwa ni Sope! Jamii ilikuwa inaamini kuwa kupata mtoto kama yule ni laana ya mizimu. Makwati akamueleza Sekai, "Lakini Sekai, endapo wataamua mtoto auawe, hata nawe utauawa kwa kupinga sheria za kale! Baada ya maelezo hayo, Makwati alitoka kibandani kimyakimya. Sekai alijihisi mwenye kutelekezwa, kwa wakati huo; maneno ya mumewe yalimtisha sana. Kutokana na mila na desturi za jamii ile, Sekai alijua kuwa lazima mambo mawili yatatokea, kati ya kuuawa mwanawe au yeye pamoja na mwanawe. Kwa kuwa Sekai hakuwa tayari mwanawe auawe, aliamua kujiandaa kutoroka kijiji chake na kukimbilia eneo asilolijua.

Asili ya jina "Takadini"[hariri | hariri chanzo]

Jina TAKADINI lina maana ya "Sisi tumefanya nini?" Jina hili limetokana na kitendo cha Sekai wakati anajiandaa kutoroka kijijini kwao na kwenda mahali asikokujua, kwa ajili ya kukimbia adhabu ya kuuawa kwa mwanawe. Mwandishi anasema kuwa, Sekai alikwishaamua aondoke asubuhi inayofuata, uamuzi wake wa kutoroka ulikamilika kwa usahihi na ushwari. Alimfunika mtoto wake katika gudza na kumtia mkekani. Kisha akafanya maandalizi ya safari yake. Alichukua mkuki pamoja na ngao na nyama iliyokaushwa kwa ajili ya safari yake. Sauti ya jogoo aliyewika katika eneo hilo ilimuamsha. Sekai alimnyonyesha mtoto wake, kisha aliketi kuiambia mizimu matatizo yake akaomba akingwe na watu na wanyama katika safari yake ya hatari. Wakati akiwasiliana na mizimu, punde jina likamjia moyoni taratibu, TAKADINI. Ni jina ambalo hakuwahi kulisikia mahali popote. Huo ulikuwa ndio mwanzo wa Sekai kuanza safari ya kutoroka kijijini kwao.

Sekai akiwa njiani[hariri | hariri chanzo]

Uamuzi wa kutoroka ulipokamilika, Sekai alimbeba mtoto wake na kuifuata njia ambayo kimsingi ilikuwa pori. Kwa bahati siku hiyo Sekai hakuweza kukutana na wanyama wowote wakali. Tukumbuke kuwa Sekai anayafanya yote haya ili kujinusuru yeye pamoja na mwanawe ambao walitajiwa kuuawa kwa sababu ya kuvunja utamaduni wa watu wa Makwati.

Wakati huo katika kijiji alichotoroka Sekai, hakuna mtu aliyejua kuwa ametoroka. Rumbidzai alikuwa na chuki na hukumu dhidi ya Sekai. "Leo tutaona kama yule mchawi atakwepa hukumu ya wazee" Rumbidzai alisema.

Akiwa anaendelea na safari yake, wakati fulani Sekai alipumzika kidogo kumnyonyesha mtoto wake. Punde si punde Sekai alishtushwa na mlio wa vipande vya miti. Sekai alisimama akaziba na pumzi zake na kuisubiri sauti ile isikike tena; ghafla akamwona mze mmoja akikusanya kuni.

Makala hii kuhusu mambo ya fasihi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Takadini kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.

h