Maafa asilia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Maafa asilia ni matukio yanayosababisha mabadiliko kwenye uso wa ardhi au angahewa ya dunia yanayoleta hasara kubwa kwa mali na maisha ya binadamu, na sababu zake ni za kiasili. Mifano yake ni tetemeko la ardhi, banguko, kimbunga, mafuriko, tsunami, mlipuko wa volkeno au pigo la asteroidi. Matukio hayo yote si lazima yawe maafa kwa maana yakitokea mahali pasipo na wanadamu na kutosababisha hasara kwa watu basi hayaitwi "maafa".

Maafa ya asili na maafa yaliyosababishwa na binadamu

Kuna maafa mbalimbali yanayosababishwa na binadamu na sababu za kibinadamu huingiliana na maafa asilia:

Mara nyingi ni matendo ya binadamu yanayofanya tukio la kiasili kuwa maafa makubwa kwa mfano ujenzi wa makazi katika mazingira ya volkeno hai (mfano: mji wa Napoli, Italia kando ya Vesuvio) au penye mipaka ya mabamba ya gandunia inayojulikana kama vile Los Angeles, Marekani.

Tetemeko la ardhi

Tetemeko la ardhi (pia: zilizala) ni mishtuko ya ghafla kwenye ganda la dunia. Likifikia ukali fulani ni hatari hasa kwa majengo. Hatari kwa binadamu hutegemea ubora wa majengo. Vifo vingi vinaweza kutokea wakati majengo yanaporomoka na kujeruhi au kuua watu. Hata tetemeko kali haliui watu waliopo porini katika tambarare ingawa linatisha.

Nguvu ya tetemeko la ardhi hupimwa kwenye skeli ya 0-9 au zaidi[1].

Nguvu ya uharibifu inaweza kutofautiana sana. Kwa mfano, tetemeko la ardhi lenye nguvu ya 6.4 liliharibu mji wa Bam, Iran mwaka 2003 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40,000. Lakini tetemeko huko Northridge, Kalifornia ya mwaka 1994 ilikuwa na nguvu ileile ila ni watu 60 tu waliofariki[2]. Tofauti ilikuwa ubora wa majengo katika maeneo yaliyohusika. Ilhali takriban wanafunzi 10,000 walifariki, huko Marekani shule zote zilisimama. Athira nyingine ilikuwa hali ya huduma za dharura na muda wa mahanga kukaa chini ya kifusi cha majengo.

Uharibifu baada ya banguko huko Venezuela mwaka 1999.

Banguko

Banguko ni kiasi kikubwa cha mawe, ardhi, theluji au barafu kinachoanza kuteleza kwenye mtelemko wa mlimani na kuelekea bondeni. Banguko unaweza kusababishwa na tetemeko la ardhi, kuyeyuka kwa theluji mlimani au mvua kali.

Banguko kubwa la mwaka 1999 nchini Venezuela liliharibu nyumba zaidi ya 8,000 na kuua idadi ya watu isiyojulikana lakini imekadiriwa kuwa kati ya watu 10,000 hadi 30,000[3]. Mwaka 2010 banguko kwenye mitelemko ya mlima Elgon huko Uganda likaua watu zaidi ya 100.[4]

Kimbunga na tufani

Tufani na kimbunga ni aina za dhoruba zenye mwendo wa kuzunguka. Zinatokea hasa katika kanda la tropiki la dunia. Zinaleta upepo mkali mno pamoja na kiasi kikubwa cha mvua. Zinaweza kubomoa nyumba, kuvuta watu na hata magari hewani na kuleta mafuriko makali.

Tufani ya Katrina ya mwaka 2005 iliharibu mji wa New Orleans huko Marekani, ikasabisha vifo zaidi ya 1,200 na hasara ya mali ya takriban dolar za Marekani bilioni 108[5] [6].

Mafuriko

Mafuriko katika eneo la TAZARA, Dar es Salaam, Tanzania.
Mafuriko huko Jangwani jijini Dar es Salaam.

Mafuriko ni hali ya kuwa na maji mengi yanayofunika nchi kavu isiyo na maji kwa kawaida.

Mafuriko yanaweza kutokea

  • popote baada ya mvua kali inayoteremsha maji mengi yasiyo na njia ya kupotea, hasa baada ya kutelemka penye mlima au mtelemko
  • kando ya mto ama baada ya mvua kali au wakati wa mvua nyingi au kwenye majira ya kuyeyuka kwa theluji
  • kando ya ziwa au bahari kama upepo mkali unasukuma maji kuelekea pwani, hasa pamoja na kutokea kwa maji kujaa au bamvua

Mafuriko mara nyingi ni hatari kwa binadamu, huleta hatari kwa uhai, mali na nyumba.

Njia za kujiokoa ni pamoja na kuhama haraka sehemu za mabondeni kwenda penye miinuko au nchi ya juu zaidi. Watu waliozoea mafuriko wana mbinu za pekee kama vile kujenga vizuizi vya maji kupanda juu, kuchimba mifereji inayopeleka maji mbali au kujenga nyumba juu ya vilima wakijua hakuna njia ya kuzuia mafuriko.

Tsunami

Tsunami ni wimbi kubwa sana katika bahari inayosababishwa na tetemeko la ardhi, mlipuko wa volkeno au matokeo mengine yanayoleta mshtuko wa ghafla chini ya maji. Mshtuko huo unapita ndani ya maji si hatari sana kwa meli baharini maana haubadilishi mno uso wa bahari. Lakini pale unapokutana na nchi kavu au kufikia sehemu ambako kina cha maji kinapungua kuna wimbi kubwa linalotokea na hii ni hatari kwenye pwani ambako wimbi hilo linafikia.

Tsunami inaweza kutokea pia baada ya banguko la mtelemko mkubwa kwenye pwani ya bahari au ziwa. Kabla ya kipindi cha kihistoria kulikuwa pia na tsunami zilizosababishwa na mgongano wa gimba la angani na uso wa dunia.

Tsunami zimewahi kutokea mara nyingi duniani. Kati ya taarifa za kwanza zilizotambua uhusiano kati ya tetemeko la ardhi na tsunami ni mwandishi Thukidides wa Ugiriki ya Kale[7] mnamo mwaka 426 KK.

Tsunami kubwa iliyotazamwa kwa msaada wa vifaa vya kisayansi ni Tsunami wa Krismasi 2004 katika Bahari Hindi iliyoua maelfu ya watu kuanzia Indonesia, Sri Lanka, Thailand na India hadi Somalia na Kenya. Ilisababishwa na tetemeko la ardhi kutokana na mwendo wa mabamba ya gandunia, hapa bamba la Burma chini ya bamba la Uhindi.

Mlipuko wa volkeno

Mwendo wa lava kutoka shimo la volkeno kwenye kisiwa cha Iceland, mnamo 1984.

Mlipuko wa volkeno ni kutokea vikali kwa lava na gesi kutoka ndani ya ganda la dunia. Volkeno hupatikana pale ambako vipande vya ganda la dunia vinaachana au kusukumana. Kuna pengo ambako magma joto kutoka ndani ya dunia inapanda juu kufika usoni.

Hii inaweza kutokea polepole lakini ikitokea kwa ghafla inaleta maafa katika mazingira yenye makazi ya watu.

Milipuko ya volkeno mbalimbali zinaweza kutofautiana kutegemeana na aina ya volkeno na hasa aina ya magma na lava zinazotoka nje.

  • Kuna milipuko mikali inayorusha kiasi kikubwa cha mwamba wa joto katika umbali wa kilomita kadhaa.
  • kuna milipuko inayorusha majivu ya moto inayofunika kila kitu na kuganda kuwa mwamba tena.
  • kuna milipuko ambako mto wa lava unatoka nje
  • kuna gesi za sumu zinazotoka nje na kuua kila uhai kwenye njia yake.
  • nguvu ya mlipuko inaweza kurusha miamba yenye kiasi cha kilomita za ujazo katika mazingira ya volkeno na kubadilisha uso wa dunia; mfano ni mlipuko wa mlima Krakatau huko Indonesia mwaka 1903; kisiwa cha Krakatau kilipotea kabisa.

Pigo la asteroidi

Dunia yetu inazunguka Jua letu katika anga-nje. Hapa inakutana mara kwa mara na violwa vinavyoanguka kwenye angahewa na kuonekana kama vimondo. Vingi ni vidogo, hivyo havileti hasara.

Lakini kiolwa kinachogonga Dunia kikiwa kikubwa kama asteroidi hatari ni kubwa. Migongano hiyo hutokea mara chache sana lakini sayansi imetambua ya kwamba pigo la asteroidi kubwa miaka milioni 66 iliyopita lilisababisha kuangamia kwa spishi nyingi, zikiwa pamoja na dinosauri. Pigo hilo lilirusha kiasi kikubwa cha vumbi kwenye angahewa pamoja na kusababisha milipuko ya volkeno nyingi na kuleta mabadiliko ya tabianchi kwa miaka kadhaa, hivyo kushusha halijoto duniani na kusababisha giza kwa muda mrefu.

Katika karne iliyopita kulikuwa na matukio mawili yaliyoonyesha nguvu haribifu ya violwa kutoka anga-nje:

  • mwaka 1908 kimondo kikubwa au asteroidi ndogo iligonga eneo la Tunguska huko Urusi na kuangamiza kilomita za mraba 2,000 za misitu, Kwa bahati nzuri wakati ule hapakuwa na watu katika eneo la Tunguska.
  • Mwaka 2013 kimondo kilichokadiriwa kuwa na kipenyo cha mita 17 pekee kilisababisha uharibifu kwa kulipuka juu ya mji wa Chelyabinsk nchini Urusi. Watu 1,500 walijeruhiwa, hasa na vioo vya madirisha vilivyopasuka kote mjini wakati wa mlipuko. Nyumba nyingi ziliathiriwa.

Kutambuliwa kwa hatari hii imesababisha mataifa mbalimbali kushirikiana katika mipango ya kutambua mapema violwa vinavyokaribia Dunia.

Marejeo

  1. Matetemeko makali yaliyopimwa yalipita kidogo kiwango cha 9; matetemeko makali zaidi yanawezekana lakini hayakupimwa bado
  2. Taarifa ya US Geological Survey. Jalada kutoka ya awali juu ya 2016-04-05. Iliwekwa mnamo 2015-10-06.
  3. Taarifa ya US Geological Survey
  4. Taarifa ya Reuters News. Jalada kutoka ya awali juu ya 2012-10-12. Iliwekwa mnamo 2015-10-06.
  5. Utathmini wa vifo kutokana na Katrina (2008). Jalada kutoka ya awali juu ya 2015-08-31. Iliwekwa mnamo 2015-10-06.
  6. THE DEADLIEST, COSTLIEST, AND MOST INTENSE UNITED STATES TRO PICAL CYCLONES FROM 1851 TO 2010, US WeatherService
  7. Thucydides, History of the Peloponnesian War , Thomas Hobbes, Ed. online

Viungo vya nje

Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu: