Uzazi wa mpango kwa njia asilia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Uzazi wa mpango kwa njia asilia maana yake ni mbinu zile za kuzuia mimba isipatikane katika tendo la ndoa ambazo zinafuata maumbile tu.

Njia asilia za kupanga uzazi ni mbinu ambazo hazihusishi vifaa wala kemikali, bali zinategemea ufahamu wa uwezo wa mwanamke kupata au kutopata mimba wakati wa kufanya tendo la ndoa.

Wanawake ambao wananyonyesha na wanapenda kukwepa mimba wanaweza kufanya tendo la ndoa kwa kutegemea kukatizwa kwa hedhi wakati wa kunyonyesha.

Mbali ya huo ujuzi wa jumla, uzazi unaweza kupangwa kwa kutofanya tendo la ndoa siku 13 hivi ambapo katika mzunguko wa hedhi kuna uwezekano wa kupata mimba.

Kinyume chake wanandoa wanaweza kulenga uzazi kwa hakika zaidi wakifanya tendo la ndoa kwa kutumia vizuri siku zinazouwezesha.

Vilevile wanaweza kuchagua jinsia ya mtoto mtarajiwa kwa kufanya tendo la ndoa siku ambapo kwa kawaida mbegu ya jinsia hiyo ndiyo inayowahi kuungana na kijiyai katika tumbo la uzazi.

Ujuzi wa kisayansi

Ni kwamba mizunguko mingi ya hedhi huwa na siku kadhaa za mwanzo ambapo mimba haiwezi kupatikana (muda wa kutoshika mimba kabla ya kudondosha kijiyai), halafu siku ambazo mimba inaweza kutungika, na kisha siku kadhaa tu kabla ya hedhi ambazo mimba haiwezi kutungika (muda wa kutoshika mimba baada ya kijiyai kudondoshwa). Siku ya kwanza ya kuvuja damu inahesabiwa kuwa siku ya kwanza ya mzunguko wa hedhi.

Mbinu za kubaini siku ambazo mwanamke hawezi kupata mimba zinajulikana tangu zamani (kuna maandishi ya mwaka 388 BK), lakini ujuzi wa kisayansi uliopatikana katika karne ya 20 umeongeza idadi na hasa usahihi wa mbinu hizo.

Kuna mbinu mbalimbali za kutambua wakati mwanamke anapoweza kushika mimba na asipoweza kushika mimba, lakini kwa jumla zinatumia ama dalili za msingi za uwezekano huo, ama historia ya mzunguko, ama njia zote mbili pamoja.

kalenda ya mwezi

Mbinu zinazotegemea dalili

Mbinu kadhaa hutegemea uchunguzi wa mabadiliko yanayoashiria uwezekano wa kutunga mimba kwa kufuatilia mzunguko wote wa hedhi na hivyo kubaini wakati ambapo inawezekana kushika mimba.

Dalili tatu za msingi za uwezekano wa kushika mimba ni joto msingi la mwili, ute wa uke na mkao wa mlango wa kizazi. Wanawake wengi hung'amua pia dalili nyingine za ziada kulingana na mzunguko wa hedhi, kama vile maumivu na uzito tumboni, maumivu mgongoni, ulaini wa matiti na maumivu ya kudondosha kijiyai.

Inawezekana pia kufanya uchunguzi wa mkojo kwa kutumia vifaa vya kubashiri udondoshwaji wa kijiyai, na uchunguzi wa ute au ugiligili wa seviksi kwa kutumia hadubini.

Isitoshe, ipo njia ya kufuatilia uwezo wa kushika mimba kwa tarakilishi.

Inapotumika kwa usahihi, na kuendana na mafundisho endelevu, baadhi ya tafiti zimeonyesha mbinu fulani za namna hiyo kuwa na 99% za ufanisi.

Mbinu zinazotegemea kalenda

Pia kuna mbinu zinazotegemea kalenda, ambazo hufuatilia mzunguko wa hedhi na kwa kuzingatia urefu wake hutambua mwanamke anapoweza kupata mimba. Mbinu hizo si madhubuti kama mbinu zinazotegemea dalili, hasa kwa baadhi ya wanawake na ya vipindi vya maisha yao.

Sifa za njia asilia

Uzazi wa mpango kwa njia asilia una sifa bainifu kadhaa:

  • Unaweza kutumika kudhibiti afya ya uzazi, kwa kuwa mabadiliko katika mzunguko wa hedhi yanaweza kumtahadharisha mtumiaji kuhusu kujitokeza kwa matatizo ya kike.
  • Unaweza kutumiwa na wanawake wote katika kipindi chote cha uzazi, bila kujali kama anakaribia kumaliza kuzaa, ananyonyesha, au anapata mzunguko wa hedhi usio wa kawaida kwa sababu nyingine.
  • Unaongeza ufahamu wa jinsi mwili wa mwanamke unavyofanya kazi, na unamwezesha kudhibiti zaidi uzazi wake mwenyewe.
  • Hauna madhara yoyote, tofauti na yale mengi yanayotokana na teknolojia inayotumiwa na mbinu nyingine.
  • Hauna gharama au ni nafuu sana ikilinganishwa na mbinu nyingine.
  • Unakubaliwa na wengi upande wa maadili kwa kuwa haupambani na umbile lilivyopangwa na Mungu.

Njia ya kupanga jinsia ya mimba

Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba unaweza kutumika pia kwa lengo la kupata mimba ya jinsia inayotamaniwa zaidi.[1]

Maharusi wanaweza kuchagua mtoto wa kiume au wa kike kwa 85% ya hakika wakifanya tendo la ndoa kwa kupanga kulingana na ute wa uke kuwa wa kuvutika na kuteleza au siyo.

Ni kwamba jinsia ya mimba inategemea tu kromosomu za mbegu za baba ambazo ni nusunusu: X kwa kuzaa watoto wa kike na Y kwa kuzaa watoto wa kiume. Mbegu zenye kromosomu X ni dhaifu kidogo nazo huogelea polepole, lakini zinaishi muda mrefu. Kumbe zenye kromosomu Y zina nguvu zaidi na kuogelea upesi, lakini hufa upesi.

Ili kupata mtoto wa kiume

Kwa kuzingatia tabia hizo mbili tofauti, maharusi wakitaka mtoto wa kiume wanatakiwa kufanya tendo la ndoa siku ya kwanza baada ya kilele (kujisikia kuteleza) na kuendelea kwa miandamo 6 ya hedhi. Kama mwanamke hajapata mimba baada ya miandamo 6, waanze kuonana siku ya kilele na siku inayofuata. Kama mwanamke amekosa siku ya kilele, yaani kama utelezi wa ute unaendelea siku inayofuata, waonane tena siku inayofuata.

Kwa njia hiyo mbegu zenye kromosomu Y tu zitafikia kijiyai kilichochopoka, kwa sababu mbegu zenye kromosomu X zinaogelea polepole tu.

Ili kupata mtoto wa kike

Kinyume chake, wakitaka mtoto wa kike wanatakiwa kufanya tendo la ndoa siku ya kwanza ya ute wa uzazi. Halafu wapumzike mpaka siku ya nne baada ya kilele. Waendelee hivyo kwa miandamo michache.

Kama mwanamke hajapata mimba baada ya miezi michache, wafanye tendo la ndoa siku ya kwanza na ya pili ya ute wa uzazi halafu wapumzike mpaka siku ya nne baada ya kilele. Waendelee hivyo kwa miandamo michache. Kama mwanamke hajapata mimba baada ya miezi michache, wafanye tendo la ndoa pia siku ya tatu ya ute wa uzazi halafu wapumzike mpaka siku ya nne baada ya kilele. Waendelee hivyo kwa miandamo michache.

Kwa njia hiyo mbegu zenye kromosomu Y zitakufa kabla ya kuweza kuungana na kijiyai, na hivyo zitabaki zenye kromosomu X kuwa na nafasi hiyo.

Siku nzuri ya kupata mtoto wa kike ni kufanya tendo la ndoa siku mbili kabla ya kilele cha utelezi.

Tanbihi

  1. Ursula Birgitta Schnell OSB (2011). Uimarishaji wa Familia - Mpango wa uzazi kwa njia ya asili Billings Ovulation Method (toleo la 15th). Ndanda, Tanzania: Benedictine Publication Ndanda-Peramiho. ISBN 9976-63-132-4. 

Marejeo

Kwa Kiswahili

Kwa Kiingereza