Wikipedia:Makala ya wiki/Kimondo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kimondo cha chuma kilichopatikaka huko Tuva, Urusi

Vimondo (pia: meteori au meteoridi) ni magimba madogo ya angani yanayozunguka jua. Yanaweza kuangukia duniani yakionekana kama moto angani. Ukubwa wa kimondo ni kuanzia punje ya mchanga hadi kufikia kipenyo cha mita kadhaa. Hivyo kimondo ni kidogo kuliko asteoridi na kikubwa kushinda vumbi la angani. Obiti ya kimondo inaweza kuingiliana na obiti ya dunia au sayari nyingine. Kimondo kikilikaribia gimba la angani kubwa zaidi kinavutwa nalo. Kikikaribia mno dunia yetu kinaingia katika angahewa na kuanguka chini kwa kasi kubwa sana. Njiani kinapashwa moto kutokana na shindikizo la hewa dhidi yake. Kiasi cha joto kinatosha kuchoma kabisa kimondo kidogo hewani. Hii inaonekana kwa macho matupu kama mstari wa moto angani. Kama kimondo ni kikubwa zaidi ni sehemu zake za nje tu zinazochomwa na kiini kinagonga uso wa dunia. Kati ya vimondo kumi vikubwa kabisa duniani ambavyo mabaki yake yanaonekana, kimojawapo ni Kimondo cha Mbozi nchini Tanzania. ►Soma zaidi