Wikipedia:Makala ya wiki/Kikingaradi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Kikingaradi

Kikingaradi ni kifaa kinachofungiwa juu ya nyumba, minara au majengo marefu mengine. Kwa kawaida ni nondo nene ya metali ambayo inaunganishwa na waya inayoishia kwenye pao la metali lililochimbwa ardhini.

Kazi ya kikingaradi ni kuvuta radi kwake na kuifikisha ardhini bila kupita ndani ya jengo. Radi ina kiwango kikubwa cha chaji ya umeme ndani yake na inaweza kusababisha uharibifu mkubwa kwenye kitu kinachopigwa naye. Pale ambako radi inatokea chaji yake inatafuta njia ya haraka ya kuingia kwenye ardhi kwa shabaha ya kutoa chaji yake. Hapo mara nyingi radi inatafuta vilele vya majengo au pia miti ambayo ni kama sehemu ya juu ya uso wa ardhi. Kuachiliwa kwa chaji katika jengo au mti kunaweza kuleta uharibifu. Mkondo wa umeme unaopatikana wakati wa kuachilia chaji unasababisha halijoto kali inayosababisha moto. Kama kuna unyevu ndani ya ukuta wa jengo unyevu huu unaanza kuchemka mara moja na kuwa mvuke kwa ghafla kunachosababisha mlipuko.

Hapo kikingaradi ni njia ambako umeme unaweza kupita na kufika ardhini haraka bila kutafuta njia ndani ya jengo. Ilhali radi daima inatafuta njia ya haraka ya kuachilia chaji yake ardhini kikingaradi kinatengenezwa kwa metali inayopitisha umeme haraka zaidi kuliko jengo lenyewe. Kwa sababu hii metali inayochaguliwa kwa kikingaradi ni kwa kawaida shaba, aloi za shaba au alumini, kwa kwa sababu metali hizi zina ukinzani mdogo kwa mkondo wa umeme. Shaba ni bora kuliko alumini lakini bei yake ni juu zaidi. ►Soma zaidi