Wasaksoni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Wasaksonia)
Ramani ya Dola la Roma na makabila ya Ulaya mwaka 125 BK, ikionyesha makazi ya Wasaksoni kaskazini mwa Ujerumani.

Wasaksoni (kwa Kilatini Saxones, kwa lugha za Kijerumaniki Seaxe, Sahson, Sassen, Sachsen, Saksen, kutoka "seax", jina la kisu maalumu walichotumia) walikuwa shirikisho la makabila kadhaa ya Wagermanik wakazi wa Ujerumani Kaskazini walioenea katika sehemu za jirani.

Baadhi yao, pamoja na jirani zao Waangli, jumla watu 200,000 hivi, walivamia Britania katika karne ya 5 BK na baada ya hapo, wakiweka msingi wa Uingereza wa leo.

Wengine wao walibaki katika Ujerumani ya Kaskazini wakapingana na milki ya Wafaranki na hatimaye kushindwa na Karolo Mkuu.

Katika karne ya 9 utemi wa Saksonia ulianza kuwa muhimu katika milki ya Ujerumani hadi mwaka 919 mtemi Heinrich I alichaguliwa kuwa mfalme wa Ujerumani.

Watawala Wasaksoni waliendelea kuongoza milki ya Wajerumani hadi mwaka 1024 hata kuchukua cheo cha kaisari chini ya Otto I.

Baadaye mtemi wa Saksonia alishindana na Kaizari Federiki I na utemi wa Saksonia uligawiwa. Cheo cha "Mtemi wa Saksonia" kilibaki na mtawala wa eneo dogo tu na kwa njia ya urithi cheo kilihamia katika kusini-mashariki mwa Ujerumani.

Tangu siku zile jina la "Saksonia" linataja maeneo upande wa kusini wa Berlin ya leo. Maeneo ya Saksonia asili (kaskazini-magharibi mwa Ujerumani) leo hii hujulikana kwa jina la "Saksonia Chini".

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]