Wallah bin Wallah

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Wallah bin Wallah (amezaliwa 1952[1]) ni mwandishi wa Kiswahili kutoka Kenya anayetambulika kwa jina la Ustadh (profesa) kwa hatua zake katika kuimarisha lugha ya Kiswahili katika jamii ya Afrika Mashariki.

Mwalimu Wallah bin Wallah ameandika vitabu vya Kiswahili Mufti na Insha Mufti vinavyotumika katika shule za msingi. Vile vile ameyaandika mashairi katika kitabu chake ‘Malenga wa Ziwa Kuu’ pamoja na vitabu vya hadithi fupi kama vile Zawadi ya Sanda, Sitaki Simu, Tumgidie Bwege na vinginevyo.

Wallah alianzisha wakfu ya tuzo za Wasta mwaka 2010 ambako anawatuza wanaojitahidi kukitumia Kiswahili kwa umakini.[2]

Utoto na elimu[hariri | hariri chanzo]

Wallah bin Wallah alizaliwa mwaka 1952 kule Nyakach, wilaya ya Nyando. Jina alilopewa na wazazi wake lilikuwa Ndedah lakini alilibadilisha baadaye maana aliliona kana kwamba lilikuwa likimsaliti kama mkabila. Alilichukua jina la babake Wallah na baadaye akaona ni vyema kujiita Wallah mwanawe Wallah. Hivyo, jina Wallah bin Wallah likakita mizizi.

Wallah alisomea nchini Tanzania maana alifuatana na baba yake aliyekuwa akifanya kazi na kampuni ya reli ya Afrika Mashariki huko Tanzania. Alijiunga na shule ya msingi ya Lukungu alikosomea kutoka darasa la kwanza hadi la nne. Baadaye alijiunga na shule ya Bukumbu alikosomea hadi darasa la saba na kuhitimu katika mtihani wa G.E.E.

Maisha ya Wallah shuleni hayakuwa mepesi maana babake hakuwa akimpa msaada na mara kwa mara, Wallah alijilipia karo. Alifanya hivi kwa kuchuuza samaki pamoja na kuwanyoa wenzake ili apate pesa. Baada ya shule ya msingi, alijiunga na shule ya seminari ya Nyegezi ambako alikuwa akisomea somo la dini ya Kikristo.

Hakumaliza hayo masomo maana aling'amua kwamba kama angetaka kuendeleza ujuzi wa Kiswahili, alifaa awe Mwislamu. Aliiacha shule na kurudi Kenya alikojiunga na shule ya upili ya Ravals, Latema. Aliweza kupata diploma ya ualimu katika chuo cha Morogoro Teachers' College mwaka 1976.

Baada ya shule, Wallah alianza kazi ya ualimu wa Kiswahili. Akiendelea kufunza katika shule mbalimbali Kenya kama vile Misiani Girls, Moi Girls Isinya, aliweza kufanya shahada ya Kiswahili na Kiarabu. Baadaye, aliendeleza uchu wake wa kukikujua Kiswahili kwa kufanya Shahada ya Uzamili katika chuo kikuu cha Dar es Salaam[3].

Vitabu[hariri | hariri chanzo]

Wallah bin Wallah ameandika vitabu vya Kiswahili Mufti vinavyotumiwa katika shule za Msingi. Pia ameandika kitabu cha Insha Mufti ambacho kinawezesha wanafunzi kuandika insha nzuri. Chemsha Bongo ni kitabu kingine ambacho Wallah alikiandika kwa madhumuni ya kutayarisha wanafunzi wanapojiandaa kuufanya mtihani wa Mwisho shuleni za msingi Kenya.

Wallah ameandika vitabu vya hadithi fupi kama vile:

  • Tumigidie Bwege
  • Zawadi ya Sanda
  • Sitaki Simu
  • Kifo cha Wema
  • Kicheko cha Maiti
  • Kitanzi cha Utandawazi
  • Mbwa wa Majini

Kukashifiwa[hariri | hariri chanzo]

Wallah bin Wallah alibatilisha ngeli za Kiswahili 'ji-ma' na kuzifanya 'li-ya'. Kwa sababu hii alikashifiwa sana na wasomi huku wakinung'una kwamba alikuwa akiharibu lugha ya Kiswahili. Licha ya hayo, Taasisi ya Elimu Kenya (Kenya Institute of Education) iliitikia mapendekezo yake ya kubatilisha ngeli hiyo kuwa ya 'li-ya'.[1]

Wallah bin Wallah amekashifiwa pia kwa kubuni maneno ya Kiswahili kwa vitu ambavyo vililetwa na Wazungu na kwa hivyo havikujulikana na Waswahili hapo nyuma. Maneno kama runinga (TV), rununu (mobile phone), tarakilishi (computer) bado hayajaitikiwa na Waswahili wasomi wengi maana wanaona kwamba ni heri kuyatohoa kwa sababu kiini chao ni Kizungu.

Mwalimu Wallah ameteteswa pia kwa kubuni mtindo mpya wa kusoma saa. Waswahili wengi huisoma saa kama isomavyo na Wazungu huku wakisema kwamba saa ni teknologia ya Mzungu. Asingekuwepo Mzungu, hamngekuwa na saa Uswahilini.[2]

Inkwell icon - Noun Project 2512.svg Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wallah bin Wallah kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

  1. [3]
  2. https://www.sde.co.ke/thenairobian/article/2000130359/pesa-mufti-i-can-make-sh70m-from-students][https://www.youtube.com/watch?v=zf6opjr5TZQ
  3. http://www.nation.co.ke/news/The-man-with-the-golden-pen/1056-1727956-95wnoo/index.html