Walatta Petros

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Picha ya Walatta Petros, iliyochorwa mnamo mwaka 1721

Walatta Petros (kwa Ge'ez: Wälättä P̣eṭros, 1592-1642) ni mtakatifu wa kike katika Kanisa la Kiorthodoksi la Ethiopia. Anakumbukwa jinsi alivyopinga kugeuzwa kwa Ethiopia upande wa Ukatoliki wa Kiroma, jinsi alivyounda jumuiya za watawa na kutekeleza miujiza.

Wasifu wake "Maisha na Mapambano ya Walatta Petros (Gädlä Wälättä Petros)" uliandikwa mwaka 1672.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Maisha ya awali[hariri | hariri chanzo]

Walatta Petros alizaliwa mnamo 1592 katika familia ya kikabaila iliyokuwa na haki juu ya ardhi kusini mwa Ethiopia. Baba yake na kaka walikuwa maofisa kwenye ikulu ya mfalme wa nchi.

Walatta aliolewa akiwa na umri mdogo na kijana aliyeitwa Malkiya Krestos, mmoja wa washauri wa Mfalme Susenyos. Alizaa watoto watatu ambao wote walikufa wakiwa wachanga na Walatta aliamua kumwacha mumewe na kuwa mtawa.[1]

Kuwa mtawa[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1621 wamisionari Wakatoliki Wareno wa Shirika la Yesu (Wajesuiti) walifaulu kumshawishi mfalme Susenyos kuachana na dhehebu lake la Waorthodoksi wa Mashariki na kuhamia Ukristo wa Kikatoliki. Katika kipindi hiki Walatta aliondoka kwake akaingia katika monasteri kwenye Ziwa Tana alipochukua kiapo cha useja akanyoa kichwa chake ili kuwa mtawa katika Kanisa la Kiorthodoksi la Ethiopia, akikataa kugeukia Ukatoliki.

Walakini, viongozi wa Kanisa na ikulu walimhimiza arudi kwa mumewe, kwa sababu huyu alikuwa akiharibu mji ule ambao alikuwa akijificha. Alirudi nyumbani, lakini aligundua kwamba mume wake aliwahi kuunga mkono uuaji wa askofu mkuu wa Kanisa la Kiorthodoksi. Hapo aliondoka tena na kuwa mtawa katika umri wa miaka 25. [1]

Upinzani wake dhidi ya Ukatoliki na Mfalme[hariri | hariri chanzo]

Mnamo 1626, mmisionari Mjesuiti alipokewa na Mfalme Susənyos kama mkuu mpya wa Kanisa la Ethiopia akaendelea kukataza mafundisho na desturi za kanisa la Kiethiopia. Mfalme alipoagiza watumishi wote wa Kanisa wale kiapo cha kumtii Papa wa Roma kufuatana na utaratibu wa Kikatoliki, maaskofu, watawa na waumini wengine wengi walikataa. Kipindi cha uasi kilifuata ambapo jeshi la mfalme lilipigana na waasi katika pande mbalimbali za nchi.

Walatta Petros alianza kuhubiri dhidi ya mabadiliko hayo. Aliwaambia waumini wasisikilize mafundisho ya wageni, alikosoa wote walioacha Uorthodoksi, pamoja na mfalme, wakubwa wake na maaskofu walioitikia madai ya mfalme. Alihubiri jina la mfalme lisitajwe tena katika liturgia ya ibada kanisani. Hapo alikataa uhalali wa ufalme wa Susenyos. Hivyo alitafutwa kama adui wa dola na mdogo wa mfalme alitumwa kumshika. Walatta alipaswa kukimbia mara kwa mara.

Hatimaye alishikwa na kupelekwa mbele ya mfalme na mkutano wa wakubwa wake. Taarifa ya wasifu wake inasimulia jinsi alivyotetea ukosoaji wake bila hofu na mume wake aliingilia kati akamwomba mfalme kumsamehe na hivyo aliokoa uhai wake. Alikabidhiwa mikononi mwa Wajesuiti waliojaribu kubadilisha msimamo wake lakini alibaki imara. Hatimaye alifukuzwa akapelekwa kama mfungwa uhamishoni mbali na makao makuu ya mfalme; lakini wafuasi Waorthodoksi walimfuata na hapo alianzisha jumuiya ya kiroho.[1]

Alipoweza kutoka uhamishoni alirudi katika eneo la Ziwa Tana akaunda jumuia nyingine za wanawake watawa.

Maisha ya baadaye[hariri | hariri chanzo]

Mnamo 1632 mfalme Susenyos aliacha majaribio yake ya kugeuza dini ya Ethiopia akawaruhusu watu wote rasmi kurudi katika Kanisa la Kiorthodoksi. Baada ya tangazo hili alijiuzulu katika ufalme akarithiwa na mwanawe Fasilides aliyetangaza tena Uorthodoksi kuwa kanisa la milki yake akiwafukuza Wajesuiti nchini.

Walatta alikuwa huru kuhubiri tena hadharani. Mwaka 1642 aligonjeka akaaga Dunia tarehe 23 Novemba 1642 akiwa na umri wa miaka 50, baada ya maisha ya utawa ya miaka 26.

Wasifu ya mtakatifu[hariri | hariri chanzo]

Walatta Petros anaheshimiwa kama mmoja wa watakatifu wa kike 21 wa Ethiopia, sita kati yao wakiwa na wasifu ya kimaandishi ya maisha yao. Kitabu cha wasifu wa Walatta Petros kiliandikwa mnamo 1672, miaka thelathini baada ya kifo chake. Mwandishi alikuwa Mmonaki aliyeitwa Galawdewos. Aliandika kwa kukusanya masimulizi mengi ya kimdomo kutoka kwa jamii ya mtakatifu, na pia kuongeza maoni yake mwenyewe. Kina sehemu tatu: wasifu, miujiza ambayo iliyotokea kwa wale walioitia jina lake baada ya kifo chake, na nyimbo mbili (Mälkəˀa Wälättä Peṭros [2] na Sälamta Wälättä Peṭros [3].

Huu ni wasifu wa kwanza wa mwanamke Mwafrika wa kusini kwa Sahara unaojulikana umetungwa na Mwafrika.

Toleo la kwanza la kuchapishwa lilichapishwa mnamo 1912, kwa msingi wa hati moja. [4] Tafsiri ya kwanza kwa lugha nyingine, Kiitalia, ilichapishwa mnamo 1970, [5] [6] Mnamo mwaka wa 2015, tafsiri ya kwanza ya Kiingereza ilichapishwa.[1] [7]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. 1.0 1.1 1.2 1.3 Galawdewos; Belcher, Wendy Laura; Kleiner, Michael (2015). The Life and Struggles of Our Mother Walatta Petros: A Seventeenth-Century African Biography of an Ethiopian Woman. Princeton: Princeton University Press. ISBN 978-0691164212. 
  2. Belcher, Wendy. The Translation of the Poem Portrait of Walatta Petros. Wendy Belcher. Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2018-03-04. Iliwekwa mnamo 2019-12-15. 
  3. Belcher, Wendy. The Translation of the Poem Hail to Walatta Petros. Wendy Belcher. Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2018-03-28. Iliwekwa mnamo 2019-12-15. 
  4. Galawdewos (1912). Conti Rossini, Carlo, mhariri. Vitae sanctorum indigenarum: Acta S. Walatta Petros. Miracula S. Zara-Buruk. I. II (kwa ut). Secrétariat du CorpusSCO. 
  5. Gälawdewos; Ricci, Lanfranco (1970). Vita Di Walatta Petros. CSCO 316; Scriptores Aethiopici 61 (kwa Italian). Leuven, Belgium: Secrétariat du Corpus Scriptorum Christianorum Orientalium. ISBN 9789042903579. 
  6. Gälawdewos (2004). Gädlä Wälättä P̣eṭros [The Life of Wälättä P̣eṭros: In the Original Gəˁəz and Translated into Amharic). Addis Ababa, Ethiopia: Ethiopian Orthodox Täwaḥədo Church Press. 
  7. Galawdewos (2018-11-27). The Life of Walatta-Petros: A Seventeenth-Century Biography of an African Woman, Concise Edition (kwa Kiingereza). Princeton, NJ: Princeton University Press. ISBN 9780691182919.