Nenda kwa yaliyomo

Wafula Chebukati

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Wafula Wanyonyi Chebukati

Wafula Wanyonyi Chebukati (Desemba 19, 1961Februari 20, 2025) alikuwa wakili wa Kenya na mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), inayosimamia uchaguzi nchini Kenya. Chebukati aliteuliwa kwa wadhifa huo kwa kipindi cha miaka sita mnamo Januari 2017 na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta. Baada ya kuteuliwa kwake, alimrithi Ahmed Issack Hassan. Alistaafu mnamo Januari 17, 2023, baada ya kukamilika kwa muda wake wa kuhudumu. Aliongoza Kenya katika chaguzi kuu mbili zilizokuwa na ushindani mkubwa na utata: Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2017 na Uchaguzi Mkuu wa 2022. [1][2][3][4][5]

Chebukati alikuwa wakili wa Kenya mwenye uzoefu wa miaka mingi. Aliendesha kampuni yake binafsi ya uwakili kwa miaka 20, na baadaye mnamo 2006 alianzisha kampuni ya uwakili ya ushirikiano yenye makao yake Nairobi, Cootow & Associates Advocates. Alijiuzulu kutoka kampuni hiyo mnamo 17 Januari 2017 kabla ya kuchukua wadhifa wa Afisa wa Serikali, kwa mujibu wa sheria, ili kuepuka mgongano wa maslahi.

Mnamo 2017, alikabiliwa na madai ya mgongano wa maslahi kwa kuhusisha kampuni yake ya uwakili katika mikataba ya IEBC, lakini suala hilo lilitupiliwa mbali na Bunge kwa kukosa ushahidi.

Chebukati pia alikuwa mwanasiasa na mwanachama wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), ambacho alikihama kabla ya kuomba nafasi ya Mwenyekiti wa IEBC. Mnamo 2007, aligombea kiti cha ubunge cha Saboti na kushika nafasi ya pili.

Maisha Binafsi na Kifo

[hariri | hariri chanzo]

Wafula Chebukati alizaliwa katika Kaunti ya Bungoma mnamo 22 Desemba 1961. Alisoma katika Shule ya St. Peters Mumias, Bokoli Secondary School, na Lenana High School.

Chebukati alikuwa na Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara (MBA) kutoka JKUAT. Alikuwa mwanachama wa Chama cha Mawakili wa Kenya (LSK), Taasisi ya Makatibu Waliohitimu (ICS), na Tume ya Kimataifa ya Sheria (ICJ).

Alimuoa Mary Wanyonyi, ambaye mnamo 2023 aliteuliwa na Rais William Ruto kuwa mwenyekiti wa Tume ya Ugawaji wa Mapato (CRA).

  1. "Chebukati's wife among first to appear for PSS interviews".
  2. Capital FM, 18 Jan 2017 President Kenyatta Appoints Chebukati To Head IEBC
  3. The Standard, 18 Jan 2017 Uhuru Kenyatta appoints Chebukati as new IEBC Chairman
  4. Citizen Digital, 29 Dec 2016 Uhuru Nominates Chebukati As IEBC Chair
  5. Nation, 30 Dec 2016 Uhuru nominates Wafula Chebukati to succeed Issack Hassan as IEBC boss