Wafiadini wa Uganda

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Karolo Lwanga katikati ya wenzake 21 wa Kanisa Katoliki katika mchoro wa Albert Wider wa mwaka 1962.
Bango likionesha picha za namna Mashahidi wa Uganda walivyoteswa na wengine walilazimishwa kutembelea migongo yao huku wakiwa wamefungwa mikono nyuma; ndiyo asili ya jina la eneo hilo Namugongo likiwa na maana ya kutembea kwa kutumia mgongo.
Muonekano wa kanisa Katoliki la Mashahidi wa Uganda huko Namugongo nchini Uganda.

Wafiadini wa Uganda ni watu wa dini mbalimbali, hasa Ukristo, hususan madhehebu ya Anglikana na Kanisa Katoliki, waliouawa katika nchi ya Uganda kutokana na dhuluma dhidi ya imani.

Wafiadini wa karne ya 19[hariri | hariri chanzo]

Watakatifu hao wanaonyeshwa katika filamu "Millions".

Wafiadini Wakatoliki[hariri | hariri chanzo]

Dirisha la kanisa la Namugongo linaloonyesha Mt. Kizito.

Kati yao wanajulikana na kuheshimiwa duniani kote kwa namna ya pekee Wakatoliki 22 waliokuwa wahudumu wa ikulu ya kabaka wa Buganda Mwanga II (1884 - 1903) ambao waliuawa kati ya tarehe 15 Novemba 1885 na tarehe 27 Januari 1887 kwa sababu ya kumwamini Yesu Kristo baada ya kuhubiriwa Injili na Wamisionari wa Afrika walioandaliwa na kardinali Charles Lavigerie.

Ndio wafiadini wa kwanza wa kusini kwa Sahara kuheshimiwa na Kanisa Katoliki kama watakatifu. Majina yao ni haya:

Katika ibada ya kuwatangaza hao (18 Oktoba 1964), Papa Paulo VI alitaja pia kwa jumla wafiadini wengine wa dhuluma hiyo waliokuwa wa madhehebu ya Anglikana.[1].

Wafiadini wa Anglikana[hariri | hariri chanzo]

Labda ni wengi zaidi Waanglikana waliouawa katika dhuluma hiyo, kuanzia Yusufu Lagamala, Mark Kakumba na Noah Seruwanga waliokatwakatwa vipandevipande na kuchomwa moto tarehe 31 Januari 1885.

Waliofuata ni askofu James Hannington na wenzake waliouawa tarehe 29 Oktoba 1885 kabla hawajaingia Buganda.

Mwaka 1886, kati ya tarehe 25 Mei na 3 Juni, waliuawa: Moses Mukasa (kwa mkuki), Muddwaguma na Elias Mbwa (kwa kuhasiwa), David Muwanga (tarehe na aina ya kifo chake haijulikani), Omuwanga, Kayizzi Kibuka, Mayanja Kitogo (aina ya kifo chao haijulikani), Alexander Kadako na Frederiko Kidza (kwa kupigwa), Noah Walikaga , Daniel Nakabandwa, Kiwanuka Gizayo, Mukasa Lwa Kisiga, Lwanga, Mubi, Wasswa, Kwabafu, Kifamunyanja, Muwanga Njigija (wote kwa kuchomwa moto), Robert Munyagabyanjo (kwa kukatwakatwa vipandevipande na kuchomwa moto).

Mfiadini wa Uislamu[hariri | hariri chanzo]

Katika dhuluma hiyohiyo aliuawa pia Mwislamu mmoja.

Wafiadini wa karne ya 20[hariri | hariri chanzo]

Wafiadini Wakatoliki[hariri | hariri chanzo]

Mwanzoni mwa karne ya 20 vijana wawili tena wa Kanisa Katoliki walimfia Yesu (1918) wakatangazwa wenye heri na Papa Yohane Paulo II mwaka 2002: Daudi Okelo na Jildo Irwa.

Mfiadini wa Anglikana[hariri | hariri chanzo]

Askofu Luwum wa Kanisa la Anglikana la Uganda aliyeuawa na Idi Amin.

Mwaka 1977 Idi Amin alimuua askofu mwingine wa Anglikana, Janani Luwum.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. "Et mentione digni sunt alii etiam, qui, anglicana instituta religiosa profitentes, pro Christi nomine morte affecti sunt." ("And the others are worthy of mention also, who, professing the Anglican religious customs, were afflicted with death for the name of Christ.") Vatican Archive

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • J. FRANSE, W.F., Mashahidi 22 wa Uganda – tafsiri ya C. Kuhenga n.k. – ed. T.M.P. Book Department – Tabora 1981

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wafiadini wa Uganda kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.