Nenda kwa yaliyomo

Vitabu vya Wafalme

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Vitabu vya Wafalme ni kati ya vitabu vya historia vya Tanakh (Biblia ya Kiebrania), vinavyopatikana pia katika Agano la Kale (sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo). Viko viwili navyo vinafuata kinaganaga habari za wafalme wote wa Israeli waliotawala baada ya mfalme Daudi hadi mwisho wa ufalme wa Yuda.

Vitabu hivyo viwili hapo mwanzo vilikuwa kitabu kimoja, navyo vinaendelea na historia ya Israeli tangu mwisho wa Vitabu vya Samweli. Muda wote unaoelezwa katika vitabu hivi ni kama miaka 400 hivi, kuanzia miaka ya mwisho ya utawala wa Daudi mpaka watu walipopelekwa katika kifungo cha Babeli. Hivyo vinaeleza mgawanyiko wa ufalme katika sehemu mbili, historia yake na jinsi falme hizo mbili zilivyorudi nyuma na kwenda mbali na mapenzi ya Mungu.

Vitabu hivyo viwili vinapitia historia ya Israeli kuanzia mwaka 972 hadi 560 hivi K.K. vikionyesha mwenendo wa kila mfalme upande wa dini, hasa katika kutekeleza maneno ya Kumbukumbu la Torati, ya kwamba Mungu ni mmoja, hivyo hekalu lake liwe moja tu. Kwa kuwa wafalme wote wa kaskazini na karibu wale wote wa kusini walikwenda kinyume, vitabu hivyo vinaanza na ufalme imara na wa fahari ulioweza kumjengea Mungu hekalu la ajabu, kumbe vinaishia na hali mbaya na ya aibu kuliko ilivyokuwa kabla ya Musa, wafalme wakiwa wafungwa Babeli, Waisraeli wote uhamishoni na hekalu lenyewe magofu tu.

Lakini waandishi hawakusimulia hayo ili kutunza kumbukumbu za zamani kama wanavyofanya wanahistoria, bali kwa lengo la kuonyesha tena uaminifu wa Mungu, aliyezidi kutuma manabii wake hata baada ya kuona hawasikilizwi, bali wanadhulumiwa hata kuuawa. Kwa kutegemea uaminifu huo, Wayahudi waliohamishiwa Babeli waliweza kutumaini mwanzo mpya. Hasa manabii wa mwisho wa wakati huo, Yeremia na Ezekieli, waliwatia moyo kuwa Mungu atabadili mioyo yao na kufanya nao Agano Jipya.

Mtindo wa uandishi[hariri | hariri chanzo]

Kama ilivyokuwa katika vitabu vya Yoshua, Waamuzi na Samweli, vitabu viwili vya Wafalme viliandikwa kama historia ya unabii. Maana yake ni kwamba, madhumuni ya mwandishi si kusimulia matukio ya historia tu, bali alitaka kuonyesha maana ya matukio hayo katika mpango wa Mungu. (Kwa maelezo zaidi kuhusu maandiko ya historia ya unabii, tazama maelezo katika Kitabu cha Yoshua).

Kwa sababu ya makusudi hayo, mwandishi hakusimulia matukio yote ya wakati fulani wala hakuorodhesha mambo yote kwa mfululizo maalumu wa wakati. Yeye alichagua na kupanga habari kadiri ya maana yake ya kidini kuliko ile ya kisiasa. Inawezekana kwamba mfalme aliyekuwa na mambo mengi makubwa ya siasa ametajwa kwa maneno machache tu (k.mf. Omri: 1 Fa 16:21-28), ambapo mambo yasiyokuwa ya maana kubwa ya siasa aliyaeleza kwa kirefu (k.mf.huduma za Eliya na Elisha). Alitaja mambo ya nchi za jirani tu kama yalikuwa na maana kwa mpango wa Mungu kwa ajili ya Israeli.

Mtunzi na wakati[hariri | hariri chanzo]

Mwandishi wa vitabu vya Wafalme hakutajwa kwa jina. Inawezekana kwamba alikuwa nabii aliyepata nafasi ya kusoma masimulizi rasmi ya historia ya kifalme pamoja na masimulizi ya manabii (1 Fa 11:41; 15:7, 23, 31; taz. 2 Nya 9:29; 33:19). Sehemu kubwa za vitabu vya manabii Isaya na Yeremia pia zinaonekana katika vitabu vya Wafalme (Isa 36:1-39:8; Yer 39:1-10; 52:1-34).

Inawezekana kwamba kazi ile yote ilimalizika baada ya kuanguka kwa taifa la Israeli, watu walipokuwa kwenye uhamisho wa Babeli.

Mwisho wa mfalme Daudi (971 hivi K.K.)[hariri | hariri chanzo]

Habari za mwisho za Daudi zinapatikana katika 1Fal 1-2 tunaposikia juu ya njama ya mtoto wake mwingine: Adonia alitaka kutawala akajifanya mfalme huku Daudi mkongwe hana habari. Lakini nabii Nathani akaingilia kati ili mwandamizi awe Solomoni, ambaye alipozaliwa na Betsabea, mke wa Uria alimhakikishia Daudi msamaha wa Mungu.

Mfalme Solomoni (971-931 hivi K.K.)[hariri | hariri chanzo]

Ufalme wake uliweza kustawi kuliko ule wa baba yake kutokana na msingi imara aliouweka Daudi.

Lakini mwenyewe aliudhoofisha na kusababisha mara baada ya kifo chake utokee utengano kati ya makabila ya Kaskazini na yale ya Kusini.

Kati ya kazi muhimu alizozifanya, mojawapo ni kujenga hekalu la Yelusalemu na kuliweka wakfu kwa sherehe kubwa ya siku saba, ambapo Mungu alionyesha kibali chake kwa kulijaza kwa sura ya wingu (1Fal 8). Polepole hekalu hilo likaja kuwa la pekee hata patakatifu pengine pote pakakatazwa chini ya mfalme Yosia.

Ingawa Solomoni anasifiwa kwa hekima yake, alishindwa kukwepa majivuno na tamaa, akataka kuwapendeza wake zake waliokuwa 700 (mbali na masuria 300), wengi wao Wapagani, hata akawajengea mahali pa kuabudia miungu yao akamchukiza Mungu hata akatabiriwa mtoto wake atanyang’anywa sehemu kubwa ya ufalme (1Fal 11:1-13) ikawa hivyo.

Wafalme wa Israeli na Yuda (931-587 K.K.)[hariri | hariri chanzo]

Baada ya Solomoni, huko Israeli (Kaskazini) walitawala watu wa koo mbalimbali (931-722), wote wabaya. Hatimaye watu karibu wote walipelekwa uhamishoni Ashuru (722). Hakuna aliyerudi.

Kumbe huko Yuda (Kusini) waliendelea kutawala watu wa ukoo wa Daudi tu (931-587). Kati yao kuna wafalme wema 2 (Ezekia na Yosia); wengine wema kiasi; wengine wabaya. Hatimaye watu wao pia walipelekwa uhamishoni Babeli (587) lakini baadhi wakarudi (kuanzia 538).

Manabii[hariri | hariri chanzo]

Tofauti na mtangulizi wake, Daudi alimpendeza Mungu, si kwa sababu hakufanya makosa, bali kwa sababu alikuwa tayari kumsikiliza akisema kwa njia ya manabii wake Nathani, Gadi n.k. Alikubali kukosolewa, kuonywa na kuambiwa la kufanya. Kila mfalme baada yake alitakiwa kufanya hivyo.

Kwa kiasi kikubwa, miaka ya wafalme wa Israeli na Yuda ni pia miaka ya manabii bora walioinuliwa na Mungu alivyotaka ili kuwakemea au kuwafariji Waisraeli.

Kazi yao kubwa haikuwa kutabiri yatakayotokea, bali kuwa madaraja kati ya Mungu na watu wake, wakiwafahamisha yeye anawaza na kutaka nini.

“Nabii” ni hasa mtu “anayesema kwa niaba” ya Mungu. Si lazima aandike kitu.

Njia zake za kuwasiliana na Mungu zinafanana na zile za dini nyingine: kuota, kupata njozi, kutoka nje ya nafsi na hata kutazamia kwa kutumia vifaa maalumu vya kubashiria. Lakini polepole hivyo vya mwisho vikaja kulaumiwa, kumbe Neno lenyewe likaja kushika nafasi ya kwanza kuliko dalili za ajabu zinazoweza zikapatikana hata katika vichaa.

Kwa kuwa Roho ni wa Bwana tu, akijalia unabii ni kama karama ipitayo: hivyo mtu yuleyule anaweza akasema mara ukweli mara uongo. Vilevile karama hiyo haithibitishi usahihi wa imani na uadilifu wa mhusika. Hatimaye baadhi yao wakaanza kuitwa “manabii wa uongo”, kwa sababu ya kutabiri uongo kwa niaba ya Mungu (kwa makusudi mazima au kwa kujidanganya) na zaidi kwa sababu ya kupotosha imani na maadili ya taifa lake.

Manabii Eliya na Elisha (865-790 hivi K.K.)[hariri | hariri chanzo]

Waisraeli walielekea dini za kandokando kwa sababu zilikuwa zinaahidi kufanikisha maombi yao kwa ibada za hakika, wakati Mungu ana hiari ya kupokea au kukataa sadaka zao. Waisraeli walijaribu kufuata pande zote mbili kwa pamoja, ila Mungu hakuweza kukubali, kwa kuwa ni peke yake tu. Imani yao iliyumba hasa wakati mfalme Ahabu alipotawala Kaskazini (869-850 hivi K.K.), ambapo Yezebeli, mke wake, alifanya juhudi kubwa za kuikomesha kabisa imani yao kwa YHWH ili wamuabudu Baali, mungu mkuu wa kwao aliyehusika na mvua, kufuatana na sanamu mbili zilizotengenezwa na Yeroboamu I zikiwa na sura ileile ya Baali ([[fahali wa dhahabu]). Mezani pa malkia huyo walikuwa wanalishwa manabii wa uongo 850, kumbe manabii wa Bwana waliuawa karibu wote.

Hapo Mungu akamtuma Eliya (1Fal 17-18) ambaye jina lake lina maana ya kwamba, “Mungu wangu ni YHWH” na linajumlisha kazi yake ya kutetea kwa ari zote imani ya kweli hata akaiokoa. Ili kuondoa utata wa kuabudu pande mbili, Eliya kwanza alizuia mvua isinyeshe nchini miaka mitatu na nusu, ibada kwa Baali zisifanikiwe hata kidogo, halafu akashindana na manabii hao hadhara ya Israeli yote juu ya mlima Karmeli. Tofauti na mbinu za manabii 450 wa Baali, waliofikia kujichanja na kutoka damu ili kuvuta moto kutoka mbinguni wasifaulu, Eliya aliomba tu kwa unyofu kwamba Mungu ajitokeze ili kugeuza mioyo ya watu wake wamrudie. Kwa kuteremsha moto juu ya sadaka yake, Bwana alithibitisha kuwa ndiye Mungu pekee na kuwa anaendelea kuwaokoa watu wake. Baada ya Eliya kuwachinja wote aliruhusu mvua inyeshe tena. Ndiyo sababu anasifika kwa nguvu ya sala yake (Yak 5:17-18).

Hasa ni kwamba, baada ya kukimbia hasira ya Yezebeli aliyemuapia atamuua kabla ya kesho yake, akisali pangoni juu ya mlima Sinai kama Musa mwanzoni mwa agano la Israeli na Bwana, alijaliwa kutokewa na kuagizwa upya na Mungu katika sauti ndogo ya upepo mtulivu akamilishe kazi yake hasa kwa kuwafanya Elisha nabii na Yehu mfalme (1Fal 19:1-18). Hata katika Yesu kugeuka sura mlimani akatokea pamoja na Musa ili wamshuhudie kama wawakilishi wa Torati na Manabii (Mk 9:2-13).

Kwa jinsi alivyofanya kazi kwa ari, na kwa kupalizwa juu ya gari la moto (2Fal 2:1-18) akalinganishwa na moto (YbS 48:1-11) akatabiriwa atarudi kabla ya siku ya Bwana (Mal 3:23-24). Ndiyo sababu Injili zinamtaja mara nyingi.

Kwa miaka zaidi ya 50 kazi yake iliendelezwa na Elisha, ambaye anasifika pia kwa miujiza yake (YbS 48:12-16) na pamoja na mwalimu wake amechukuliwa na Yesu kama mfano wa unabii wake utakaowaokoa mataifa baada ya Israeli kumkataa (Lk 4:24-27). Elisha alijihusisha sana na siasa akaombwa shauri na wafalme mbalimbali hata wa nchi za nje. Kwa kumpaka mafuta Yehu alianzisha mapinduzi dhidi ya ukoo wa Ahabu na kukomesha upotoshaji wake wa imani. Mapinduzi hayo yakaenea kusini kwa kumuua Atalia, binti wa Yezebeli, aliyetawala miaka saba kisha kuua watu wote wa ukoo wa Daudi (mtoto Yoashi tu alinusurika).

Muhtasari wa kitabu cha kwanza[hariri | hariri chanzo]

1:1-4:34 Sulemani aimarisha ufalme wake

5:1-9:25 Majengo ya Sulemani

9:26-11:43 Mambo mengine katika utawala wa Sulemani

12:1-16:28 Siku za kwanza katika ufalme uliogawanyika

16:29-22:53 Huduma ya Eliya

Muhtasari wa kitabu cha pili[hariri | hariri chanzo]

1:1-8:15 Huduma ya Elisha

8:16-12:21 Kuondolewa kwa Ubaali wa Yezebeli

13:1-17:41 Historia ya kuangyuka kwa Israeli

18:1-25:30 Historia ya kuangyuka kwa Yuda

Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.