Vita vya Iraki na Irani

Mstari mwekundu: Mwisho wa kusogea mbele kwa muda upande wa Iraki
Mstari njano: Mwisho wa kusogea mbele kwa muda upande wa Uajemi.
Vita vya Iraki na Irani vilitokea kuanzia Septemba 1980 hadi Agosti 1988. Vilipigwa kati ya majeshi ya nchi jirani za Iraki na Irani vikisababisha vifo vya watu milioni moja na kuisha bila mshindi. Viliitwa pia "Vita Vya ghuba" kutokana na ghuba ya Uajemi ambayo nchi zote mbili zinapakana nayo; baadaye viliitwa pia "vita vya kwanza vya ghuba" kutokana na vita vya Marekani dhidi ya Iraki vilivyofuata.
Vita vilianza kwa mashambulio ya Iraki dhidi ya Irani. Dikteta Saddam Hussein wa Iraki alitaka kutumia nafasi ya kudhoofishwa kwa jeshi la Irani baada ya mapinduzi ya Kiislamu ya Irani ya mwaka 1979. Mwaka ule serikali ya shah wa Irani ilipinduliwa na harakati iliyoongozwa na ayatollah Mwislamu Ruhollah Khomeini na maafisa wengi wa jeshi la shah ama waliuawa ama walikimbia nchi. Saddam Hussein alilenga kushika utawala juu ya Shat al Arab ambayo ni mdomo wa mito Frati na Hidekeli kwenye ghuba ambako mizigo ya mafuta ya petroli ya Iraki inapaswa kupitia ikiuzwa nje. Alilenga pia kutwaa sehemu za Irani zilizokuwa na wasemaji wa lugha ya Kiarabu na sehemu hizo zinaitwa Khuzistan; Saddam alidai ya kwamba ilikuwa eneo la kihistoria ya Iraki iliyotekwa na Uajemi.
Mwanzoni Wairaki walifaulu kuteka maeneo karibu na mpakani upande wa Irani lakini serikali mpya ya Kiislamu iliweza kutuma wanamgambo hasa vijana wengi ambao walikuwa tayari kufa hata kama hawakufundishwa kazi ya askari. Mtindo huo ulirudisha Wairaki nyuma lakini ulikuwa pia sababu ya kwamba Wairani wengi walikufa kuliko Wairaki. Ila tu Irani ni nchi yenye watu wengi zaidi na wengi wao walikuwa tayari kwa kifo kwa sababu waliona ya kwamba nchi yao ilishambuliwa. Viongozi wa kidini walitangaza ya kwamba ulikuwa wajibu wa kidini kushika silaha.
Nchi za nje kama Marekani zilihofia mapinduzi ya Kiislamu zikasaidia Iraki kwa silaha na habari kama picha kutoka vyombo vya angani. Vita hivyo vilikuwa maarufu kwa sababu Iraki ilitumia silaha marufuku kama gesi ya sumu.
Vita viliendelea ingawa Umoja wa Mataifa ulisihi pande zote mbili kumaliza mauaji. Mwishowe walipatana kusimamisha mapigano na kurudi kwenye mipaka ya kimataifa kwa sababu ya uchovu na uharibifu mkubwa pande zote mbili.
Picha
[hariri | hariri chanzo]-
Wanajeshi wa Uajemi wakivaa kinga dhidi ya silaha za sumu
-
Makaburi ya wafu wa vita mjini Yazd (Uajemi)
-
Wanajeshi wa Iraki wakijisalimisha mjini Khoramshahr
-
Vita kati ya Irak na Uajemi vilivyoanza tarehe22 Septemba 1980 - Tehran
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]![]() |
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Vita vya Iraki na Irani kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |