Funguvisiwa la Komori
Funguvisiwa la Komori (kwa Kifaransa: Comores) ni funguvisiwa katika Bahari Hindi upande wa Mashariki wa Afrika. Iko katika Mlangobahari wa Msumbiji kaskazini kwa Madagaska na mashariki kwa Msumbiji. Jina limetokana na lugha ya Kiarabu ambapo Juzur al-Qamar (جزر القمر) linamaanisha "visiwa vya mwezi".
Jiografia
[hariri | hariri chanzo]Komori ina visiwa vinne vikubwa: Ngazija, Anzwani, na Mwali, vinavyounda Umoja wa Komori, na Mayote ambayo kisiasa ni sehemu ya Ufaransa kwa sababu wakati wa kupata uhuru watu wake walitamka kwa kura nyingi (73%) ya kwamba wanataka kubaki na Ufaransa. Lakini Umoja wa Komori unadai ni sehemu ya eneo lake. Ina pia visiwa mbalimbali vidogo.
Hali ya hewa ni ya kitropiki. Kuna mvua miezi yote.
Kitovu cha kisiwa kikubwa zaidi (Grande Comore) ni mlima wa volkano hai Karthala wenye mita 2,461 juu ya UB. Safari iliyopita Karthala ililipuka mwaka 1977 ikaharibu kijiji kimoja.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Visiwa vya Komori vimekaliwa na watu mbalimbali kutoka Afrika na Asia Kusini katika historia ndefu. Wanaakiolojia walitambua mabaki ya makazi ya watu kutoka karne ya 6 kwenye kisiwa cha Anzwani lakini haijulikani kama watu walitangulia kufika mapema bila kuacha mabaki ya kutambulika.
Waswahili wa kwanza walifika kama sehemu ya uenezi wa Wabantu tangu karne ya 9 BK.
Kipindi cha kwanza huitwa kipindi cha Dembeni (karne ya 9 - 10) ambako Waswahili walianzisha kijiji kimoja katika kila kisiwa.
Wakati wa karne ya 11 hadi ya 15 biashara iliongezeka na Madagaska pia na wafanyabiashara kutoka Uarabuni. Vijiji vidogo vikaongezeka na vijiji vya awali vikakua vikawa miji.
Kumbukumbu ya wenyeji hutaja mara nyingi majina ya Waarabu kutoka Yemen na Saba' kama mababu wa koo asilia lakini hakuna uhakika kama kumbukumbu hizo zinalingana na historia halisi.
Athira ya Kiarabu na ya Kiislamu ikaongezeka kutokana na biashara ya watumwa, dhahabu na pembe za ndovu kati ya Afrika ya Mashariki na nchi za Kiislamu.
Waarabu na Waajemi walijenga vituo kwa ajili ya biashara yao pamoja na misikiti na kueneza dini ya Uislamu kwenye visiwa.
Hata kama Komori si karibu sana na pwani, hata hivyo kutokana na mwendo wa upepo ni kituo muhimu cha jahazi kwenye safari kati ya Kilwa na Msumbiji iliyokuwa bandari kuu ya dhahabu ya Zimbabwe.
Kufuatana na katiba ya uhuru ya mwaka 1975 Umoja wa Komori ulitangazwa kuwa jamhuri ya Kiislamu. Serikali zilipinduliwa mara kwa mara na wanajeshi au na mamluki.
Katiba mpya ya mwaka 2001 imeondoa tabia ya kidini ya dola na iliunda utaratibu wa urais kuzunguka kati ya visiwa vitatu vikubwa. Katika muundo huo rais wa jamhuri atateuliwa kila baada ya miaka minne kutoka kisiwa tofauti.
Watu
[hariri | hariri chanzo]Watu wa Komori ni mchanganyiko wa Waarabu, Wamadagaska, Waafrika wa bara ambao mababu walikuwa watumwa, Wahindi na Wazungu kadhaa.
Wakazi wengi ni Waislamu (98%, hasa Wasuni), wakifuatwa na Wakristo (2%). Karibu nusu ya wananchi wote hawajui kusoma.
Nje ya Kifaransa, Kiarabu na Kimalagasy Sanifu, kuna lugha nne za asili ambazo huzungumzwa na Wakomori, yaani Kimwali, Kianzwani, Kingazija na Kimaore ambazo ziko karibu na Kiswahili.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]| Nchi za Afrika | |
|---|---|
| Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe | |
| Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika | |
| Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira | |
| Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Funguvisiwa la Komori kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |