Nenda kwa yaliyomo

Vincent van Gogh

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Van Gogh alivyojichora mwenyewe

Vincent Willem van Gogh (30 Machi 1853 - 29 Julai 1890) alikuwa mchoraji kutoka Uholanzi.

Huhesabiwa kati ya waanzilishaji wa uchoraji wa kisasa. Aliacha picha 864 na vichoro zaidi ya elfu moja na zote alichora katika miaka 10 ya mwisho wa maisha yake.

Van Gogh alizaliwa mjini Zundert (Uholanzi) kama mtoto wa mchungaji wa kanisa la Reformed. Baada ya shule alianza kazi katika duka la sanaa la mjomba wake. Kazi hii ilimpeleka pia London na Paris. 1876 aliacha ajira hii akaendelea kujaribu kazi mbalimbali. Alifundisha katika shule, alikuwa msaidizi wa mchungaji wa kanisa, aliuza vitabu. Wazazi walimshauri kusoma theolojia lakini aliacha masomo haya tena. Badala yake alitaka kuwa mhubiri akaajiriwa kama mmisionari kati ya wafanyakazi maskini katika migodo ya makaa ya Ubelgiji. Wakati huu alikuwa ameshaanza kuchora watu na mazingira alimoishi. Alisaidia wagonjwa na kufundisha Biblia akijitahidi kuishi sawa na maskini wa mazingira yake. Mtindo huu ulipingwa na wakubwa wake, akarudi kwa wazazi kwa muda mfupi halafu akaamua kuishi kama msanii.

Tangu 1880 van Gogh alikuwa msanii akafuata kozi ya uchoraji na kufundishwa na mjomba wake aliyekuwa mchoraji. 1886 alihamia Paris alipokaa kwa mdogo wake Theo van Gogh aliyekuwa mfanyabiashara wa sanaa. 1888 alihamia Ufaransa kusini alipokaa hadi mauti yake. Aliishi pamoja na mchoraji Mfaransa Paul Gauguin.

Pamoja na kuchora picha nyingi alipatwa na matatizo ya kiafya hasa ya kiakili na ya kiroho. Alitibiwa lakini 27 Julai 1890 alijipigia risasi akafa siku mbili baadaye.

Wakati wa maisha yake hakufaulu wala hakutambuliwa isipokuwa na watu wachache. Aliishi katika hali ya umaskini akipata misaada ya fedha kutoka kwa Theo, mdogo wake.

Katika karne ya 20 picha za van Gogh zilikuwa maarufu zikauzwa kwa pesa mamilioni ya dollar.

Picha[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

[1]