Nenda kwa yaliyomo

Umeme wa upepo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Uwezo wa miradi ya umeme wa upepo iliyoanzishwa duniani kati ya 1996 na 2008
Mradi wa Umeme wa Upepo Fenton Wind Farm katika Minnesota (Marekani).

Umeme wa upepo ni umeme unaopatikana kwa njia ya mitambo inayotumia nguvu ya upepo na kuibadilisha kuwa umeme. [1]

Jinsi ya kutumia nguvu ya upepo

[hariri | hariri chanzo]

Nguvu ya upepo kiasili ni nishati inayopatikana ndani ya upepo ambayo mwendo wa masi za hewa katika angahewa ya dunia. Mwendo huu unaendeshwa na joto la jua na tofauti zilizopo katika halijoto kwenye sehemu mbalimbali ya dunia.

Nguvu hii ya upepo ilitumiwa kwa manufaa ya kibinadamu tangu miaka mingi sana, hasa kwa njia ya usafiri kwenye maji kwa kutumia tanga za kusukuma jahazi na pia kwa kuendesha vinu vya upepo vya kusagia nafaka.

Tangu mwisho wa karne ya 20 nguvu ya upepo inatumiwa zaidi na zaidi kwa kuzalisha umeme wa upepo. Hapo mwendo wa hewa unatumiwa kuzungusha tabo (rafadha - en:turbine). Mitambo hii ya kisasa inafanana kiasi na kinu cha upepo cha karne zilizopita ila tu mzunguko wa mikono yake hauzungushi mashine ya kusagia bali rafadha inayotengeneza umeme.

Umeme wa upepo kama nishati mbadala dhidi ya kupanda kwa halijoto duniani

[hariri | hariri chanzo]

Wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa gesijoto duniani na madhara ya kupanda kwa halijoto duniani zilileta mikataba ya kimataifa kama Kongamano la Mfumo wa UM kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Mapatano ya Paris kuhusu Tabianchi na hapo matumizi ya nguvu ya umeme yamepata maendeleo makubwa sana. Umeme wa upepo unaongezeka kuwa muhimu kama nishati mbadala ya kupunguza matumizi ya fueli kisukuu.

Mwisho wa mwaka 2009 takriban asilimia 1.3 ya mahitaji ya umeme duniani yalipatikana kwa umeme wa upepo.[2] Lakini nchi kadhaa zilizotangulia kuendesha teknolojia hii zinapata kiasi kikubwa zaidi. Nchi inayopata kiwango kikubwa cha mahitaji yake ya umeme ni Denmark yenye asilimia 20 za umeme wa upepo. [3][4] Katika Hispania ni 11% na 9% katika Eire. [5]

Mnamo mwaka 2015 nchi ya Denmark ilizalisha asilimia 40% ya umeme wake kwa njia ya umeme wa upepo[6]. Angalau nchi 83 duniani zinaingiza umeme kutokana na matumizi ya nguvu ya upepo katika mitandao ya umeme ya kitaifa.[7] Mnamo mwaka 2014 umeme wa upepo ulifikia tayari asilimia 4 za umeme wote uliotumiwa duniani. Katika Umoja wa Ulaya kiasi hiki kilifijia tayari asilimia 11.4 [8]

Katika Afrika ni hasa Afrika Kusini iliyoanza kutumia chanzo hiki cha nishati. Nchini Kenya Mradi wa umeme wa upepo wa Ziwa Turkana ulianzishwa mwaka 2010 ukilenga kutoa megawati 300 baada ya kukamilika.[9]

Maswali kuhusu matumizi ya nguvu ya upepo

[hariri | hariri chanzo]
Roscoe Wind Farm in West Texas

Matumizi ya nguvu ya upepo yanapambana na matatizo kadhaa ambayo ni mabadiliko ya upepo halafu maoni kati ya wananchi wa sehemu ambako vituo vinajengwa.

Upepo ni mwendo wa hewa ambao uthabiti wake hubadilikabadilika. Umeme wa upepo hivyo unazalishwa kwa wingi wakati kuna upepo una mwendo mzuri. Wakati wa dhoruba mara nyingi rafadha zinasimamishwa. Wakati wa ukimya wa upepo rafadha hazizunguki na katika hali zote mbili hakuna umeme unaozalishwa. Kama mwendo wa upepo ni mdogo hata uzalishaji ni duni.

Kwa hiyo hata kama uwezo wa upepo wa kuzalisha umeme ni mkubwa si rahisi kufikia uzalishaji thabiti na hii inahitaji vyanzo vingine vya umeme vinavyoweza kuongeza uzalisaji wakati upepo ni hafifu. Hapo ni hasa vituo vya umeme vinavyoendeshea kwa gesi ambavyo vinaweza kuwaka haraka vikishirikiana na vituo vya umeme wa upepo.

Kwa jumla mabadiliko haya yanaweza kusawazishwa kama mtandao wa umeme wa nchi una uwezo wa kusafirisha viwango vikubwa vya umeme kati ya pande zote za eneo kubwa kwa sababu hapa tofauti za upepo dhaifu na wenye nguvu zinaweza kusaidiana kufikia wastani wa kawaida. Lakini hadi sasa mitandao ya nchi nyingi kubwa bado hazitoshi kwa mahitaji haya.

Katika nchi kadhaa kulikuwa na upinzani wa wananchi dhidi ya ujenzi wa vituo vinavyoweza kuwa na minara mamia ya rafadha za upepo kwa sababu zinabadilisha sana uso wa eneo ambao watu waazoea.

  1. "Wind power in the UK". BBC News. 2007-12-18. Iliwekwa mnamo 2010-03-10.
  2. World Wind Energy Association (2008). Wind turbines generate more than 1 % of the global electricity Archived 22 Novemba 2009 at the Wayback Machine.
  3. Global wind energy markets continue to boom – 2006 another record year Archived 7 Aprili 2011 at the Wayback Machine. (PDF).
  4. Global Wind Energy Council (2009). Global Wind 2008 Report Archived 7 Aprili 2011 at the Wayback Machine., p. 9, accessed on 4 Januari 2010.
  5. International Energy Agency (2009). IEA Wind Energy: Annual Report 2008 Archived 29 Septemba 2011 at the Wayback Machine. p. 9.
  6. Denmark breaks its own world record in wind energy, tovuti ya Euractiv.com (15 Januari 2016). Iliangaliwa juni 2017.
  7. "Renewables 2011: Global Status Report" Archived 19 Juni 2013 at the Wayback Machine. tovuti ya Germanwatch.org(PDF). uk. 11
  8. Wind in power 2015 European statistics February 2016, tovuti ya EWEA EUROPEAN WIND ENERGY ASSOCIATION
  9. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2012-01-29. Iliwekwa mnamo 2011-04-18.

Viungo vya njə

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Umeme wa upepo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.