Uasi wa kijeshi wa 1982 nchini Kenya

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Wanajeshi wa Kenya na Marekani,mwaka 2006

Uasi wa kijeshi wa 1982 nchini Kenya ulikuwa jaribio lililoshindikana la kumpindua rais Daniel arap Moi.

Matukio[hariri | hariri chanzo]

Tarehe 1 Agosti 1982, siku ya Jumapili, kundi la wanajeshi wa anga walivamia kituo cha Redio ya Sauti ya Kenya wakidai kuwa wamepindua serikali. Kiongozi wao alikuwa Hezekiah Ochuka ambaye alikuwa afisa wa ngazi ya chini ya jeshi akishirikiana na wenzake. Tangazo lao lilisema, "Serikali ya Kenya imepinduliwa na majeshi na sasa iko mikononi mwa majeshi. Viongozi wetu wamekuwa watu wafisadi wenye matumbo makubwa wasiojali maskini."

Tangazo lilitolewa na kikundi cha wanajeshi waasi lilisababisha watu wengi kuandamana mjini na kupora mali ya maduka wakilenga hasa raia wa asili ya Uhindi mjini Nairobi. Inakadiriwa ya kwamba zaidi ya maduka 1,000 yaliporwa na nyumba za Wahindi zilivunjwa pamoja na wanawake wao kunajisiwa. Inasemekana kwamba, sababu za kuporwa kwa maduka ya Wahindi ilikuwa kutokuwepo kwa usawa wa kimaisha kati ya Wakenya na Wahindi mjini Nairobi.

Jeshi la ardhi na polisi walipambana na uasi[hariri | hariri chanzo]

Jaribio la mapinduzi halikudumu kwa muda mrefu baada ya jeshi la ardhi pamoja na polisi kuingilia kati na kupambana na uasi kwa baada ya saa sita tu. Rais Moi alikuwa nje ya Nairobi na mipango ya kurusha mabomu kwa nyumba yake huko Kabarnak haikutekelezwa.

Hezekiah Ochuka alipanda ndege akakimbilia Tanzania alipokamatwa na kurudishwa Kenya baadaye alipopelekwa mahakamani na kuhukumiwa kunyongwa kama msaliti.

Sababu za uasi[hariri | hariri chanzo]

Idadi kubwa ya viongozi wa uasi walikuwa wanajeshi kutoka kabila la Waluo. Inasemekana kwamba jaribio la mapinduzi lilisababishwa na azimio la Bunge la Kenya la tarehe 9 Juni 1982 lililofanya Kenya kuwa nchi ya chama kimoja. Sheria hiyo ilizuia jaribio la kiongozi wa Kiluo Jaramogi Oginga Odinga kuanzisha chama cha upinzani.

Nini kilifuata baada ya kushindwa kwa jaribio la Mapinduzi?[hariri | hariri chanzo]

Uasi ulisababisha ukandamizi mkubwa sana. Polisi walipita katika nyumba za askari wa anga pia katika mitaa ya vibanda ambako maelfu ya wakazi walikamatwa. Pia jeshi la anga lilifutwa kufuatia tuhuma za kushindwa kutekeleza vema majukumu yake. Jumla ya watu 145 waliuawa ama na waasi au baadaye katika ukandamizi wake.

Viongozi wa Waluo walikamatwa pia; Jaramogi Odinga alifungwa katika nyumba yake na kushtakiwa: baadaye mashtaka yaliondolewa lakini mwanae Raila Odinga alifungwa jela kwa miaka sita bila kuhukumiwa.

Kwa jumla siasa ya rais Moi ilibadilika kuwa ya kidikteta baadaye na polisi ilipewa mamlaka pana kutafuta wapinzani kata kuwatesa na kuwakamata bila kuwapeleka mahakamani.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]