Uandishi wa habari

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Uandishi wa habari (kwa Kiingereza journalism) ni kazi ya kukusanya, kupanga na kusambaza habari kwa wasomaji, wasikilizaji na watazamaji katika jamii.

Usambazaji hutokea kupitia vyombo vya habari na media mbalimbali kama vile gazeti, redio, televisheni na intaneti.

Katika jamii ya kisasa media ni njia kuu ya kushirikisha watu wengi na mambo yote yanayoathiri umma, jamii, siasa, uchumi na utamaduni wake.

Penye mfumo wa kisiasa ya demokrasia upatikanaji wa habari huru, nyingi na tofauti ni muhimu sana kwa uwiano sawa kati ya washiriki katika siasa, uchumi na utamaduni.

Kutokana na nafasi hii muhimu uandishi wa habari na media vinaitwa pia mhimili wa nne kati ya madaraka ya umma.

Hapo maadili ya wanahabari ni muhimu wakifuata kanuni za kukusanya na kusambaza habari zinazoweza kuchunguliwa na kupimwa kulingana na hali halisi na kusahihishwa kama makosa yalitokea.

Kuja kwa intaneti kumeleta kipindi kipya cha uandishi na usambazaji wa habari ambako raia wana nafasi ya kutangaza habari na rai kwa watu wengi. Hapo si rahisi tena kutofautisha kati ya habari, maoni na uvumi.