Twiga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pitio kulingana na tarehe 19:34, 28 Septemba 2016 na ChriKo (majadiliano | michango) (Nyongeza spishi)
Twiga
Twiga kusi
Twiga kusi
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mammalia (Wanyama wanaonyonyesha watoto wao)
Oda: Artiodactyla (Mamalia wanaokanyaga kwa kwato mbili-mbili)
Nusuoda: Ruminantia (Wanyama wanaocheua)
Familia: Giraffidae (Wanyama walio na mnasaba na twiga)
Jenasi: Giraffa (Twiga)
Brünnich, 1771
Ngazi za chini

Spishi 11:

Twiga ni jenasi ya wanyama ya Afrika katika familia Giraffidae. Spishi hizi ni mamalia wenye kwato shufwa na shingo ndefu kuliko ile ya wanyama wote wa nchi kavu. Mwili wao umepambwa kwa madoa yasiyo na umbo maalumu, yenye rangi ya njano mabaka meusi na kutenganishwa na rangi nyeupe, au rangi ya manjano-kahawia.

Twiga wana uhusiano na tandala na ng’ombe, lakini wanawekwa kwenye familia yao pamoja na ndugu wao wa karibu okapi. Wanapatikana hasa kuanzia Nijeri mpaka Afrika Kusini.

Twiga huishi hasa maeneo ya savanna na nyika. Hata hivyo wakati chakula kinapokuwa adimu, hupendelea maeneo yenye miti mingi, migunga na vikwata hasa. Hunywa maji mengi sana wakati yanapopatikana ili kukabili ukame ukija.

Mabadiliko ya zamani

Twiga ni spishi nne katika familia ya Giraffidae pamoja na okapi. Familia hii hapo awali ilikuwa na wanyama wengi kiasi. Twiga huaminika kuwa walitokana na swala aliyekuwa na urefu wa futi 3 tu, mnamo miaka milioni 30–50 iliyopita.

Kutokea kwa shingo ndefu ya twiga kumezua mjadala mkubwa sana. Hadithi iliyozoeleka ni kwamba ilikuwa ni kutokana na juhudi za twiga kuyafikia matawi ya juu ya miti wakati wa ushindani wa chakula na wanyama wenzie walao majani.

Kuna nadharia nyingine isemayo kuwa twiga dume ndio waliokuwa na shingo ndefu kuleta tofauti na jike, na kuweza kufikia majani ya juu ili kupata chakula, kukua kwa shingo zao kulikuwa tu ni kama ukuaji wa pilic baada ya balehe. Hata hivyo, nadharia hii ya pili haikubaliki sana na kulingana na tafiti za hivi karibuni, imeonyesha udhaifu mkubwa na kubakiza nadharia ile ya kuanza peke yake.

Hata madoa ya twiga yanaaminika kuwa hapo awali yalikuwa ni ya rangi angavu juu ya mwili wa ngozi nyeusi. Madoa hayo taratibu yaliendelea kuwa ya muundo wa nyota na maua, leo hii yamekuwa hayana umbo maalumu.

Pembe

Twiga katika zoo
Twiga mama na mtoto
Twiga wakijamiiana

Jinsia zote wana pembe, japo pembe za twiga jike ni ndogo. Na kwa pembe hizi unaweza ukatambua jinsia ya twiga kwa urahisi, kwa sababu twiga jike wana nywele juu ya nundu za pembe zao, huku pembe za twiga dume zikiwa na vipara tu. Twiga dume wakati mwingine huwa na mkusanyiko wa kalsiamu kwenye fuvu zao za kichwa, ambao (mkusanyiko) hukua kadiri wanavyoongezeka umri, na kuwa kama nundu nyingine na kufanya jumla ya nundu kuwa tatu.

Shingo

Twiga wana shingo ndefu wanaoitumia kula majani ya miti mirefu kabisa. Twiga wana pingili saba za mifupa ya shingoni, kama wanyama wengine, japo baadhi ya wataalamu wanadai zipo nane zaidi, mifupa hiyo ina maungio.

Miguu na miondoko

Twiga wana miguu mirefu sana, kwa kadiri ya 10% zaidi ya miguu ya nyumbu. Mwendo wa twiga ni wa maringo, lakini akiwa anafukuzwa hukimbia sana, mpaka kufikia mwendokasi wa km. 55 kwa saa. Twiga ni kazi kuwindwa, na ni hatari. Wanapendwa hujihami kwa teke la nguvu. Teke la twiga mkubwa ni laweza kupasua fuvu la kichwa cha simba au hata kuvunja uti wa mgongo. Simba pekee ndio wanyama wanaoweza kuwa tishio kwa twiga.

Mfumo wa mzunguko wa damu

Moyo wa twiga una uzito wa kg. 10 na una urefu wa sm. 60, na hutakiwa kuzalisha mgandamizo wa damu mara mbili zaidi ukilinganisha na wanyama wa kawaida, ili kusaidia kusukuma damu mpaka kwenye ubongo, kichwani. Karibu na shingo kuna mfumo wa damu tata, unaomida damu nyingi isiende kwenye ubongo wakati twiga anapoinamisha kichwa chake pia.

Tabia

Twiga jike hujikusanya pamoja kwenye makundi ambao wakati mwingine hujumuisha twiga dume wadogo. Twiga dume wadogo hao hupenda kujiunga na dume wakubwa. Utafiti wa mwaka 1920 ulithibitisha kuwa twiga hawachangamani na twiga wasio wa kundi moja. Pia pindi dume atakapo kumpanda jike, basi huchagua yeyote aliye katika kipindi cha joto, kwenye kundi lolote. Twiga dume hutambua twiga jike walio katika kipindi cha joto kwa kuonja ladha ya mikojo yao. Twiga huchangamana vizuri na wanyama wengine wala nyasi. Kuwa pamoja na twiga hawa ni faida kubwa, kwa sababu urefu wao husaidia hata kuona adui wakiwa tangu mbali.

Uzazi

Twiga hubeba mimba kwa siku 400 mpaka 460 ambapo mara nyingi huzaa ndama mmoja hatimaye japo mapacha hutokea mara kadhaa. Mama hujifungua akiwa amesimama na kende lake hukatika mtoto aangukapo ardhini. Ndama akizaliwa huwa na urefu wa mita 1.8. Baada ya masaa kadhaa, mama huweza kukimbia japo ndani ya wiki mbili za mwanzo ndama hutumia muda mwingi kujilaza chini huku akilindwa na mama yake. Ndama huyo huwa hatamaniwi kuwindwa na simba, chui, fisi au mbwa mwitu. Ni asilimia 25–50 tu ya twiga ndiyo hufikia kuwa wakubwa. Twiga hukadiriwa kuishi miaka 20–25 mwituni na miaka 28 wakifugwa nje ya mbuga.

Kushindana/kupigana kwa shingo

Twiga mapiganoni

Kitendo hiki cha twiga kufanywa kwa madhumuni mbali mbali lengo mojawapo ni kupigana vita, vita vinaweza kuwa kubwa kwelikweli. Kadiri shingo inavyokuwa ndefu, ndipo kichwa napo kinapokuwa kikubwa zaidi, na nguvu ya kupigana huwa kubwa vile vile. Na imeonekana twiga dume wanaofanikiwa kupata jike wa kujamiiana ni wale twiga dume waliofanikiwa kushinda kwenye vita. Ndiyo maana husikika kuwa, shingo ndefu imetokana na ushindani wa kijinsia, lakini mara nyingine twiga, husuguana tu shingo zao kwa kujipatia raha/ashki ya kimapenzi. Tena ajabu, twiga dume, wao kwa wao ndio hushiriki zaidi zoezi hili hasa nyakati za upweke. Mhemko wakati wa shughuli hii unaweza kuwa mkubwa mpaka kufikia kileleni.

Kulala

Twiga ni miongoni mwa mamalia wanaolala kwa muda kidogo kuliko wote, na hulala kwa wastani wa dakika kumi mpaka saa 2 katika masaa 24 ya siku moja na kuwa na wastani wa saa 1. za kulala kwa siku.

Chakula

Twiga anayekula

Twiga hula majani ya miti, na pia hula nyasi nyingi na matunda. Ulimi wake ni mgumu sababu mlo wa twiga huhusisha miiba pia. Twiga anaweza kula mpaka kilo 29 za majani kwa siku, lakini anaweza hata kustahimili kwa kilo 6.8 tu za nyasi. Twiga hula kidogo sana kwa sababu hupata chakula chenye virutubisho vingi sana na pia mfumo wake wa mmeng’enyo wa chakula ni wa uhakika sana. Twiga pia huweza kukaa kwa vipindi virefu bila kunywa maji. Ulimi wa twiga una urefu wa takribani sentimeta 45.

Spishi

Spishi za kabla ya historia

  • Giraffa gracilis
  • Giraffa jumae
  • Giraffa priscilla
  • Giraffa punjabiensis
  • Giraffa pygmaea
  • Giraffa sivalensis
  • Giraffa stillei

Picha

Marejeo

Ili kupata maelezo kuhusu masanduku ya uanapwa ya spishi angalia: Wikipedia:WikiProject Mammals/Article templates/doc.