Nenda kwa yaliyomo

Togo ya Kiingereza

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Togo iligawiwa 1918; magharibi liliwekwa chini ya Ghana (=Goald Coast), mashariki ikawa chini ya Ufaransa

Togo ya Kiingereza ilikuwa eneo lililokabidhiwa mkononi wa Uingereza baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Mwaka 1914 Uingereza na Ufaransa walipatana kuvamia Togo ya Kijerumani na kugawana eneo lake. Theluthi ya magharibi ya koloni ya Kijerumani iliwekwa chini ya Uingereza na kutawaliwa pamoja na maeneo ya Ghana. Sehemu kubwa zaidi ilikuwa chini ya Ufaransa.

Katika Mkataba wa Versailles iliamuliwa ya kwamba koloni za kale za Ujerumani zitakuwa chini ya mamlaka mkuu wa Shirikisho la Mataifa zikitawaliwa na nchi zinazotekeleza utawala. Nafasi ya Shirikisho la mataifa ilichukuliwa baada ya 1945 na Umoja wa Mataifa.

Waingereza walitawala Koloni ya Pwani la Dhahabu, eneo la kulindwa la Ashanti na maeneo ya kaskazini pamoja na Togo ya Kiingereza kama vitengo vinne chini ya Gavana wa Cape Coast. Mwaka 1946 walifuta vitengo na kutawala yote kama "Pwani la Dhahabu".

Masharti ya UM yalikuwa nadharia tu kwa muda mrefu lakini yalipata umuhimu tena wakati wa uhuru. Kwa sababu hiyo wakazi wa maeneo ya Ghana yaliyowahi kuwa sehemu za eneo la Togo ya Kijerumani walipewa nafasi ya kuamua kama wangependelea kuendelea na Ghana au kuunganishwa tena na Togo yenyewe.

Katika kura ya Desemba 1956 waliamua kubaki upande wa Ghana.