Nenda kwa yaliyomo

Theogonia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Theogonia (Kigiriki cha Kale: Θεογονία, Theogonía, maana yake “vizazi au kuzaliwa kwa miungu”) ni shairi la Hesiodo (karne ya 8–7 K.K.) linaloelezea asili na nasaba za miungu ya Kigiriki. Lilitungwa takribani mwaka 730–700 K.K. kwa lahaja ya kishairi ya Kigiriki cha kale na lina mistari 1,022. Ni mojawapo ya vyanzo muhimu zaidi vya kuelewa ulimwengu wa kale wa Kigiriki (kosmolojia ya awali ya Wagiriki).

Theogonia ya Hesiodo ni muunganiko mkubwa wa desturi mbalimbali za kienyeji za Kigiriki kuhusu miungu, uliopangwa kama simulizi linaloeleza jinsi miungu ilivyoanza kuwepo na jinsi ilivyopata mamlaka ya kudumu juu ya ulimwengu. Ni hadithi ya kwanza inayojulikana ya uumbaji wa ulimwengu (kosmogonia) katika utamaduni wa Kigiriki. Hali ya awali ya ulimwengu ilielezwa kama “khaos”, yaani utupu wenye giza usio na mipaka, uliotazamwa kama hali ya kimungu ya mwanzo ambayo vitu vyote vilitokea kutoka humo. Theogonia na hadithi nyingine za aina hiyo ni sehemu ya visasili vya kigiriki zinazodhihirisha hamu ya kuelezea uhalisia wa ulimwengu mzima kwa jumla; msukumo huu wa kutaka kuelewa mambo kwa ujumla ndio uliokuwa msingi wa michakato ya awali ya kufikiri kwa falsafa.[1]

Zaidi ya hayo, katika kipande kinachoitwa “Wafalme na Waimbaji” (mistari 80–103)[2], Hesiodo anajipa mamlaka ambayo kwa kawaida yalihusishwa na ufalme mtakatifu. Mshairi anatangaza kwamba ni yeye, (ambapo tungetarajia mfalme) ndiye ambaye Muza wamempa zawadi mbili: fimbo ya kifalme na sauti yenye mamlaka (Theogonía, mistari 30–33), ambazo ni alama zinazoonekana za kifalme. Si kwamba tendo hili linakusudia kumfanya Hesiod kuwa mfalme, bali kusisitiza kwamba mamlaka ya kifalme sasa yanamilikiwa na sauti ya kishairi, sauti inayosoma na kutangaza Theogonia.

Muza tisa kwenye jeneza la Kirumi (karne ya pili BK) - Louvre, Paris.

Ingawa mara nyingi Theogonia hutumiwa kama kitabu cha rejea cha visasili vya kigiriki, kwa kweli ni zaidi na pia pungufu ya hilo. Kwa mtazamo wa kimaumbo, ni wimbo wa kishairi (hymn) unaomwomba Zeu na Muza. Ulinganifu kati ya sehemu fulani za Theogonia na Wimbo wa Kihomeri kwa Muza, (ambao ni fupi zaidi) unaonyesha wazi kwamba Theogonia ilitokana na desturi ya nyimbo za utangulizi ambazo warapsodi (waimbaji au wasimuliaji wa kale wa mashairi) wa Kigiriki walitumia kuanzisha utumbuizaji wao katika mashindano ya kishairi. Ni muhimu kuelewa kwamba Theogonia siyo chanzo cha mwisho au kamili cha hadithi za Kigiriki, bali ni taswira ya muda maalum ya mapokeo hai ambayo yalipata umbo la kudumu wakati Hesiodo alipoyatunga hadithi alizojua. Ni lazima pia tukumbuke kwamba mapokeo hayo yameendelea kubadilika tangu wakati huo hadi sasa.

Umbo lililoandikwa la Theogonia liliimarishwa katika karne ya 6 K.K. Hata baadhi ya wahariri wahafidhina wamehitimisha kwamba kipindi cha Typhon (mistari 820–868) kimeingizwa baadaye (interpolation).

Inawezekana kwamba Hesiodo aliathiriwa na baadhi ya desturi za Mashariki, kama vile Nasaba ya Babiloni ya Dunnum,[3] ambazo ziliunganishwa na desturi za kienyeji. Hata hivyo, inaonekana ni alama za kuendelea kuwepo kutoka desturi za kimikene kuliko matokeo ya mawasiliano ya moja kwa moja na Mashariki wakati wa Hesiodo.

Nakala za maandishi

[hariri | hariri chanzo]

Nakala za kale zaidi zilizopo za Theogonia zinatoka mwishoni mwa karne ya 13. Mfano wa awali ni Vaticanus gr. 1825, ambao unakadiriwa kuwa umetengenezwa takriban mwaka 1310 kulingana na alama za maji (watermarks). Kuna takriban nakala 64 zinazojulikana ambazo zinatoka mwaka 1600 au kabla yake.[4][5]

Maoni ya Kikristo ya Theogonia

[hariri | hariri chanzo]

John Milton aliona Theogonia kama ikichochewa na Shetani. Mtazamo wa Milton, uliofafanuliwa katika Paradise Lost, ulikuwa kwamba mara Shetani alipotupwa kutoka mbinguni, alikuwa Muza aliyemchochea Hesiodo. Kwa hiyo, kile Hesiodo alichoandika kilionekana kama kudhoofisha au kuharibu matukio “halisi” yaliyotokea katika mapambano ya Shetani dhidi ya Mungu. Zaidi ya hayo, Milton aliweka msisitizo kwamba ushindi wa Zeu (yaani miungu ya juu) kupitia hila, mazungumzo, na muungano na wengine, ulikuwa ukosefu wa ukweli kwa sababu Nguvu ya Mungu haihitaji mshirika yeyote.[6]

Mtazamo wa Milton unafanana na wa waandishi wa mapadre wa Kikristo wa mwanzo. Kwa mfano, Yustino Mfiadini na Athenagora wa Athene walidai kwamba visasili vya kienyeji kwa ujumla ni uharibifu wa kishetani wa historia halisi ya ulimwengu. [6]

  1. Sandwell, Barry (1996). Presocratic Philosophy vol.3. New York: Routledge. ISBN 9780415101707.
  2. Stoddard, Kathryn B. (2003). "The Programmatic Message of the 'Kings and Singers' Passage: Hesiod, Theogony 80-103". Transactions of the American Philological Association. 133 (1): 1–16. doi:10.1353/apa.2003.0010. JSTOR 20054073. S2CID 161532502.
  3. Lambert, Wilfred G.; Walcot, Peter (1965). "A New Babylonian Theogony and Hesiod". Kadmos. 4 (1): 64–72. doi:10.1515/kadm.1965.4.1.64. S2CID 162417685.
  4. M. L. West (Novemba 1964). "The Medieval and Renaissance Manuscripts of Hesiod's Theogony". The Classical Quarterly. 14: 165–189. doi:10.1017/S0009838800023739. JSTOR 637722.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  5. Guillermo Galán Vioque (2009). "Notes on a Forgotten Manuscript of Hesiod's "Theogony"". Mnemosyne. Fourth Series. 62 (1): 1–10. doi:10.1163/156852508X252885. JSTOR 27736292.
  6. 1 2 Philip J. Gallagher (Winter 1979). "Paradise Lost and the Greek Theogony". English Literary Renaissance. 9. The University of Chicago Press: 121–148. doi:10.1111/j.1475-6757.1979.tb01404.x. JSTOR 43446941.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link) Hitilafu ya kutaja: Invalid <ref> tag; name "Gallagher" defined multiple times with different content

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]