The Mechanic (filamu ya 1972)
| The Mechanic | |
|---|---|
Posta ya filamu ya "The Mechanic" (1972). | |
| Imeongozwa na | Michael Winner |
| Imetayarishwa na | Irwin Winkler |
| Imetungwa na | Lewis John Carlino |
| Nyota | Charles Bronson Jan-Michael Vincent Keenan Wynn |
| Muziki na | Jerry Fielding |
| Sinematografi | Arthur J. Ornitz |
| Imehaririwa na | John Howard |
| Imesambazwa na | United Artists |
| Imetolewa tar. | 1972 |
| Ina muda wa dk. | 98 dakika |
| Nchi | Marekani |
| Lugha | Kiingereza |
| Bajeti ya filamu | $3,000,000 |
| Mapato yote ya filamu | $21,000,000 |
| Ikafuatiwa na | The Mechanic 2011 |
The Mechanic ni filamu ya mapigano na kusisimua ya mwaka 1972 kutoka nchini Marekani. Iliongozwa na Michael Winner na kutungwa na Lewis John Carlino. Filamu hii inamshirikisha Charles Bronson katika ushirikiano wake wa pili na Winner, pamoja na Jan-Michael Vincent kama wahusika wakuu. Waigizaji wasaidizi ni pamoja na Keenan Wynn, Jill Ireland, na Frank de Kova.
Hadithi inamfuata Arthur Bishop (Bronson), muaaji wa kulipwa mwenye ustadi mkubwa, anayemchukua chini ya uangalizi wake Steve McKenna (Vincent), ambaye ni mtoto mwenye tamaa na ukatili wa Harry McKenna (Wynn), kiongozi wa zamani wa shirika la kijasusi analofanyia kazi Bishop. Filamu hii inajulikana kwa sehemu yake ya mwanzo, ambayo haina mazungumzo kwa dakika 16 za kwanza, huku mhusika wa Bronson akijitayarisha kumuua shabaha yake. Jina la filamu linarejelea neno la mafumbo linalotumiwa kwa muaaji wa kulipwa.
Filamu ilipopigwa kwa mara ya kwanza, ilipata maoni mchanganyiko kutoka kwa wakosoaji, lakini ilisifiwa kwa sehemu zake za mapigano, uigizaji, na picha zake za filamu, ingawa uongozaji wa Winner na namna hadithi ilivyosimuliwa vilikosolewa. Toleo jipya la jina hilo hilo lilitolewa mwaka 2011, ambalo pia lilipokelewa kwa maoni yaliyogawanyika.
Muhtasari wa hadithi
[hariri | hariri chanzo]Arthur Bishop ni muuaji wa kulipwa mwenye ujuzi wa hali ya juu, anayejulikana kama "mechanic", anayefanya kazi pekee kwa shirika la kimataifa la uhalifu lenye sheria kali sana. Kazi yake inampa maisha ya kifahari—hupenda kusikiliza muziki wa klassiki, ana mkusanyiko wa sanaa, na ni mtaalam wa mivinyo bora. Hata hivyo, analazimika kuishi peke yake—hawezi kuonyesha hisia au kuwaamini watu. Bishop yuko chini ya shinikizo la kihisia kiasi kwamba amepewa dawa za kutuliza msongo wa mawazo. Siku moja, anaanguka na kupoteza fahamu kutokana na mfadhaiko na wasiwasi, na kulazwa kwa muda mfupi hospitalini. Baadaye, Bishop hulipa msichana wa starehe ili kumfanya aonekane ana uhusiano wa kimapenzi, ikiwa ni pamoja na kuandika barua za mapenzi za bandia.
Bishop anapewa kazi ya kumuua mmoja wa viongozi wa shirika hilo, "Big Harry" McKenna. Anamshambulia kwa risasi huku akimfanya aamini kuwa kuna mfyatuaji risasi wa siri. Harry, ambaye Bishop anajua ana tatizo la moyo, anakimbia juu ya kilima kikiwa na mteremko mkali, jambo linalosababisha mshtuko wa moyo. Bishop anamkamilisha kwa kumpiga na kumkaba hadi kufa.
Katika mazishi ya Big Harry, Bishop anakutana na mtoto wa Harry mwenye tabia ya ubinafsi, ukatili, na tamaa ya madaraka, aitwaye Steve. Steve anavutiwa na Bishop na anatafuta kujua zaidi kumhusu. Bishop pia anavutiwa naye. Baada ya muda, na kutokana na msukumo kutoka kwa Steve, Bishop hatimaye anamweleza kazi yake ya muaaji wa kulipwa. Anamweleza Steve kila kitu anachojua na kumpa funzo la kipekee.
Katika mafunzo yake, Bishop anamfundisha Steve kuwa "kila mtu ana udhaifu, na ukishagundua udhaifu wake, ni rahisi kumuua". Hata hivyo, Bishop hakupata ruhusa kutoka kwa wakuu wake kabla ya kumpa Steve mafunzo hayo. Kufuatia mauaji yaliyofanyika kwa fujo na Bishop pamoja na Steve, shirika linampa Bishop onyo kali, likisema kuwa chaguo lake la kumhusisha Steve limeonekana kuwa la ubinafsi.
Shirika linampa Bishop misheni ya dharura, safari hii nchini Italia. Bishop bado anamshirikisha Steve katika mpango mpya, lakini kabla hawajaondoka, Bishop anapata jalada lenye taarifa zake miongoni mwa vitu vya Steve. Jalada hilo linafanana kabisa na majalada anayopokea kutoka kwa shirika. Hata hivyo, Bishop anampa Steve ruhusa kwenda naye Italia.
Italia, Bishop na Steve wanaelekea kwenye boti ambapo shabaha yao inapaswa kuwepo, lakini ni mtego, na wao ndio walengwa wa mauaji. Wanavamiwa, lakini wanafanikiwa kuwaua maadui wao wote.
Walipokuwa wakipakia mizigo yao hotelini, Steve anashiriki chupa ya divai na Bishop, huku akiweka sumu ya brucine kwenye glasi ya Bishop. Bishop anapogundua kuwa amepewa sumu, Steve anamdhihaki, akisema "Ulisema kila mtu ana sehemu dhaifu. Yako ni kwamba huwezi kuhimili ukiwa pekee yako". Bishop anapomuuliza Steve ikiwa ni kwa sababu Bishop alimwua baba yake, Steve anajibu hakujua kama baba yake aliuawa. Steve anafichua kwamba hakufuata maagizo ya kumuua Bishop, bali ni muuaji wa kujitegemea aliyesema "Nitachagua mlengwa wangu mwenyewe, nimpige pale ninapotaka".
Steve anarudi nyumbani kwa Bishop kuchukua gari lake, Ford Mustang. Anapoingia ndani ya gari tayari kuliwasha, anaona karatasi iliyobandikwa kwenye kioo cha nyuma, ikisomeka:
"Steve, ikiwa unasoma hii, basi sikufanikiwa kurudi. Pia inamaanisha kuwa umevunja uzi unaodhibiti mlipuko wa sekunde 13. Mwisho wa mchezo. Boom! Umeuawa."
Steve anapojaribu kufungua mlango kwa haraka, gari linapasuka na kumuua.
Waigizaji
[hariri | hariri chanzo]- Charles Bronson kama Arthur Bishop
- Jan-Michael Vincent kama Steve McKenna
- Keenan Wynn kama Harry McKenna
- Jill Ireland kama Msichana
- Linda Ridgeway kama Louise
- Frank de Kova kama Mwanamume
- Takayuki Kubota kama Yamoto
- Patrick O'Moore kama Mzee
- Enzo Fiermonte kama Mlengwa
- Celeste Yarnall kama Mpenzi wa Mlengwa
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Froug, William (1991). The screenwriter looks at the screenwriter. Silman-James press.
- Russo, Vito (1987). The Celluloid Closet: Homosexuality in the Movies (rev. ed). New York: Harper & Row. ISBN 0-06-096132-5.
- Stevens, Brad (2003). Monte Hellman: His Life and Films. McFarland. ISBN 0-7864-1434-0.