Siasa ya Gabon
|
Nembo ya Taifa ya Gabon | |
| Aina ya Serikali | Jamhuri ya Kifederali ya Urais |
| Rais wa Nchi | Brice Clotaire Oligui Nguema |
| Makamu wa Rais | Séraphin Moundounga |
| Chama Tawala | Union démocratique des Bâtisseurs (UDB) |
| Vyama Vikuu | UDB, Gabonese Democratic Party (PDG), RPM, Les Démocrates |
| Uchaguzi wa Mwisho | Aprili 12, 2025 |
| Uchaguzi Ujao | Mnamo 2032 |
| Katiba | Katiba ya 2024 |

Siasa ya Gabon inaendeshwa kwa mfumo wa demokrasia ambapo Rais ndiye mkuu wa nchi na serikali. Ingawa mfumo wa vyama vingi ulianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1990, chama tawala kimeendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za nchi hiyo. Tangu ilipopata uhuru kutoka kwenye utawala wa Ufaransa mnamo1960, Gabon imekuwa na mlolongo wa viongozi wachache lakini wenye utawala wa muda mrefu, hali iliyojenga siasa zenye mvuto wa kihistoria, kiuchumi, na kijamii.[1]
Uhuru na Uongozi wa Awali (1960–1967)
[hariri | hariri chanzo]Gabon ilijipatia uhuru kutoka Ufaransa mnamo Agosti 1960. Rais wa kwanza alikuwa Léon M'ba, ambaye aliongoza hadi kifo chake mwaka 1967. Uongozi wake ulijengwa kwa misingi ya urafiki wa karibu na nchi ya Ufaransa, na alitetea mfumo wa chama kimoja.[2]
Uongozi wa Omar Bongo (1967 – 2009)
[hariri | hariri chanzo]Baada ya Léon M'ba, alifuata Albert-Bernard Bongo na baadae Omar Bongo Ondimba alichukua uongozi na alitawala kwa takribani miaka 42, akawa mmoja wa marais waliotawala kwa muda mrefu zaidi duniani.
Mwaka 1968, alianzisha chama tawala Parti Démocratique Gabonais (PDG), na kuifanya Gabon kuwa nchi ya chama kimoja hadi 1990. Shinikizo la ndani na nje lilisababisha kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mnamo 1991, ingawa PDG iliendelea kushinda uchaguzi kwa asilimia kubwa.
Uongozi wa Ali Bongo (2009 – 2023)
[hariri | hariri chanzo]Baada ya kifo cha Omar Bongo mwaka 2009, mwanawe Ali Bongo Ondimba alichaguliwa kuwa rais kupitia chama cha PDG. Utawala wake ulijawa na tuhuma za ubadhirifu wa kura katika uchaguzi, ukandamizaji wa upinzani, na maandamano ya mara kwa mara. Ali Bongo alishinda chaguzi za 2016 na 2023, licha ya pingamizi kutoka kwa vyama vya upinzani.
Mapinduzi ya Kijeshi (2023)
[hariri | hariri chanzo]Mnamo Agosti 30, 2023, jeshi la Gabon lilitangaza kumpindua Ali Bongo baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wenye utata. Mapinduzi hayo yalifanywa na kundi lililojitambulisha kama Kamati ya Mpito kwa Taasisi na Amani (CTRI), inayoongozwa na Jenerali Brice Oligui [3]Nguema, ambaye baadaye aliapishwa kuwa Raisi wa mpito.[4]
Mapinduzi haya yalipokelewa kwa mitazamo tofauti wakati baadhi ya raia walionyesha furaha wakitumaini mabadiliko, jumuiya ya kimataifa ilionyesha wasiwasi kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini Gabon.
Muundo wa Serikali
[hariri | hariri chanzo]Gabon ina serikali ya urais mkubwa, ambapo rais huchaguliwa kwa muda wa miaka mitano (hapo awali miaka saba). Rais huteua waziri mkuu, ambaye anasimamia baraza la mawaziri. Bunge linajumuisha Bunge la Kitaifa na Seneti, ingawa mamlaka ya kisheria mara nyingi yamekuwa dhaifu mbele ya nguvu ya urais.
Vyama vya Siasa
[hariri | hariri chanzo]Gabon ina mfumo wa vyama vingi vya siasa, lakini kwa muda mrefu, siasa zake zilitawaliwa na chama cha Parti Démocratique Gabonais (PDG), ambacho kilikuwa chama tawala tangu 1968 hadi mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2023[5]. Mapinduzi hayo yalimuondoa madarakani Rais Ali Bongo Ondimba na kukatiza uongozi wa kizazi cha familia ya Bongo baada ya zaidi ya miaka 50 ya utawala.
Baada ya mapinduzi hayo, Jenerali Brice Clotaire Oligui Nguema alichukua uongozi wa mpito, na baadaye alishinda uchaguzi wa rais uliofanyika Aprili 12, 2025 kwa zaidi ya asilimia 90 ya kura[6]. Kufuatia ushindi huo, alianzisha chama kipya kiitwacho Union Démocratique des Bâtisseurs (UDB), kilichozinduliwa rasmi mnamo Julai 2025. Na ndicho chama tawala cha sasa nchini Gabon.
Chama hicho kipya kimevutia wanachama wengi kutoka chama tawala za zamani PDG na vyama vingine vya siasa, hivyo kubadilisha kabisa mandhari ya kisiasa ya nchini humo. PDG, licha ya kuwa na historia ndefu ya kutawala, sasa kinaonekana kuwa chama cha upinzani kilicho na ushawishi mdogo.
Vyama vingine vya upinzani kama:
- Union Nationale (UN)
- Rassemblement pour la Patrie et la Modernité (RPM)
- Les Démocrates (LD)
- Parti Républicain Démocratique (PRD)
vimeendelea kuwepo, lakini vina ushawishi mdogo katika siasa za kitaifa, hasa kutokana na ukosefu wa rasilimali, changamoto za kiutawala, na mazingira mapya ya kisiasa yanayoendelea kujengwa baada ya mabadiliko ya utawala na katiba[7].
Mabadiliko ya Katiba
[hariri | hariri chanzo]Mnamo Novemba 2024, katiba mpya ya Gabon ilipitishwa kupitia kura za maoni. Katiba hii ilifuta wadhifa wa Waziri Mkuu, ikampa Raisi mamlaka makubwa zaidi ya kiutendaji, na kuanzisha utaratibu wa uchaguzi wa Raisi kwa vipindi viwili vya miaka saba[8]. Masharti mapya ya kikatiba pia yalilenga kuzuia siasa za kurithishana madaraka ndani ya familia.
Siasa za Kigeni
[hariri | hariri chanzo]Gabon ni mshirika wa karibu wa Ufaransa, na ina uhusiano mzuri na mataifa ya Magharibi. Aidha, ni mwanachama wa mashirika mbalimbali ya kikanda na kimataifa kama Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN), na Jumuiya ya Afrika ya Kati (ECCAS).
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Freedom House. (2022). Gabon: Freedom in the World Report. Retrieved from www.freedomhouse.org
- ↑ Britannica. (2023). Politics of Gabon. Retrieved from www.britannica.com
- ↑ Al Jazeera. (2023). Who is Brice Oligui Nguema, Gabon’s coup leader? Retrieved from www.aljazeera.com
- ↑ BBC News. (2023). Gabon coup: Army seizes power after disputed election. Retrieved from www.bbc.com
- ↑ "Gabon swears in former military chief as president, signalling return to constitutional order". AP News (kwa Kiingereza). 2025-05-03. Iliwekwa mnamo 2025-07-21.
- ↑ Obangome, Gerauds Wilfried; Dione, Ngouda (2025-04-13), "Gabon's leader Nguema elected president with 90.35% of vote, interior minister says", Reuters (kwa Kiingereza), iliwekwa mnamo 2025-07-21
- ↑ Au Gabon, le général Brice Oligui Nguema se taille une Constitution sur mesure (kwa Kifaransa), 2024-10-25, iliwekwa mnamo 2025-07-21
- ↑ Au Gabon, le général Brice Oligui Nguema se taille une Constitution sur mesure (kwa Kifaransa), 2024-10-25, iliwekwa mnamo 2025-07-21
| Makala hii kuhusu mambo ya siasa bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Siasa ya Gabon Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |