Nenda kwa yaliyomo

Shoghi Effendi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Shoghí Effendi (1896 au 1897 – Novemba 4, 1957) alikuwa Mlinzi wa Dini ya Bahá'í kutoka 1922 hadi kifo chake mwaka wa 1957.[1] Kama mjukuu na mrithi wa ʻAbdu'l-Bahá, alipewa jukumu la kuongoza maendeleo ya Imani ya Kibahá'í, likiwemo kuunda muundo wake wa kiutawala wa kimataifa na kutekeleza mfululizo wa mipango ya ufundishaji ambayo iliongoza upanuzi wa dini hiyo katika nchi kadhaa mpya. Kama mfasiri aliyeidhinishwa wa Maandiko ya Kibahá'í tafsiri zake za Maandiko yalizoandikwa na watendaji wakuu wa Imani hii, zilitoa umoja wa ufahamu kuhusu mafundisho muhimu ya Imani na kuwalinda wafuasi wake dhidi ya mgawanyiko. Baada ya kifo chake mwaka wa 1957, uongozi ulishikiliwa na Mikono wa Imani, na mwaka wa 1963 Wabahá'í wa ulimwengu walichagua Nyumba ya Haki ya Ulimwengu, taasisi ambayo ilikuwa imeelezewa na kupangwa na Baháʼu’lláh.[2]

Effendi, Afnán, alizaliwa kama Shoghí Rabbání huko ʻAkká (Acre) ambako alitumia maisha yake ya awali,[3] lakini baadaye aliendelea kusoma katika Haifa na Beirut, akipata digrii ya sanaa kutoka Chuo cha Waprotestanti cha Syria mwaka 1918 na kisha kumhudumia ʻAbdu'l-Bahá kama katibu na mfasiri. Mnamo 1920, alihudhuria Chuo cha Balliol, Oxford, ambako alisoma sayansi ya siasa na uchumi, lakini kabla ya kumaliza masomo yake alifikiwa na habari za kifo cha ʻAbdu'l-Bahá, ambazo zilimlazimu kurudi Haifa. Mara tu baada ya kurudi mwishoni mwa Desemba 1921 alijifunza kwamba katika Wosia na Agano lake ʻAbdu'l-Bahá' alikuwa amemteua kama Mlinzi wa Dini ya Kibaháʼí.[4] Maono ya wazi ya Shoghi Effendi kwa maendeleo ya dini ya Kibaháʼí yalirithiwa kutoka kwa ʻAbdu'l-Bahá na yalitegemea maandiko yenyewe ya Baháʼu’llah, vipengele viwili muhimu sana vya uongozi wake vililenga kujenga utawala wa dini ya Kibaha'i na kueneza imani kote duniani.[5]

Katika miaka yake 36 kama Mlinzi, Shoghi Effendi alitafsiri na kufafanua maandiko mengi ya Bahá’u’lláh na ʻAbdu'l-Bahá, alianzisha mipango iliyoruhusu dini kusambaa kote duniani,[2] na alituma barua zaidi ya 17,500. Aliendelea kuwasiliana na kufuatilia maendeleo katika jamii zote za Kibahá’i zilizopo pamoja na kufuatilia na kukabiliana na hali katika Mashariki ya Kati, ambako waumini bado walikuwa wakiteswa. Pia alianza kazi ya kuanzisha Haifa, Israeli, kama Kituo cha Ulimwengu cha Kibahá’i, na akaunda Baraza la Kimataifa la Wabahá’i kumsaidia katika kazi yake, wajumbe kadhaa wakiwa ni Mikono wa Hoja. Pia alisimamia upanuzi wa jamii kutoka maeneo 1,034 mwaka 1935 hadi 2,700 mwaka 1953, na zaidi hadi maeneo 14,437 mwaka 1963. Kuanzia mwanzoni hadi mwishoni mwa uongozi wake, idadi ya jumla ya Wabahá’i duniani kote ilikua kutoka 100,000 hadi 400,000.[6]

Shoghi Effendi alifariki dunia wakati wa ziara yake mjini London mwaka 1957, baada ya kuambukizwa homa ya Asia,[7] na amezikwa katika Makaburi ya New Southgate jijini London.[8]

Historia

[hariri | hariri chanzo]
Shoghi kijana, c. 1905

Alizaliwa ʻAkká katika Acre Sanjak ya Milki ya Ottoman mnamo 1896 au 1897, Shoghi Effendi alikuwa na uhusiano na Báb kupitia baba yake, Mírzá Hádí Shírází, na uhusiano na Baháʼu'lláh kupitia mama yake, Ḍíyáʼíyyih Khánum, binti mkubwa wa ʻAbdu'l-Bahá.[9] ʻAbdu'l-Bahá, ambaye alitoa mafunzo mengi ya awali, alimuathiri sana Shoghi Effendi tangu mwanzo wa maisha yake. Shoghi Effendi alijifunza sala kutoka kwa babu yake, ambaye alimhimiza aziimbe. ʻAbdu'l-Bahá pia alisisitiza kwamba watu wamuite mtoto huyo "Shoghi Effendi", ("Effendi" maana yake "Bwana"), badala ya kumuita tu "Shoghi", kama ishara ya heshima kwake.[10]

Shoghi Effendi alipokuwa mtoto alifahamu matatizo waliyopitia Wabaháʼí huko ʻAkká, ambayo yalijumuisha mashambulizi kutoka kwa Mírzá Muhammad ʻAlí dhidi ya ʻAbdu’l-Bahá. Mírzá Muhammad-ʻAlí, ambaye alikuwa kaka wa kambo wa ʻAbdu’l-Bahá, na ambaye alihuzunishwa na uteuzi wa ʻAbdu’l-Bahá kama mrithi wa Baháʼu’lláh, alianza kupanga njama za kumchafulia jina kwa kumlaumu kwa uongo kuwa yeye ndio chanzo cha ghasia huko Syria ya Ottoman. Matatizo ambayo yalisababishwa na hili katika jamii ya Wabaháʼí yalihisiwa hata mbali kama Iran na kwingineko.[11] Akiwa kijana mdogo, alijua kuhusu nia ya Sultan Abdul Hamid II (alitawala 1876–1909) ya kumfukuza ʻAbdu'l-Bahá hadi kwenye jangwa la Afrika Kaskazini, ambako alitarajiwa kuangamia.[10]

Barua kutoka kwa ʻAbdu'l-Bahá

[hariri | hariri chanzo]

Akiwa mjukuu wa kwanza wa ʻAbdu'l-Bahá na mwana wa kwanza wa binti mkubwa wa ʻAbdu'l-Bahá Ḍíyáʼíyyih Khánum, Shoghi Effendi alikuwa na uhusiano maalum na babu yake. Zia Baghdadi, mbaháʼí wa wakati huo, anasimulia kwamba wakati Shoghi Effendi alikuwa na umri wa miaka mitano tu, alimshawishi babu yake aandike waraka kwa ajili yake, ambapo ʻAbdu'l-Bahá alifanya hivyo:

Yeye ni Mungu! Ee Shoghi Wangu, sina muda wa kuongea, niache peke yangu! Umesema niandike, nimeandika. Nini kingine kinapaswa kufanywa? Sasa sio wakati wako wa kusoma na kuandika. Ni wakati wa kurukaruka huku ukiimba Ee Mungu Wangu! Kwa hivyo, kariri sala za Uzuri Ulio Barikiwa na uzisome ili niweze kusikia. Kwa sababu hakuna muda wa kitu kingine chochote.[12]

Shoghi Effendi kisha alianza kukariri sala kadhaa, na kuzisema kwa sauti kubwa kadiri alivyoweza. Hii iliwafanya wanafamilia kumuomba ʻAbdu'l-Bahá amnyamazishe, ombi ambalo inaonekana alilikataa.[12]

Elimu ya awali ya Shoghi Effendi ilifanyika nyumbani pamoja na watoto wengine wa nyumba hiyo, na ilisimamiwa na walimu binafsi waliomfundisha Kiarabu, Kifarsi, Kifaransa, Kiingereza, na fasihi. Kuanzia 1907 hadi 1909 alihudhuria taasisi ya Kijerumani iitwayo College des Freres, taasisi ya Kijerumani huko Haifa, ambapo alijifunza Kiarabu, Kituruki, Kifaransa na Kiingereza. Mnamo 1910, wakati ambapo ʻAbdu'l-Bahá alikuwa akiishi Misri kabla ya safari za ʻAbdu'l-Bahá kwenda Magharibi, Shoghi Effendi alijiunga kwa muda mfupi na chuo cha Freres huko Ramleh. Mipango ya yeye kuandamana na babu yake katika safari zake ilivurugika wakati mamlaka ya bandari huko Naples ilipomzuia kuendelea, inasemekana kuwa ni kutokana na masuala ya afya. Aliporudi Misri baada ya Machi 1912 alipelekwa katika shule ya bweni ya Kijerumani huko Beirut, akihamishiwa Oktoba kwenye shule ya maandalizi iliyoko kwenye Chuo cha Kiprotestanti cha Syria mjini Beirut, akihitimu mwaka wa 1913. Baadaye mwaka huo Shoghi Effendi alirudi katika Chuo cha Kiprotestanti cha Syria kama mwanafunzi wa shahada ya kwanza, akipata shahada ya elimu ya sanaa mnamo 1917, lakini licha ya kujiandikisha hapo kama mwanafunzi wa shahada ya uzamili, alirejea Haifa bila kukamilisha shahada yake. Wakati wa muda wake katika Chuo cha Kiprotestanti cha Syria alitumia ziara zake nyumbani Haifa kumsaidia ʻAbdu'l-Bahá katika kutafsiri, na kuwa katibu na mtafsiri wake wa muda wote kuanzia mwishoni mwa 1918.

Shoghi Effendi kabla ya 1940

Katika msimu wa masika wa mwaka wa 1919, wingi wa kazi ya Shoghi Effendi kama katibu ulikuwa umeathiri afya yake, na kusababisha matukio ya mara kwa mara ya malaria. Kufikia msimu wa masika wa mwaka wa 1920, alikuwa katika hali mbaya kiafya kiasi kwamba ʻAbdu'l-Bahá alipanga kwa ajili yake apate nafuu katika sanatorium huko Paris. Baada ya afya yake kurejea, alijiandikisha katika Chuo cha Non-Collegiate Delegacy ya Balliol, Oxford, ili kuboresha ujuzi wake wa kutafsiri Kiingereza.[13]

Kifo cha ʻAbdu'l-Bahá

[hariri | hariri chanzo]

Wakati Shoghi Effendi alipokuwa akijifunza nchini Uingereza, alisikia kuhusu kifo cha ʻAbdu’l-Bahá katika saa za mapema za tarehe 28 Novemba 1921, habari ambazo zilikuja kama mshtuko mkubwa kwani hakuwa na taarifa kuwa babu yake alikuwa mgonjwa.[14] Baada ya kurejea kwake Haifa tarehe 29 Desemba 1921, maagizo ya Wosia wa ʻAbdu'l-Bahá yalitangazwa, yakieleza waziwazi kuwa Shoghi Effendi alikuwa ameteuliwe kama mrithi wa ʻAbdu'l-Bahá na Mlinzi wa dini ya Kibaháʼí.[4][15] Taasisi ya Ulinzi iliundwa na Baháʼu’llah, huku ʻAbdu'l-Bahá akieleza kazi zake maalum na mamlaka katika Wosia wake, kazi mbili muhimu kuwa ni kutafsiri mafundisho ya Kibaháʼí na kuongoza jamii ya Kibaháʼí.[16]

Maisha binafsi na ndoa

[hariri | hariri chanzo]

Maisha binafsi ya Shoghi Effendi yalikuwa kwa kiasi kikubwa yamefunikwa na kazi yake kama Mlinzi,[8] na haikuwa hadi 1950 ambapo aliweza kupata msaada wa kikatibu aliouhitaji ili kushughulikia mawasiliano yaliyoongezeka. Kufikia wakati huo alikuwa ameanzisha ratiba iliyojaa kazi ngumu mfululizo alipokuwa Haifa, na mapumziko wakati wa kiangazi ambapo alitumia muda barani Ulaya, mwanzoni kwenye Milima ya Alps ya Uswisi, akiivuka Afrika kutoka kusini hadi kaskazini mnamo 1929 na 1940. Mnamo 1937 alimuoa Mary Maxwell, binti wa msanifu majengo wa Kanada William Sutherland Maxwell na May Maxwell, na kumpa jina Rúhíyyih Khánum. Shoghi Effendi alikutana kwa mara ya kwanza na Mary mnamo 1923 alipokwenda hija na mama yake, na ilikuwa wakati wa hija ya tatu mnamo 1937 ambapo Shoghi Effendi alimwomba mama yake idhini ya kufunga ndoa na binti yake. Ndoa ilifanyika Haifa mnamo 25 Machi 1937, katika chumba cha Bahíyyih Khánum katika Nyumba ya ʻAbdu'l-Bahá. Baada ya sherehe ujumbe ulitumwa Marekani ukisema, "Tangazeni sherehe za Mabaraza harusi ya Mlinzi mpendwa. Heshima isiyo na kifani aliyopewa mjakazi wa Baháʼu'lláh Ruhiyyih Khanum Miss Mary Maxwell. Muungano wa Mashariki na Magharibi uliosemwa na Imani ya Kibaháʼí umeimarishwa. Ziaiyyih mama wa Mlinzi."[17] Rúhíyyih Khánum, kama alivyokuwa anajulikana tokea hapo, alikua sio tu mke wake bali pia msaidizi wake wa maisha yake yote katika kazi yake.[18] Shoghi Effendi alikuwa na uraia wa Irani (Uajemi) wakati wote wa maisha yake na kusafiri kwa pasi ya kusafiria ya Irani, ingawa hakuwahi kufika Irani.[3]

Mtindo wa Uongozi

[hariri | hariri chanzo]

Shoghi Effendi alikuwa na umri wa miaka 24 alipochukua nafasi ya Ulinzi wa dini ya Kibaháʼí, na baada ya mapumziko mafupi ya kujiandaa kwa majukumu haya, alianza kutekeleza kazi hiyo. Akiwa na elimu ya Magharibi na mavazi ya Magharibi, mtindo wa uongozi wa Shoghi Effendi ulikuwa wa kipekee ukilinganishwa na wa babu yake ʻAbdu'l-Bahá. Barua zake kwa Wabaháʼí zilisainiwa "ndugu yako wa kweli", na badala ya kuzingatia nafasi yake ya kibinafsi kama Mlinzi, mtazamo wake ulikuwa kwenye taasisi ya ulinzi. Aliweka nguvu zake katika kujenga dini hiyo ulimwenguni kote, kuweka msingi wa utawala katika Nchi Takatifu, na kutumia mawasiliano mengi kwa njia ya barua badala ya kusafiri moja kwa moja ili kutoa ushauri kwa jamii inayokua duniani. Alikuwa akitumia muda na Wabaháʼí wengi waliotembelea Haifa kwa ajili ya hija, akiwahamasisha na kuwafundisha na mara nyingi akiwatumia kama wajumbe wanaporudi kwenye jumuiya zao za nyumbani.[8]

Usimamizi

[hariri | hariri chanzo]

Moja ya malengo makuu ya Shoghi Effendi alipokuwa Mlinzi ilikuwa kuandaa kazi ya utawala ya Kituo cha Ulimwengu cha Wabaháʼí, kwa kuanzia akilenga kwenye kudumisha mawasiliano na idadi inayoongezeka ya Wabaháʼí duniani kote. Hii ilihusisha uhitaji wa msaada wa kikatibu ambao katika miaka ya mwanzo ulitoka kwa baba yake na Wabaháʼí wawili wa Kiajemi ambao walikuwa wamehudumu kama makatibu wa ʻAbdu'l-Bahá. Kati ya mwishoni mwa 1924 na 1927 alipokea msaada mwanzoni kutoka kwa Daktari John Esslemont, na baaada ya kifo chake cha ghafula mwaka mmoja baadaye, kutoka kwa Ethel Rosenberg, wote wawili wakiwa Wabaháʼí kutoka Uingereza. Alisaidiwa pia katika kazi hii na ndugu zake kadhaa. Katika jaribio la kupunguza mawasiliano, Shoghi Effendi alihimiza jamii za Wabaháʼí kuchapisha na kusambaza nyaraka kwa jamii nyingine, nyaraka iliyotoka Haifa ikijumuisha taarifa kutoka kwa Kituo cha Ulimwengu cha Wabaháʼí na shughuli za Wabaháʼí kote duniani, hivyo kupunguza uhitaji wa Wabaháʼí kumtumia barua kuuliza taarifa. Kama upanuzi wa Kituo cha Ulimwengu cha Wabaháʼí alianzisha Ofisi ya Wabaháʼí huko Geneva, inayowakilisha jamii kwenye majukwaa ya kimataifa na mikutano pamoja na mashirika ya kimataifa ambayo yalikuwa na makao makuu huko Geneva.

Katika miaka ya mwanzo ya ulinzi wake, Shoghi Effendi alilenga katika kuunda na kulea Mabaraza ya Kiroho ya Kitaifa na ya Mahali kwa njia ya kuhamasisha kuenea kwa dini na kama kigezo cha uchaguzi wa Nyumba ya Haki ya Ulimwengu. Mabaraza ya Kitaifa yalichaguliwa kulingana na maagizo ya ʻAbdu'l-Bahá na kufuata taratibu zilizowekwa na Shoghi Effendi, ambaye alichukua jukumu la kufafanua mahitaji ya uchaguzi wao, kuainisha mamlaka yao, kueleza na kutathmini sheria za utendaji wao, na kusimamia utumizi wa vigezo hivi katika hali mbalimbali na mazingira ya kijamii. Mabaraza ya kwanza matatu ya Kiroho ya Kitaifa yaliundwa kwa maagizo ya Shoghi Effendi nchini Uingereza, India na Ujerumani mnamo 1923.[19]

Mnamo 1951 Shoghi Effendi alianza kupanua taasisi za kimataifa za Kibahá'í, kwa kuteua watu kumi na mbili kuwa Mikono wa Hoja kama ilivyopendekezwa kama moja ya majukumu yake na ʻAbdu'l-Bahá katika wosia wake. Katika mwaka huo huo alianzisha Baraza la Kimataifa la Kibahá'í, sekretarieti na chombo cha ushauri ambacho wajumbe wake mwanzoni aliwateua na baadaye walichaguliwa, na ambacho kilichukua jukumu la kuwasiliana na jamii na kushirikiana na serikali ya Israeli. Mnamo 1952 aliteua Mikono wa Hoja saba zaidi, akiongeza wengine wanane mnamo 1957. Mnamo 1954 aliomba Mikono wa Hoja kuteua watu 36 kuhudumu kwenye Bodi za Wasaidizi za bara tano ili kuwasaidia katika kazi yao. Kusudi la kuunda taasisi hizi za kimataifa lilionekana kuwa ni kutoa msaada katika kutekeleza malengo ya upanuzi wa Mpango wa Miaka Kumi Mjuhudi pamoja na maandalizi ya uchaguzi wa Nyumba ya Haki ya Ulimwenguni.[20]

Shoghi Effendi alikuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza Kituo cha Ulimwengu cha Wabaháʼí, mwanzoni kwa kununua jumba huko Bahji, karibu na Akko (zamani ikijulikana kama Acre), ambapo Baha’u’llah aliishi hadi alipoaga dunia mwaka wa 1892, ambapo Kaburi la Baháʼu'lláh limejengwa, na kuzunguka hapo alionunua ardhi ya ziada na kuunda bustani kubwa. Alisimamia ujenzi wa jengo lenye kuba la dhahabu juu ya Kaburi la Báb, aliendeleza ardhi inayozunguka na akajenga jengo la Majalada ya Kimataifa karibu na hapo. Pia alithibitisha mipango iliyohusisha kuanzishwa kwa kituo ambacho kilitarajiwa kukua na kuwa mtandao wa majengo, bustani zilizopangwa vizuri na makaburi, na ambayo ingetambuliwa na Wabaháʼí duniani kote kama kituo cha dini ya Kibaháʼí.[21]

Mnamo 1937 Shoghi Effendi alielekeza Baraza la Kiroho la Kitaifa la Wabahá’í wa Marekani na Kanada kukamilisha sehemu ya nje ya Nyumba ya Ibada ya Kibahá’í huko Wilmette, Illinois, kama moja ya malengo ya Mpango wao wa Miaka Saba.[22] Hii ilikamilika hatimaye mnamo 1943, na uzinduzi wa hekalu ulifanyika Mei 1953.[23] Mnamo tarehe 23 Agosti 1955 Shoghi Effendi alitangaza kwamba Afrika ingejenga Nyumba yake ya kwanza ya Ibada, ambayo ingekaa Kampala, Uganda; hekalu liliwekwa wakfu Januari 1961.[22]

Wakati wa miaka ambayo Shoghi Effendi alikuwa Mlinzi wa dini ya Kibaháʼí, idadi ya waumini iliongezeka hadi zaidi ya 400,000, na mipango aliyoiweka wakati huu ilipilitiza malengo yake. Kabla ya mpango wa kwanza kuanzishwa mwaka 1935 kulikuwa na mabaraza ya kiroho 139 duniani kote, na Wabaháʼí wakiishi katika maeneo 1,034. Idadi hizi ziliongezeka hadi mabaraza ya kiroho 670 na maeneo 2,700 kufikia mwaka wa 1953, na ilikuwa katika mwaka huo ambapo alianzisha Kampeni ya Kimataifa ya Miaka 10 yenye lengo la kueneza imani hii ulimwenguni,[24] ikienea sana katika sehemu za Amerika ya Kusini, Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, India, Asia ya Kusini-mashariki, na visiwa vya Pasifiki.[25] Ingawa Shoghi Effendi alifariki mwaka 1957, kufikia 1963 uwepo wa kijiografia wa dini ya Kibaháʼí duniani ulikuwa umeongezeka hadi maeneo 14,437,[24] ikiwa na mabaraza ya kitaifa 56 na mabaraza ya kiroho ya mahali 3,551.[25]

Nyingine

[hariri | hariri chanzo]

Katika nyanja zisizo za kidini, kabla ya Vita vya Pili vya Dunia alisaidia kazi ya mhifadhi wa misitu Richard St. Barbe Baker ya kurudisha upya misitu ya Palestina, akimtambulisha kwa viongozi wa kidini kutoka dini kuu za eneo hilo, ambao walitoa msaada kwa ajili ya urejeshaji wa misitu.[26]

Tafsiri na maandiko

[hariri | hariri chanzo]
Moja ya barua za mwanzo za Shoghi Effendi kama mwandishi wa Abdu'l-Bahá, 1919

Shoghi Effendi aliandika kwa kiasi kikubwa kwa Kiingereza na Kiajemi, na kama Mlinzi wa dini ya Kibaháʼí Abdu'l-Bahá alimpa jukumu la kufafanua neno la Mungu, akiwa na mamlaka ya kueleza maana na athari za maneno ya Baháʼu'lláh na ʻAbdu'l-Bahá. Kwa kuwa tafsiri za Shoghi Effendi zinachukuliwa kuwa na mamlaka na zisizoweza kubadilishwa, maandiko yake yanachukuliwa kuwa ni sehemu kuu ya kuunda imani ya kisasa ya Kibaháʼí. Pia alikuwa na jukumu muhimu katika kutafsiri maandiko mengi ya Baháʼu'lláh, ikiwa ni pamoja na Maneno Yaliyofichwa mwaka 1929, Kitáb-i-Íqán mwaka 1931, Gleanings mwaka 1935 na Epistle to the Son of the Wolf mwaka 1941.[27] Alitafsiri pia maandiko ya kihistoria kama The Dawn-Breakers.[27] Umuhimu wake sio tu kama mtafsiri, bali pia kama mfasiri wa maandiko ya Kibaháʼí aliyechaguliwa na mwenye mamlaka. Tafsiri zake, kwa hivyo, ni mwongozo kwa tafsiri zote za baadaye za maandiko ya Kibaháʼí.[27]

Idadi kubwa ya maandiko yake yalikuwa katika mtindo wa barua kwa Wabaha'i kutoka sehemu zote za dunia. Barua hizi, ambazo 17,500 zimekusanywa hadi sasa,[27] zinaaminika kuwa na jumla ya kazi 34,000 za kipekee.[28] Zilijumuisha mawasiliano ya kawaida kuhusu masuala ya Wabaha'i duniani kote hadi barua ndefu kwa Wabaha'i wa dunia zikishughulikia mada maalum. Baadhi ya barua zake ndefu na mkusanyiko wa barua zinajumuisha World Order of Baháʼu'lláh, Advent of Divine Justice, na Promised Day is Come.[27]

Barua nyingine zilijumuisha maelezo juu ya imani za Kibaháʼí, historia, maadili, kanuni, utawala na sheria. Pia aliandika maombolezo ya baadhi ya Wabaháʼí mashuhuri. Barua zake nyingi kwa watu binafsi na mabaraza zimekusanywa katika vitabu kadhaa ambavyo vinaonekana kama vyanzo muhimu vya fasihi kwa Wabaháʼí duniani kote.[27] Kitabu pekee alichoandika ni God Passes By, (Mungu Apita) cha mnamo 1944 ili kuadhimisha kumbukumbu ya miaka mia moja ya dini hiyo. Kitabu hicho, ambacho kiko kwa Kiingereza, ni tafsiri ya matukio ya kihistoria ya karne ya kwanza ya Imani za Kibábí na Kibaháʼí. Toleo fupi la lugha ya Kiajemi pia liliandikwa.[27]

Kifo cha ghafla

[hariri | hariri chanzo]
Mahali pa kupumzika pa Shoghi Effendi huko London katika Makaburi ya New Southgate

Kifo cha Shoghi Effendi kilitokea bila kutarajiwa mjini London, tarehe 4 Novemba 1957, alipokuwa safarini huko Uingereza na akaambukizwa Homa ya Asia,[29] wakati wa janga ambalo liliua watu milioni mbili duniani kote, na amezikwa huko katika Makaburi ya New Southgate.[27] Mke wake alituma telegrafu ifuatayo:

Shoghi Effendi mpendwa wa mioyo yote amana takatifu walipewa waumini na Bwana amefariki ghafla mshituko wa moyo usingizini kufuatia homa ya Asia. Nawahimiza waumini wabakie imara washikamane na taasisi ya Mikono iliyolelewa kwa upendo na imara hivi karibuni iliyopewa msisitizo na Mlinzi Mpendwa. Ni umoja wa moyo na umoja wa lengo pekee vinaoweza kushuhudia uaminifu wa kweli wa Mabaraza yote ya Kitaifa kwa Mlinzi aliyefariki ambaye alijitolea kabisa kwa huduma ya Imani.

Walengwa wa hatima ya kumrithi walitazamiwa katika maandiko ya Kibahá'í kuteuliwa kutoka mmoja hadi mwingine. Kila Mlinzi alipaswa kuteuliwa na mtangulizi wake kutoka miongoni mwa watoto wa kiume wa Baháʼu'lláh, ikiwezekana kwa kufuata urithi wa mtoto wa kwanza.[30] Uteuzi ulipaswa kufanywa wakati wa uhai wa Mlinzi na kuridhiwa waziwazi na kikundi cha Mikono wa Hoja.[30] Wakati wa kifo cha Shoghi Effendi, watoto wote wa kiume walio hai wa Baháʼu'lláh walikuwa wametangazwa Wavunjaji wa Agano ama na ʻAbdu'l-Bahá au Shoghi Effendi, wakiacha hakuna mrithi aliyekidhi vigezo aliye hai. Hii ilileta mgogoro mkubwa wa uongozi.[31] Mikono 27 walio hai walikusanyika katika mfululizo wa makongamano sita (au walitia saini mikataba kama hawakuwepo) kuamua jinsi ya kukipita kipindi hiki kilichokosa muongozo ulio wazi.[32] Mikono wa Hoja walipiga kura kwa kukubaliana kwamba ilikuwa haiwezekani kumtambua na kumridhia mrithi halali.[33] Walifanya tangazo tarehe 25 Novemba 1957 la kuchukua usimamizi wa Imani, wakadhibitisha kwamba Shoghi Effendi hakuacha wosia au uteuzi wa mrithi, walisema kuwa hakuna uteuzi ungeweza kufanywa, na kuchagua wanachama tisa kati yao kubaki katika Kituo cha Ulimwengu cha Kibaháʼí huko Haifa kutekeleza kazi za utendaji za Mlinzi (hawa walijulikana kama Wahifadhi).[32]

Uongozi wa Watunzaji

[hariri | hariri chanzo]

Katika ujumbe wa mwisho wa Shoghi Effendi kwa Dunia ya wabaha'i, ulioandikwa Oktoba 1957, aliwataja Mikono wa Hoja ya Mungu, "Viongozi Wakuu wa Jumuiya ya Dunia ya Baháʼu'lláh iliyo mbioni." Kufuatia kifo cha Shoghi Effendi, dini ya Kibaháʼí ilisimamiwa kwa muda na Mikono wa Hoja, ambao walichagua kati yao tisa "Watunzaji" kuhudumu Haifa kama mkuu wa Dini. Walisimamia mabadiliko ya Baraza la Kimataifa la Wabaháʼí kuwa Nyumba ya Haki ya Ulimwengu.[34] Utunzaji huu ulisimamia utekelezaji wa miaka ya mwisho ya maagizo ya Shoghi Effendi ya mpango wa miaka kumi (ambayo yalidumu hadi 1963) ukihitimishwa na kuhamishwa kwa uchaguzi na kuanzishwa kwa Nyumba ya Haki ya Ulimwengu, katika Kongresi ya Dunia ya Kibaha'i ya kwanza mnamo 1963.

Uchaguzi wa Nyumba ya Haki ya Ulimwengu

[hariri | hariri chanzo]

Mwisho wa Mpango wa Miaka Kumi mwaka wa 1963, Nyumba ya Haki ya Ulimwengu ilichaguliwa kwa mara ya kwanza. Iliruhusiwa kutoa maamuzi kuhusu mambo ambayo hayakufunuliwa waziwazi kwenye maandiko. Kama jukumu lake la kwanza la shughuli zake, Nyumba ya Haki ya Ulimwengu ilitathmini hali iliyosababishwa na ukweli kwamba Mlinzi hakuwa ameteua mrithi. Ilibaini kwamba chini ya hali zilizopo, ikizingatia vigezo vya urithi vilivyoelezwa katika Wosia na Agano la ʻAbdu'l-Bahá, hapakuwa na njia halali ya kuteua Mlinzi mwingine.[30][35] Kwa hivyo, ingawa Wosia na Agano la ʻAbdu'l-Bahá umeweka masharti ya mrithi wa Walinzi, Shoghi Effendi anabakia kuwa wa kwanza na wa mwisho kushikilia chombo hiki. Bahá'u'lláh aliona hali katika Kitáb-i-Aqdas ambapo mstari wa Walinzi ungevunjika kabla ya kuanzishwa kwa Nyumba ya Haki ya Ulimwengu, na kwa muda Mikono wa Hoja ya Mungu wangezisimamia shughuli za jamii ya wabaha'i.[36]

  1. Smith 2000, p. 314.
  2. 2.0 2.1 Hartz 2009, p. 13.
  3. 3.0 3.1 Momen 2011.
  4. 4.0 4.1 Smith 2000, p. 315.
  5. Hartz 2009, p. 80.
  6. Hartz 2009, p. 79-84.
  7. Stockman 2022, p. 115.
  8. 8.0 8.1 8.2 Smith 2000, p. 316.
  9. Stockman 2022.
  10. 10.0 10.1 Bergsmo 1991.
  11. Stockman 2022, p. 79.
  12. 12.0 12.1 Rabbani 2000, p. 8.
  13. Stockman 2022, p. 105–106.
  14. Adamson 2007, p. 438.
  15. Stockman 2022, p. 93.
  16. Hatcher & Martin 1986, p. 62.
  17. Adamson 2009, p. 19-21.
  18. Stockman 2022, p. 112.
  19. Stockman 2022, pp. 108–109.
  20. Stockman 2022, p. 114.
  21. Hartz 2009, p. 84.
  22. 22.0 22.1 Stockman 2022, p. 573.
  23. Smith 2000, p. 236.
  24. 24.0 24.1 Hartz 2009, pp. 83–85.
  25. 25.0 25.1 Stockman 2022, p. 507.
  26. St. Barbe Baker 1985.
  27. 27.0 27.1 27.2 27.3 27.4 27.5 27.6 27.7 Smith 2000.
  28. Stockman 2013, pp. 3.
  29. NY Times 1956.
  30. 30.0 30.1 30.2 Smith 2000, pp. 169–170.
  31. Johnson 2020, p. xxx.
  32. 32.0 32.1 Johnson 2020, pp. 8–18.
  33. Momen 2003, §G.2.e.
  34. Smith 2008, pp. 176–177.
  35. Universal House of Justice 1996, p. 14.
  36. Saiedi 2000, pp. 276–277.

Mkusanyo wa ziada

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]