Ronaldo Nazário
Ronaldo Nazário mnamo 2019 | |||
| Taarifa binafsi | |||
|---|---|---|---|
| Jina kamili | Ronaldo Luís Nazário de Lima | ||
| Tarehe ya kuzaliwa | 18 Septemba 1976 | ||
| Mahali pa kuzaliwa | Rio de Janeiro, Brazil | ||
| Kimo | 1.83 m (6 ft 0 in) | ||
| Nafasi anayocheza | Mshambuliaji | ||
| Taarifa za klabu | |||
| Klabu ya sasa | Amestaafu | ||
| Kazi katika klabu | |||
| Miaka | Timu | Mechi† | (Goli)† |
| 1993–1994 | Cruzeiro | 14 | (12) |
| 1994–1996 | PSV Eindhoven | 46 | (42) |
| 1996–1997 | Barcelona | 37 | (34) |
| 1997–2002 | Inter Milan | 68 | (49) |
| 2002–2007 | Real Madrid | 127 | (83) |
| 2007–2008 | AC Milan | 20 | (9) |
| 2009–2011 | Corinthians | 31 | (18) |
| Timu ya Taifa ‡ | |||
| 1993–1994 | Brazil U17 | 7 | (5) |
| 1996 | Brazil U23 | 8 | (6) |
| 1994–2011 | Brazil | 98 | (62) |
| * Senior club appearances and goals counted for the domestic league only and correct as of 9 Agosti 2026. † Appearances (Goals). | |||
Ronaldo Luís Nazário de Lima (alizaliwa 18 Septemba 1976), anajulikana zaidi kama Ronaldo au Ronaldo Nazário, ni mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu kutoka nchini Brazil aliyetambulika kwa kucheza kama mshambuliaji wa kati. Anajulikana kwa majina ya utani kama O Fenômeno ("Kioja") na R9, na anatambulika kwa kiasi kikubwa kama mmoja wa wachezaji bora zaidi katika historia ya mchezo wa mpira wa miguu.[1] Akiwa mshambuliaji aliyebadili mbinu za ushambuliaji duniani, Ronaldo alitwaa tuzo ya FIFA World Player of the Year mara tatu na kushinda Ballon d'Or mara mbili.
Ronaldo alianzia taaluma yake katika klabu ya Cruzeiro kabla ya kuhamia PSV Eindhoven mwaka 1994. Mwaka 1996, alijiunga na Barcelona kwa ada ya usajili iliyovunja rekodi ya dunia, na akiwa na umri wa miaka 20 pekee, alitajwa kuwa mchezaji bora wa mwaka katika tuzo za FIFA, akiwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kutwaa tuzo hiyo. Mwaka 1997, Inter Milan ilivunja tena rekodi ya dunia ya usajili ili kumsajili Ronaldo, na kumfanya kuwa mchezaji wa pili baada ya Diego Maradona kuvunja rekodi hiyo mara mbili. Akiwa na umri wa miaka 21, alitwaa tuzo ya Ballon d'Or ya mwaka 1997 na anasalia kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kushinda tuzo hiyo. Baadaye alijiunga na Real Madrid mwaka 2002 na kutwaa ubingwa wa La Liga, kabla ya kuchezea AC Milan na Corinthians kisha kustaafu soka mwaka 2011.
Katika ngazi ya kimataifa, Ronaldo aliichezea Timu ya taifa ya Brazil mechi 98 na kufunga mabao 62, akiwa mfungaji wa tatu wa muda wote wa timu hiyo. Akiwa na umri wa miaka 17, alikuwa mchezaji mdogo zaidi katika kikosi cha Brazil kilichotwaa ubingwa wa Kombe la Dunia la FIFA 1994. Katika mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA 1998, alishinda tuzo ya FIFA World Cup Golden Ball baada ya kuifikisha Brazil hatua ya fainali. Mwaka 2002, aliiongoza Brazil kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia la FIFA 2002 akishirikiana mastaa wengine kama Ronaldinho na Rivaldo, ambapo alifunga mabao mawili katika mechi ya fainali na kutwaa tuzo ya FIFA World Cup Golden Boot. Pia alitwaa ubingwa wa Copa América mwaka 1997 na 1999.
Maisha ya awali
Ronaldo Luís Nazário de Lima alizaliwa 18 Septemba 1976 katika eneo la Itaguaí, Rio de Janeiro, akiwa mtoto wa tatu wa Nélio Nazário de Lima Sr. na Sônia dos Santos Barata.[2] Wazazi wake walitengana akiwa na umri wa miaka 11, na muda mfupi baadae aliacha shule ili kuelekeza nguvu zake zote katika mpira wa miguu. Alianza kucheza mpira katika mitaa ya Bento Ribeiro na kujiunga na timu za mpira wa ukumbini (futsal), mchezo aliosisitiza kuwa ulimsaidia sana kujenga ujuzi wake uwanjani.
Baada ya kuonyesha uwezo mkubwa katika timu ya vijana ya São Cristóvão, aliyekuwa mchezaji wa zamani wa Brazil, Jairzinho, aligundua kipaji chake na kumfanyia mipango ya kujiunga na klabu ya Cruzeiro akiwa na umri wa miaka 16.[3]
Klabu
Cruzeiro na PSV
Ronaldo alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na klabu ya Cruzeiro 25 Mei 1993. Katika msimu wake wa kwanza, alifunga mabao 44 katika mechi 47, akiiongoza Cruzeiro kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa Copa do Brasil mwaka 1993 na ubingwa wa jimbo wa Campeonato Mineiro mwaka 1994.
Baada ya FIFA World Cup ya 1994, alijiunga na klabu ya PSV Eindhoven kufuatia ushauri wa mchezaji mwenzake Romário. Katika msimu wake wa kwanza nchini Uholanzi, alikuwa mfungaji bora wa Eredivisie akiwa na mabao 30 ya ligi. Licha ya kupata jeraha la goti katika msimu wake wa pili, alimaliza muda wake klabuni hapo akiwa amefunga jumla ya mabao 54 katika michezo 58 na kushinda KNVB Cup mwaka 1996.
Barcelona na Inter Milan
Mwaka 1996, Barcelona ilimsajili Ronaldo kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia ya dola milioni 19.5.[4] Katika msimu wake pekee klabuni hapo (1996–97), alifunga mabao 47 katika mechi 49 za mashindano yote, akiisaidia Barcelona kutwaa UEFA Cup Winners' Cup, Copa del Rey na Supercopa de España, huku akishinda tuzo ya European Golden Shoe na FIFA World Player of the Year wa mwaka 1996.
Mnamo majira ya joto ya mwaka 1997, Inter Milan ilimsajili kwa ada nyingine ya rekodi ya dunia ya dola milioni 27. Akiwa na Inter Milan, alitwaa tuzo ya Ballon d'Or na FIFA World Player of the Year mwaka 1997, na aliisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa UEFA Cup mwaka 1998. Hata hivyo, kipindi chake nchini Italia kiligubikwa na majeraha makubwa ya goti yaliyomweka nje ya uwanja kwa karibu miaka mitatu.
Real Madrid, AC Milan na Corinthians
Baada ya kuonyesha kiwango bora katika FIFA World Cup ya 2002, Ronaldo alijiunga na Real Madrid kwa ada ya euro milioni 46. Akiwa na Real Madrid, alitwaa ubingwa wa La Liga msimu wa 2002–03 na kushinda Ballon d'Or ya mwaka 2002. Alifunga jumla ya mabao 104 katika mechi 177 za klabu hiyo.
Mnamo Januari 2007, alihamia AC Milan na baadaye akarejea Brazil kujiunga na Corinthians mwaka 2009, ambapo alishinda Campeonato Paulista na Copa do Brasil kabla ya kutangaza kustaafu soka mnamo Februari 2011.
Taifa ya taifa
Ronaldo aliichezea Brazil mechi 98 na kufunga mabao 62. Alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani. Katika mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA mwaka 1998 nchini Ufaransa, aliongoza timu hiyo hadi hatua ya fainali lakini alipatwa na tatizo la kiafya saa chache kabla ya mechi ya fainali dhidi ya Ufaransa, ambapo Brazil ilipoteza 3–0.
Katika Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2002 nchini Korea Kusini na Japani, Ronaldo alirejea kwa kiwango cha juu na kufunga mabao nane, ikiwa ni pamoja na mabao mawili kwenye fainali dhidi ya Ujerumani, na kuipatia Brazil ubingwa wao wa tano wa dunia. Katika Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2006 nchini Ujerumani, alifunga bao lake la 15 la mashindano hayo na kuweka rekodi ya mfungaji bora wa muda wote wa mashindano ya Kombe la Dunia kwa wakati huo.
Tuzo na mafanikio

Klabu
- Cruzeiro
- Campeonato Mineiro: 1994
- Copa do Brasil: 1993
- PSV Eindhoven
- KNVB Cup: 1995–96
- Johan Cruyff Shield: 1996
- Barcelona
- Copa del Rey: 1996–97
- UEFA Cup Winners' Cup: 1996–97
- Supercopa de España: 1996
- Inter Milan
- UEFA Cup: 1997–98
- Real Madrid
- La Liga: 2002–03
- Intercontinental Cup: 2002
- Supercopa de España: 2003
- Corinthians
- Campeonato Paulista: 2009
- Copa do Brasil: 2009
Kimataifa
- Brazil
- FIFA World Cup: 1994, 2002; Mshindi wa pili: 1998
- Copa América: 1997, 1999; Mshindi wa pili: 1995
- FIFA Confederations Cup: 1997
Binafsi
- FIFA World Player of the Year: 1996, 1997, 2002
- Ballon d'Or: 1997, 2002
- European Golden Shoe: 1996–97
- Pichichi Trophy: 1996–97, 2003–04
- FIFA World Cup Golden Ball: 1998
- FIFA World Cup Golden Boot: 2002
- Laureus World Sports Award for Comeback of the Year: 2003
- FIFA 100: 2004
- Ballon d'Or Dream Team: 2020
Marejeo
- ↑ Rob Hughes (10 Juni 2014). "On Team of All-Time Greats, Pelé Shines Brightest". The New York Times. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 26 Julai 2020. Iliwekwa mnamo 18 Julai 2025.
{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "Ronaldo's return to glory". BBC Sport. 8 Desemba 2002. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 13 Machi 2009. Iliwekwa mnamo 4 Oktoba 2018.
{{cite news}}: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "Ronaldo awaits coronation". Irish Times. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 19 Agosti 2020. Iliwekwa mnamo 2 Septemba 2018.
{{cite news}}: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ Adams, Tom (14 Aprili 2011). "Ronaldo's record-breaking season". ESPN. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 24 Juni 2021. Iliwekwa mnamo 19 Juni 2021.
{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)