Ptahhotep

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sanamu mbili zinazoaminiwa kuwa za Ptahotep

Ptahhotep (kwa maana ya "Amani ya Ptah ", Ptahhotep I au Ptahhotpe) alikuwa waziri wa farao wakati wa nasaba ya tano ya Misri ya Kale mwishoni mwa karne ya 25 KK na mwanzoni mwa karne ya 24 KK.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Ptahhotep alikuwa msimamizi wa jiji la Sakara na waziri wa kwanza wakati wa utawala wa Farao Djedkare Isesi katika Nasaba ya Tano. Anasifiwa kwa kuandika kitabu Maagizo ya Ptahhotep, ambacho ni mfano wa kwanza wa fasihi inayolenga kufundisha hekima kwa vijana.

Alikuwa na mwana wa kiume aliyeitwa Akhethetep, ambaye pia alikuwa waziri. Ptahhoteb na uzao wake walizikwa Sakara.  

Kaburi la Ptahhotep liko katika jengo la mastaba upande wa kaskazini wa Sakara (Mastaba D62), ambapo alilazwa peke yake. Mjukuu wake Ptahhotep Tshefi, aliyeishi wakati wa utawala wa Farao Unas, alizikwa katika mastaba ya baba yake (mastaba 64). [1] Kaburi lao ni maarufu kwa michoro bora ya ukutani. Pamoja na cheo cha waziri anashikilia nyadhifa nyingine nyingi muhimu, kama vile msimamizi wa hazina, mwangalizi wa waandishi wa hati za mfalme, mwangalizi wa ghala ya nafaka na mwangalizi wa kazi zote za kifalme.

Maagizo ya Ptahhotep[hariri | hariri chanzo]

Kitabu chake kiliitwa Maagizo ya Ptahhotep. Aliandika kuhusu mada kadhaa ambazo zilitokana na dhana kuu ya hekima katika utamaduni wa Misri ya Kale. Maagizo ya Ptahhotep yaliandikwa kama ushauri kwa watu kwa matumaini ya kudumisha "utulivu wa kijamii". Aligusa mambo mengi kuanzia kwenye adabu za kula pamoja mezani na mwenendo mzuri ili kufanikiwa katika mazingira ya mfalme hadi ushauri kwa mume jinsi ya kutunza uzuri wa mke wake. Ptahhotep alishauri pia kuhusu kuepukana na watu wabishi na jinsi ya kujidhibiti. [2]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Grimal, p.79
  2. Fontaine, Carole (1981). "A Modern Look at Ancient Wisdom: The Instruction of Ptahhotep Revisited". Biblical Archaeologist 44 (3): 155–160. 

Bibliografia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]